Wanahabari wahimizwa kuripoti habari za nishati jadidifu
- Watakiwa kuongeza kasi ya kuripoti habari zilizopo katika sekta ya nishati jadidifu ili kuwafunguliwa wananchi fursa mbalimbali ikiwemo ajira na kukuza shughuli za uchumi katika maeneo ya vijijini.
- Ripoti ya Nishati Jadidifu ya Benki ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2015, inaeleza kuwa Takriban tani milioni 1 za mkaa hutumika kwa mwaka nchini.
Dar es Salaam. Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amewataka Wanahabari kuongeza kasi ya kuripoti habari zilizopo katika sekta ya nishati jadidifu ili kuwafungulia wananchi fursa mbalimbali ikiwemo ajira na kukuza shughuli za uchumi katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo maalum ya Wanahabari kwa vitendo katika masuala ya nishati jadidifu (Renewable energy reporting) leo jijini Dar es salaam, Balile amesema nishati jadidifu ina fursa nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuboresha maisha ya wananchi ambao hawajapitiwa na gridi ya taifa.
“Waandishi wa habari wakielimisha jamii tutajikuta tuna watu wanaotengeneza sola, wanaosambaza sola na mwisho wa siku tutajikuta sola nayo inainua kiwanda,” amesema Balile.
Amebainisha kuwa Wanahabari ni chachu ya kusambaza taarifa sahihi kwa wananchi ambapo matumizi ya nishati jadidifu yakiwekewa mkazo yatapunguza changamoto nyingi za wananchi wanazokumbana nazo wakati wa kupata huduma za kijamii ikiwemo afya na maji.
“Mbali ya kuandika habari za nishati jadidifu ni chanzo kingine cha kupunguza umaskini, nchi zilizoendelea wanatumia freezer (majokofu) zinazotumia nishati ya jua,” amesema Balile.
Nishati jadidifu inahusisha umemejua, umemeupepo, gesi, tungamotaka na nishati zingine mbadala.
Katika ufafanuzi wake, Balile amesema Tanzania imeanza mchakato wa kuhimiza matumizi ya nishati jadidifu lakini kasi hiyo haitoshi kwa sababu wastani wa asilimia saba wa kaya nchini zinatumia gesi kupikia.
Mkaa hutumika kwa mwaka nchini jambo linalozidisha ukataji miti na uharibifu wa mazingira ambao unaathiri mfumo mzima wa viumbe hai na shughuli za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo ambayo inategemea mvua kustawisha mazao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Afrika limited, Nuzulack Dausen amesema kuna umuhimu wanahabri kuhabarisha umma juu ya nishati jadidifu ikiwa ni sehemu ya kutekeleza wajibu wao kwa sababu sekta hiyo inagusa maisha ya kila mtu na kila sekta.
“Kuna fursa nyingi katika sekta ya nishati jadidifu ikiwemo kupata matangazo hata kama yanaleta hela kidogo,” amesema Dausen.
Amesisitiza kuwa waandishi wengi huacha habari muhimu kutokana na kukosa mafunzo ya kuandika habari zinazogusa moja kwa moja maisha ya watu hivyo mafunzo maalum ya wanahabari ya nishati jadidifu yatawasaidia kuandika habari zilizofanyiwa na utafiti na zenye matokeo chanya kwa umma.
“Tukiendelea na mafunzo ya namna hii kuna uhakika wa maudhui. Mapato yanayotokana na matangazo yanashuka sana na ni kweli,” amesema Dausen.
Washiriki wa uzinduzi wa mafunzo maalum ya uandishi wa habari za nishati jadidifu. Picha| Daniel Samson.
Mafunzo hayo pia yatawawezesha Wanahabari kutokutegemea maudhui kutoka kwenye makampuni na mashirika pekee bali yatafungua mlango wa kufahamu njia mpya za kidijitali za kuandika habari.
Mratibu wa maabara ya kijamii ya Energy Change Lab, Sisty Basil amesema kuwa asilimia 90 ya watanzania wanatumia kuni na mkaa kama nishati kwa mazoea licha ya ukweli kuwa nishati zingine ni nafuu kuliko mkaa.
Kulinganana maelezo yake, Basil amesema kuna sehemu ambazo Gridi ya Taifa haiwezi kufika hivyo elimu juu ya matumizi ya nishati jadidifu ni muhimu kutolewa kwa maeneo haya kwani itawapatia watu ajira na fursa za kiuchumi.
“Watanzania asilimia 67 wamefikiwa na nishati ya umeme lakini ni asilimia 32.8 tuu ndiyo wameunganishwa na umeme huo,” amesema Basil.
Afisa Mhamasishaji wa Shirika la Hivos Afrika Mashariki, Maimuna Kabatesi amesema matumizi ya kuni na mkaa yana madhara kwa watumiaji wake hasa watoto na wanawake ambao hukumbana na matatizo ya mfumo wa upumuaji na watoto wa kike kukatisha masomo ili kutafuta kuni.
“Watoto wanaondolewa mashuleni ili kwenda kutafuta kuni. Nishati jadidifu inatoa mbadala kwa mapishi na hata umeme” amesema Kabatesi
Mafunzo Maalum ya nishati jadidifu yazinduliwa
Katika kuhakikisha wanahabari wana maarifa kuhusu sekta hiyo, Hivos Afrika Mashariki (Hivos East Africa) kwa kushirikiana na kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa Ltd wamezindua mafunzo maalum ya wanahabari kwa vitendo katika masuala ya nishati jadidifu (Renewable energy reporting) ili kuzalisha habari za nishati zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na kwa vyombo habari husika.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kati ya Desemba 2018 na Mei 2019. Wanahabari watakaochaguliwa pia watakuwa na fursa ya kuhudhuria tamasha maalum la nishati kwa wanahabari (Energy Change Safari for Journalists) kwa siku tano mkoani Arusha.
Fomu ya maombi ya mafunzo inapatikana:
Safari hiyo itafanyika kati ya Novemba 26 hadi Desemba mosi, 2018 na itaratibiwa kwa ushirikiano na maabara ya kijamii ya Energy Change Lab ambayo ni programu ya mafunzo na kiunganishi cha wadau kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nishati.
Ili kuhakikisha maarifa yatakayopatikana katika mafunzo hayo yanatumika ipasavyo, wanahabari watapatiwa ruzuku ya kuwawezesha kufanya uchunguzi wa kihabari katika maeneo watakayochagua na kuzalisha habari zilizofanyiwa utafiti wa kina kuhusu nishati jadidifu.
Usaili wa washiriki utazingatia wasifu, motisha uliyonayo, usawa wa kijinsia, taaluma, aina ya chombo cha habari na eneo unalotokea hapa nchini. Muombaji unapaswa kuwa na umri kati ya miaka 18 na 45. Tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni Oktoba 14, 2018.
Kwa swali lolote kuhusu maombi ya kujiunga na mafunzo haya, tafadhari wasiliana na Nuzulack Dausen kupitia barua pepe; ndausen@nukta.co.tz au kupitia simu ya mkononi +255 714382 434 na Daniel Mwingira kupitia danny@nukta.co.tz na kwa njia ya simu +255 716 731 383.