Waandishi Nukta Africa vinara tuzo za EJAT 2021

May 28, 2022 1:55 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Mariam John na Daniel Samson (kushoto) mara baada ya kutangazwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2021. Picha| Tulinagwe Malopa.


  • Ni Daniel Samson na Mariam John.

Dar es Salaam. Waandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Mariam John na Daniel Samson wametangazwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2021.

Hii ni mara pili kwa waandishi wa Nukta Africa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo hizo za  juu katika tasnia ya habari nchini ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Mariam John ameshinda tuzo ya uandishi wa habari za gesi, mafuta na uchimbaji madini katika upande wa habari za vyombo vya habari vya mtandaoni.

Mariam anayeripoti habari zake kutoka mkoani Mwanza amesema ni mara ya kwanza kuwania tuzo hizo na kufanikiwa kuwa mshindi wa kwanza katika kipengele hicho.

“Sikutegemea kwa kweli kuwa mshindi, nitafanya kazi kwa bidii ili kuboresha uandishi wangu,” amesema Mariam muda mfupi baada ya kupata tuzo hiyo.

Samson, mhariri wa tovuti ya habari ya Nukta (www.nukta.co.tz) amekuwa mshindi wa pili katika tuzo za uandishi wa habari za takwimu (Data journalism) na tuzo ya uandishi wa habari ya utawala bora na uwajibikaji.

Samson na Mariam ni sehemu ya waandishi wa habari 61 walioteuliwa kuwania tuzo hizo kutoka katika kazi 598 za wanahabari waliotuma kazi zao.

Kati ya wateule hao, tisa wanatoka televisheni, redio (8), magazeti (32) na mtandaoni ni 12.

“Nimefarijika kuwa mshindi wa pili, safari ilikuwa ndefu, tuzo za leo zimeniongezea nguvu ya kufanya kazi kwa bidii ili kutoa mchango wangu kwa jamii,” amesema Samson.

Menejimenti ya Nukta Africa imesema inafarijika kuona habari zinazochapishwa na Nukta Habari na Nukta Tv zinathaminiwa kiasi cha kushinda tuzo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema wataendelea kutoa mafunzo kwa wanahabari na kuwekeza zaidi katika habari zenye tija na zinazoboresha maisha ya watu. 

“Malengo yetu ni kwamba habari si tu zipate tuzo bali ziboreshe maisha ya Watanzania katika kila nyanja, iwe uchumi, biashara, afya, elimu…tunataka kuona watu wanasonga mbele kimaisha kwa sababu ya habari au makala zetu,” amesema Dausen ambaye ni mwanahabari mwandamizi na mkufunzi wa masuala ya habari za takwimu, dijitali na biashara. 


Soma zaidi:


Nukta Africa hujihusisha na kufanya utafiti wa masuala ya habari, kutoa mafunzo kwa wanahabari na kuzalisha habari za takwimu za kidijitali kupitia Nukta Habari, Nukta TV, Jiko Point na Nukta the Podcast.

Tuzo za EJAT mwaka huu zimetolewa leo Mei 28, 2021 jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyesema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wanahabari. 

Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuunga mkono tuzo hizo ili kutambua kazi za waandishi wa habari wanaofanya vizuri huku akiwataka waandaaji kuongeza vipengele vinavyogusa maendeleo ikiwemo zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mshindi wa jumla wa tuzo hizo ni Masekepa Natisa Masekepa kutoka kituo binafsi cha televisheni cha ITV. 

Mshindi wa tuzo ya maisha

Katika hafla ya utoaji tuzo hizo, Majaliwa amemkabidhi   Tuzo ya Maisha ya Mafanikio katika Uandishi wa Habari (Laja) kwa mwaka 2022 mwandishi mkongwe Ndimara Tegambwage.

Ndimara, ambaye amefanya kazi na vyombo mbalimbali vya habari nchini na nje, ni mwandishi wa tano  kushinda tuzo hiyo tangu zilipoanza kutolewa mwaka 2019 ambapo amekabidhiwa zawadi ya hundi ya Sh10 milioni.

Tuzo za EJAT hutolewa kwa waandishi wa habari wa magazeti, redio, televisheni na vyombo vya habari vya mtandaoni ambazo huwatambua waandishi waliofanya vizuri katika tasnia hiyo kila mwaka.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV