Waandishi wa habari Nukta Africa kuwania tuzo za Ejat 2022
- Ni pamoja na Daniel Samson na Lucy Patrick
- Kilele kufanyika Julai 22, 2023 Mlimani City jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam.Waandishi wa habari wanne kutoka Kampuni ya Habari na Teknolojia ya Nukta Africa wameingia katika kinyang’anyiro cha tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zitakazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Julai 22, mwaka huu.
Waandishi hao ni pamoja na Daniel Samson ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mafunzo na Lucy Patrick ambaye ni mwandishi wa habari kutoka Nukta Africa, Herimina Mkude pamoja na na Suleiman Omary Mwiru.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ejat mwaka 2022 Kajubi Mukajanga aliyekuwa akitangaza wateule hao jijini Arusha leo Ijumaa, Juni 23,2023 amesema waandishi 91 pekee ndio wameteuliwa kati ya 728 waliowasilisha kazi zao.
Kati ya waandishi hao 36 wanaandikia magazeti, 27 mitandao ya kijamii na 15 ni kutoka redioni na huku 15 wakitokea katika televisheni..
“Washindi wa tuzo kujulikana rasmi Julai 22, katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Haki Jinai,” amesema Mukajanga.
Hii ni mara ya nne Nukta Africa kuingiza washindani katika tuzo za Ejat ambapo kwa mwaka 2022 ndio wameingiza wateule wengi zaidi yaani wanne.
Mwaka 2021 mwandishi wa Nukta Africa Mariam John aliibuka kinara katika uandishi wa habari za madini, mafuta na gesi huku Daniel Samson akiwa mshindi wa pili wa uandishi wa habari za takwimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Oparesheni na Uendeshaji wa Nukta Afrika Maphosa Banduka amewapongeza waandishi waliochaguliwa kuwania tuzo hizo na kuongeza kuwa tuzo hizo ni kichocheo kwa waandishi kuendelea kuzalisha maudhui bora yatakayoisaidia jamii kufanya maamuzi sahihi.
“Hii ni heshima kubwa sana kwetu kama chombo cha habari, tuzo hizi zitaendelea kuwa kichocheo cha hamasa kwa waandishi na katika kuongeza weledi kwenye utayarishaji wa maudhui ambayo yanazisaidia jamii zetu kufanya maamuzi sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali,” amesema Maphosa.
Aidha, Lucy Samson ambaye ni mara yake ya kwanza kuteuliwa kuwania tuzo hizo ameiambia Nukta Habari kuwa kuteuliwa katika nafasi hiyo kumempa moyo na kumfanya aongeze bidii katika utendaji wa majukumu yake.
Latest