Nukta Afrika yatoa wanahabari wawili kuwania tuzo za EJAT 2021
- Ni Mariam John na Daniel Samson.
- Tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zitatolewa Mei 28, 2022.
Dar es Salaam. Waandishi wa habari Marium John na Daniel Samson wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa ni miongoni mwa wanahabari 60 wa Tanzania walioteuliwa kuwania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari (EJAT) kwa mwaka 2021.
Hii ni mara pili kwa Nukta Africa kutoa waandishi wa habari kuwania tuzo hizo za juu katika tasnia ya habari ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Tuzo hizo ambavyo hujumuisha vyombo vya habari vyote vikiwemo vya mtandaoni zinazohamasisha uandishi wenye hamasa kwa jamii zimegawanyika katika vipengele 20 kikiwemo kipengele cha habari za takwimu.
Samson ambaye ni mhariri wa tovuti ya Nukta (www.nukta.co.tz) ameteuliwa kwa mara ya pili ambapo katika tuzo za mwaka 2020 aliibuka mshindi katika kipengele cha habari za elimu zinazochapishwa mtandaoni.
“Kwangu ni heshima kubwa kuteuliwa tena kuwania tuzo hizo kwa sababu zinanipa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii ili kutoa mchango kwenye jamii hasa watu wanaoishi vijiji ambao wamekuwa wakibua na kutatua changamoto zao,” amesema Samson.
Mariam anayeripoti habari zake kutoka mkoani Mwanza anakuwa miongoni mwa wanawake 28 walioteuliwa kuwania tuzo hizo sawa na asilimia 47 ya wateule wote.
Mariam, ambaye huandika habari za wanawake, afya na uchumi, amesema kuteuliwa katika tuzo hizo ni kama ndoto kwake kwani alikuwa hategemei kufikia hatua hiyo.
“Hii ni mara yangu ya kwanza sikutegemea kuwa naweza kufikia hatua hii ya kuteuliwa kuwania tuzo hizi kwangu ni heshima kubwa, namshukuru Mungu.” amesema Mariam.
Soma zaidi:
Wateule hao 60 wametoka katika kundi la wanahabari 598 waliotuma kazi zao ili kuwania kuteuliwa katika tuzo hizo ambapo kati yao, tisa wanatoka televisheni, redio (8), magazeti (31) na mtandaoni ni 12.
Tuzo za EJAT mwaka huu, kwa mujibu wa MCT, zitatolewa Mei 28, 2021 katika ukumbi wa Serena hoteli jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema tuzo za mwaka huu zimekuwa na hamasa kubwa kutoka kwa wanahabari, jambo lililowafanya majaji kutumia siku tisa badala nane kupitia kazi na kuwachagua wateule 60.
Mukajanga aliyekuwa akizungumza leo Mei 19, 2022 jijini Dar es Salaam amesema pia tuzo hizo wameshuhudia waandishi wa habari wa mtandaoni wakijitokeza kwa wingi, jambo linaloashiria kuimarika kwa uandishi wa habari za mtandaoni Tanzania zenye manufaa kwa jamii.
“Ukitazama statistics (takwimu) za wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari utagundua wanawake ni wachache zaidi hivyo kwa idadi hii inapaswa wapongezwe,” amesema.
Miaka ya nyuma ilikuwa ni ngumu kuona habari za mtandaoni zikipewa kipaumbele katika tuzo mbalimbali licha ya kuwa wapo wanahabari wanaofanya kazi nzuri.
Samson amewasihi waandishi wa habari za mtandaoni kujituma kwa kuchapisha maudhui yenye mchango kwa jamii badala ya kusambaza uzushi au kufanya kazi kwa haraka haraka ili kuvuta wasomaji na watazamaji.
“Ni wakati sasa waandishi wa habari za mtandaoni kuzingatia weledi na taaluma ya uandishi ili kuripoti kwa usahihi, kwa kina na uchambuzi habari mbalimbali kwenye jamii hasa zile zinagusa maisha ya watu,” amesema Samson.
Nukta Africa ndani ya miaka minne tangu ianzishwe wanahabari wake na kampuni imeshinda tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi hususan katika habari za takwimu na matumizi bora ya kidijitali katika vyombo vya habari.
Kampuni hiyo hutoa pia mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi bora wa takwimu na kidijitali huku waandishi waliopata mafunzo hayo nao wakizoa tuzo mbalimbali katika vipindi tofauti nchini.
Tangazo:

Ni fursa mpya kwa wanahabari
Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema anafurahi kuona kuwa MCT wameona na wanakubali ubora wa kazi zao kwani vyombo vya habari vya mtandaoni vimekuwa haviaminiki
“Hii ni heshima kubwa kwa Nukta Africa na uandishi wa habari mtandaoni Tanzania, tunaamini tutatoboa ili tuendelee kuchapisha maudhui yanayogusa maisha ya watu kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka yote tangu kampuni ianzishwe,” amesema Dausen.
Dausen amesema tuzo hizi ni fursa mpya kwa wanahabari kuzalisha habari zenye mashiko zenye kuacha alama zitakazo badilisha jamii.
Waandishi wengine waliotajwa kuwania tuzo hizo wametoka katika magazeti, redio, vyombo vya habari za mtandaoni na televisheni mbalimbali nchini ikiwemo ITV, Star TV, Mwananchi na The Chanzo.