Waandishi Nukta Africa wang’ara tuzo za Ejat 2022

July 22, 2023 5:51 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Daniel Samson, Suleiman Mwiru, Hermina Mkude na Lucy Patrick
  • Waibuka na ushindi katika vipengele sita, vinne wanyakua tuzo.
  • Hii ni mara ya tatu Nukta Africa kuibuka vinara katika tuzo hizo kubwa Tanzania

Dar es Salaam. Kwa mara nyingine tena waandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa wameibuka vinara kwa kupata tuzo nne katika tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Ejat zilizotolewa hii leo Julai 25,2023.

Waandishi Daniel Samson, Lucy Patrick, Suleiman Mwiru pamoja na Herimina Mkude wametangazwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2022.

Hii ni mara tatu kwa waandishi wa Nukta Africa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo hizo za  juu katika tasnia ya habari nchini ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Tuzo nne zanyakuliwa

Daniel Samson ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Nukta Africa ameshinda tuzo mbili ambazo ni ya uandishi wa habari za uchumi, biashara na fedha pamoja na tuzo ya habari za tozo na kodi katika upande wa vyombo vya habari vya mtandaoni.

Samson ambaye mwaka 2021 alishika nafasi ya pili katika tuzo za uandishi wa habari za takwimu na uwajibikaji amebainisha kuwa ushindi huo ni hatua kubwa kwake kwani unathibitisha kuwa amepata nafasi ya kuitumikia jamii.

“Nimefarijika kwamba kuna watu wanaotambua kazi ya waandishi wa habari inayofanyika, ni wasaa mzuri wa mimi kufanya kazi kwa bidii kuitumikia jamii yangu na kuhakikisha wanapata maendeleo kupitia kalamu yangu,” amesema Samson.

Daniel Samson alipokuwa akipokea tuzo yake katika hafla ya tuzo za Ejat iliyofanyika Julai 22, 2023. PichalDaniel Samson/Nukta

Kwa upande wake Lucy Samson ambaye ameshiriki tuzo hizi kwa mara ya kwanza na kushika nafasi ya pili katika tuzo za uandishi wa habari za data amesema kuteuliwa katika nafasi hiyo kumempa moyo na kumfanya aongeze bidii katika utendaji wa majukumu yake.

Nukta imenyakua tuzo nyingine mbili kupitia kwa mwandishi wake Suleiman Mwiru ambaye ameshinda tuzo ya mwandishi bora wa habari za elimu pamoja na habari bora ya teknolojia kwa vyombo vya mtandaoni.

Mwiru ambaye kwa sasa yupo nchini Ujerumani amewashukuru viongozi wa Nukta Afrika pamoja na wafanyakazi wote  kwa ushirikiano walioutoa na kufanikisha kupatikana kwa tuzo hiyo.

Mwandishi mwingine Hermina Mkude ameshika nafasi ya tatu katika kipengele cha habari za mazingira na utunzaji wa maji.

Washindi hao wamepatikana kutoka kwa wateule 91 walioteuliwa kati ya waandishi 728 waliowasilisha kazi zao.

Kati ya waandishi hao 36 wanaandikia magazeti, 27 mitandao ya kijamii na 15 ni kutoka redioni na huku 15 wakitokea katika televisheni.

Menejimenti yanena

Menejimenti ya Nukta Africa imesema inafarijika kuona habari zinazochapishwa na Nukta Habari na Nukta Tv zinathaminiwa kiasi cha kushinda tuzo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema miongoni mwa misingi ya kampuni hiyo ni kuandaa habari bora, zenye uhakika na maslahi kwa umma, ambazo zitasaidia kuboresha maisha ya watu hivyo ushindi wa tuzo hizo ni sehemu ya mchango wa Nukta kutambulika.

“Ushindi wetu mkubwa si yule aliyeshinda tuzo bali ni pale ambapo mwananchi wa kawaida anaponufaika na kazi zetu za uandishi, kama kukuza biashara, au kuepuka magonjwa hiyo ndio tuzo ya msingi tunayipigania,” amesema Dausen.

Dausen amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi kwa ubora siku zote kwa kusimamia misingi ya habari na kutoa mafunzo kwa waandishi pamoja na vyombo vya habari kuzalisha maudhui yenye tija kwa jamii.

Hii ndio Nukta

Nukta Africa hujihusisha na kufanya utafiti wa masuala ya habari, kutoa mafunzo kwa wanahabari na kuzalisha habari za takwimu za kidijitali kupitia Nukta Habari, Nukta TV, Jiko Point , Nukta Fakti na Nukta the Podcast.

Hivi karibuni Nukta imezindua jukwaa la mtandaoni la Kozica mahususi kwa ajili ya mafunzo kwa wanahabari kujiongezea ujuzi katika masuala mbalimbali.

Kwa miaka mitano sasa kampuni hii imekuwa ikizalisha washiriki na washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari nchini Tanzania kupitia mafunzo ya uandishi wa habari za takwimu, habari za mtandaoni pamoja na uthibitishaji wa habari.

Kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake mwaka 2018 Nukta Afrika imepata tuzo nne kati ya sita ilizowania na kuibuka mshindi wa pili na wa tatu katika baadhi ya vipengele.

Enable Notifications OK No thanks