Waandishi wa Nukta Africa wateuliwa kuwania tuzo EJAT 2020
- Ni Rodgers George na Daniel Samson ambao walishawahi kushinda tuzo nyingine za uandishi wa habari za takwimu za NBS.
- Waandishi hao wanawania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari zitakazo tolewa Septemba 10, 2021 jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Waandishi wa habari wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa, Rodgers George na Daniel Samson wameteuliwa kuwa miongoni mwa waandishi 59 nchini Tanzania wanaowania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari mwaka 2020.
Tuzo hizo zenye hazi ya juu katika tasnia ya habari hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na zinalenga kuhamasisha uandishi wenye hamasa kwa jamii katika vipengele 19 mbalimbali ikiwemo kipengele cha habari za takwimu.
Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) mwaka huu, kwa mujibu wa MCT, zitatolewa Septemba 10, 2021 katika ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2019 Mhariri wa habari wa Nukta Africa, Daniel Samson aliibuka mshindi wa kwanza wa tuzo za uandishi bora wa takwimu zinazolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) akiwa ni mwandishi wa kwanza Tanzania kupata tuzo hiyo. Baadae mwaka 2020 Rodgers George akaibuka mshindi wa tatu katika tuzo hizo.
Ni Daniel Samon (Kushoto) na Rodgers George (Kulia) ambao wametangazwa kuwania tuzo za umahiri wa uandishi wa habari kwa mwaka 2020 kutoka Nukta Africa. Picha | K15
George, ambaye huandika habari za teknolojia na jamii, amesema kuteuliwa katika tuzo hizo kunampa kujiamini kuwa licha ya kuwapo kwa miaka michache katika tasnia ya habari bado habari zake zina mchango mkubwa kwa taifa.
“Sikutegemea kama mwandishi wa habari mdogo kama mimi ninaweza hata kupata nafasi ya ‘nomination’ (kuteuliwa) kwenye mashindano haya kitaifa. Nomination hii inanisahihisha kuwa licha ya udogo nilionao kama mwandishi, kazi zangu zinaonekana,” amesema George.
Miaka ya nyuma ilikuwa ni ngumu kuona habari za mtandaoni zikipewa kipaumbele katika tuzo mbalimbali licha ya kuwa wapo wanahabari wanafanya kazi nzuri.
Samson amewasihi waandishi wa habari za mtandaoni kujituma kwa kuchapisha maudhui yenye mchango kwa jamii badala ya kusambaza uzushi au kufanya kazi kwa haraka haraka ili kuvuta wasomaji na watazamaji.
“Ni wakati sasa waandishi wa habari za mtandaoni kuzingatia weledi na taaluma ya uandishi ili kuripoti kwa usahihi, kwa kina na uchambuzi habari mbalimbali kwenye jamii hasa zile zinagusa maisha ya watu,” amesema Samson.
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) inamilikiwa na Nukta Africa na ndani ya miaka mitatu na nusu tangu ianzishwe wanahabari wake na kampuni imeshinda tuzo mbalimbali za nje hususan katika habari za takwimu na matumizi bora ya kidijitali katika chumba cha habari.
Kampuni hiyo hutoa pia mafunzo kwa wanahabari kuhusu uandishi bora wa takwimu na kidijitali huku waandishi waliopata mafunzo hayo nao wakizoa tuzo mbalimbali katika vipindi tofauti nchini.
Ni safari yenye matumaini
Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema wataendelea kuwa mfano katika tasnia ya habari kwa kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi zinazochochea maendeleo kupitia maudhui ya mtandaoni.
“Hii ni heshima kubwa kwa Nukta Africa na uandishi wa habari mtandaoni Tanzania, tunaamini tutatoboa ili tuendelee kuchapisha maudhui yanayogusa maisha ya watu kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka yote tangu kampuni ianzishwe,” amesema Dausen.
Waandishi wengine waliotajwa kuwania tuzo hizo wametoka katika magazeti, redio na televisheni mbalimbali nchini ikiwemo Azam TV, Mwananchi, The Citizen na Shirika la Habari la kimataifa la DW.
Dausen amesema anatarajia kuona wanahabari wengi wa mtandaoni wakiongeza weledi huku watoa tuzo wakiwapatia kipaumbele kama vyombo vingine vya habari.