Vodacom, Smart Lab wazindua programu ya kuwainua vijana kiuchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu ya Vodacom Accelerator jana. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Smart Codes, Edwin Bruno pamoja na Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia. Picha|Vodacom.
- Programu hiyo mpya iliyozinduliwa jana itawawezesha wajasiriamali chipukizi na wale wanaoendelea kuanzisha biashara zenye faida zinazoweza kuwaingizia kipato cha kujikimu kimaisha.
- Lengo kuu la kusaidia wajasiriamali wanaochepukia katika soko la simu, mawasiliano na teknolojia katika taasisi mbalimbali zikiwemo za kifedha, habari, afya, elimu pamoja na biashara ya mitandao (E-commerce).
- Vodacom imewekeza Sh344.8 milioni kufanikisha malengo ya programu hiyo.
Dar Es Salaam. Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania na kituo cha ubunifu cha Smart lab wamezindua programu mpya ya kuwawezesha wajasiriamali chipukizi na wale wanaoendelea kuanzisha biashara zenye faida zinazoweza kuwaingizia kipato cha kujikimu kimaisha.
Program hiyo iliyozinduliwa jana (Septemba 13, 2019) inafanyika kila mwaka ikiwa na lengo kuu la kuwasaidia wajasiriamali wanaochipukia katika soko la simu, mawasiliano na teknolojia katika taasisi mbalimbali zikiwemo za kifedha, habari, afya, elimu pamoja na biashara ya mitandao (E-commerce).
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi amesema ushirikiano uliopo baina ya Vodacom Tanzania na kampuni ya Smart Codes kama moja ya kiungo cha Smart Lab ni hatua muhimu na nzuri katika kuwawezesha na kuwasaidia wajasiriamali hasa vijana kijikwamua kiuchumi katika kutatua matatizo na kuleta maendeleo.
“Kampuni ya Vodacom mara zote inakusaidia kuleta mabadiliko endelevu yenye manufaa kwa jamii ambako tunaendesha shughuli zetu sambamba na mtazamo wa mkakati wetu wa kibiashara na programu ya “Vodacom Accelerator” inakusaidia kuthibitisha suala hilo”, amesema Hendi.
Amesema Vodacom imeshirikiana na Smart Lab, kituo maarufu cha ubunifu ambacho kinakusudia kuleta matokeo halisi ambayo yatabadilisha mwelekeo wa ubunifu wa mifumo ya kiuchumi Tanzania.
Soma zaidi:
- Bosi Vvodacom Tanzania afikishwa mahakamni kujibu mashataka uhujumu uchumi
- Hisham Hendi kuipaisha Vodacom Tanzania?
- Kigogo wa Safaricom kuiongoza Vodacom Tanzania
Hiyo itakuwa ni fursa kwa wafanyabiashara wanaoanza na wavumbuzi katika vigezo vya kiteknolojia vilivyochaguliwa kuonyesha bidhaa zao na kunufaika kutokana na programu hiyo.
Pia watakaoingia katika programu hiyo watapata ushauri, msaada wa kitaalamu, masoko na fursa ya kupata nafasi ya kuwa karibu na mtandao mkubwa wa washirika wa kampuni za Vodacom na Smart Lab na kuweza kufanya majaribio na kupata uzoefu wa masuluhisho yao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Smart Codes, Edwin Bruno amesema progamu hiyo inaenda sambamba na mkakati wa kampuni yake wa kuwasaidia vijana wanaotumia teknolojia ya dijitali kunufaika kiuchumi.
“Tunafuraha kuwa sehemu ya program ya Vodacom Accelerator na kushirikiana na Vodacom, kwa pamoja tunatumaini kutengeneza jukwaa la kipekee kwa ajili ya vijana wenye ari katika teknolojia,”amesema Bruno.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau kutoka serikalini, wawekezaji, vituo vya uvumbuzi, taasisi za kifedha, mashirika, wafanyabiashara chipukizi, washirika wa maendeleo, Mabalozi na watendaji wengine katika teknolojia.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia amesema katika kutambua mchango mkubwa wa program hiyo, Vodacom imewekeza Zaidi ya dola za Marekeani 150,000 (Sh344.7 milioni) katika mpango huo ili kusaidia vijana kielimu na utaalamu kutimiza malengo yao kibiashara.
Latest