Bosi Vodacom Tanzania afikishwa mahakamani kujibu mashtaka uhujumu uchumi
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, Hisham Hendi. Picha|Mtandao.
- Ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Hisham Hendi na wenzake nane ambao wanakabiliwa na mashtaka 10 kuisababishia Serikali hasara ya Sh5.8 bilioni.
- Mashtaka hayo ni pamoja na kuongoza mtandao wa uhalifu, kuingiza na kuendesha mitambo ya mawasiliano ya kielektroniki bila kuwa na leseni.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania, Hisham Hendi na wenzake nane wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka 10 yakiwamo kuingiza mitambo ya mawasiliano ya kielektroniki bila kuwa na leseni na kuisababishia Serikali hasara ya Sh5.8 bilioni.
Washtakiwa hao wamefikishwa katika mahakama hiyo leo ( April 3, 2019) na kusomewa mashtaka hayo katika kesi ya uhujumu uchumi namba 20/2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambayo imesomwa kwa mara ya kwanza leo ni Meneja Uendeshaji Biashara katika kampuni ya Inventure Mobile limited, Ahmed Hashim Ngassa; Mtaalam wa Tehama, Brian Keneth Lusiola; Mkuu wa Uhakiki wa Mapato wa Vodacom Tanzania, Joseph Gichuchi Nderitu na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Vodacom Tanzania, Olaf Peter Mumburi.
Wengine ni Mkuu wa Mauzo wa Vodacom Tanzania, Joseph Muhere na Meneja wa Fedha wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Bonzo.
Pia katika kesi hiyo kampuni mbili za Vodacom Tanzania na Inventure Mobile Tanzania Limited (Tala Tanzania) nazo zimejumuishwa katika kesi hiyo.
Upande wa jamhuri umesema watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwa ni pamoja na kuongoza mtandao wa kihalifu kinyume na taratibu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuingiza nchini, kufunga na kuendesha mitambo ya mawasiliano ya kielektroniki bila kuwa na leseni.
Pia matumizi mabaya ya mifumo ya kimtandao, kutumia vifaa vya kielektroniki visivyothibitishwa vilivyounganishwa na mfumo wa huduma wa mawasiliano ya kielektroniki.
Soma zaidi:
Baada ya kusomewa tuhuma zinazowakabili, watuhumiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote na wamerudishwa rumande wakati wakisubiri kurudi mahakamani Aprili 17, 2019 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Huenda kitakuwa ni kipindi kigumu kwa Hendi ambaye amekaa katika nafasi yake kwa majuma mawili tu tangu alipoteuliwa rasmi na Bodi ya Wakurugenzi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Machi 17 mwaka huu baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Septemba 2018.
Kutokana na kesi hiyo inayowakabili vigogo hao wa Vodacom Tanzania, uongozi wa kampuni hiyo umewahakikishia wateja wake kuwa kesi hiyo haitaathiri mwenendo wa utoaji huduma na hatua zimechukuliwa kuhakikisha shughuli za utendaji wa kampuni zinaendelea kama kawaida bila kuingiliwa.
“Tutawapa taarifa ya kinachojiri kulingana na muendelezo wa suala hili,” imeeleza sehemu ya taarifa ya Vodacom iliyotolewa katika tovuti ya kampuni hiyo yenye wateja zaidi ya milioni 14 wa simu za mkononi.