Tume ya Chande yapendekeza katiba mpya kabla ya 2028

April 23, 2026 6:30 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Tume yapendekeza katiba mpya mapema ili itumike wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2030.

Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuanzisha mchakato wa katiba mpya ifikapo mwaka 2028 baada ya kubainika kuwa ni miongoni mwa vyanzo vilivyochochea vurugu za wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 uliosababisha watu 518 kupoteza maisha. 

Pendeko hilo limetolewa leo na ripoti ya tume ya rais ya kuchunguza matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mwaka jana ulioshuhudia maelfu ya vijana wakiandamana maeneo mbalimbali nchini wakidai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi na kuimarishwa hali ya kiuchumi. 

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman amesema katika mapendekezo yao ni muhimu katiba mpya ipatikane mwaka 2028 ili iweze kutumika katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2029 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2030. 

Katika pendekezo hilo, Chande amesema wanapendekeza Serikali iunde kamati ya wataalamu wa katiba ambayo itakuwa na jukumu la kupitia katiba iliyopo, rasimu ya katiba ya tume ya mabadiliko ya katiba, katiba pendekezwa ya mwaka 2014 na ripoti mbalimbali zinazohusu masuala ya katiba.

Mchakato wa katiba mpya ulikwama mwaka 2014 na kwa zaidi ya miaka 10 vyama vya upinzani na wadau wa haki za binadamu wamekuwa wakiitaka Serikali ianzishe mchakato wa katiba mpya ili kuimarisha mfumo mzima wa kidemokrasia ukiwemo wa uchaguzi. 

Tume hiyo, iliyokosolewa vikali na vyama vikuu vya upinzani vya Chadema na ACT-Wazalendo, imewasilisha mapendekezo hayo baada ya kukamilisha kazi ya siku 153 kuchunguza kilichojiri katika vurugu hizo mbaya kuwahi kurekodiwa nchini zilizosababisha majeruhi 2,390. 

Chande amesema tume hiyo inapendekeza pia kuundwa kwa tume ya maridhiano ya kitaifa chini ya mamlaka ya Rais, itakayoratibu majadiliano ya kitaifa kuhusu masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Akiwasilisha mapendekezo ya tume kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam, Chande amesema tume hiyo inapendekeza kutengwa kwa siku maalumu ya maombolezo ya kitaifa kuwakumbuka Watanzania waliopoteza maisha katika matukio hayo katika maeneo mbalimbali nchini. 

Licha ya kumaliza kazi hiyo iliyokuwa imepewa na Rais Samia, Chande amesema kuna mambo ya kijinai waliyabaini yanayohitaji kuundwa kwa tume nyingine ya jinai itakayochunguza matukio mahsusi ya kijinai. 

“Tume hiyo itakuwa na jukumu la kupeleleza na kufuatilia masuala mahususi yanayohitaji upelelezi zaidi ili kushughulikia tuhuma, kubaini wahusika wakuu, waliopanga, walioratibu, waliofadhili ghasia (Masterminds), kushughulikia masuala tatanishi ya vifo na pia maiti ambazo hazijulikani zilizopo,” amesema Chande. 

Serikali imetakiwa kuandaa mkakati maalum wa kutoa huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa waathirika, pamoja na kuhakikisha majeruhi wanapatiwa matibabu stahiki bila malipo ikiwemo vifaa saidizi kama viungo bandia.

Chande amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa maadili ya viongozi, utekelezaji wa sheria za vijana, kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, ajira, pamoja na ulinzi katika maeneo ya mipaka.

Tume hiyo iliundwa na Rais Samia Novemba 20, 2025 kufuatia matukio ya vurugu yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi zenye thamani ya Sh125 bilioni nchini, hatua iliyolenga kufanya uchunguzi wa kina na kutoa mapendekezo ya kudumu ya kurejesha amani na utulivu wa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: WABUNGE WAKIJADILI HOTUBA YA WIZARA YA NISHATI BUNGENI

🔴LIVE: WABUNGE WAKIJADILI HOTUBA YA WIZARA YA NISHATI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: NDEJEMBI AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI WIZARA YA NISHATI

🔴LIVE: NDEJEMBI AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI WIZARA YA NISHATI

Nukta TV

🔴LIVE: RAIS SAMIA, MAMALISHE,  BABALISHE WANAJAMBO LAO LEO

🔴LIVE: RAIS SAMIA, MAMALISHE, BABALISHE WANAJAMBO LAO LEO

Nukta TV

BENEFIT FROM
Nukta ADS
Advertise with us to reach a wider audience with high conversion rates.
Other Nukta Africa Products
Nukta Habari
Stories that matter
Topics
Inuldge yourself with the topics in Nukta
All
Business
Africa
Contact
Tel
+255 750 881 888
Mail
newsroom@nukta.co.tz
Address
Mwananyamala kwa Kopa Dabe House Dar es Salaam TZ, 14108
Social Media

© 2024 Nukta Africa. All Rights Reserved.