Nukta Africa kuzindua Nukta AI, siku ya uhuru wa vyombo vya habari
- Ni katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Aprili 27, yatakayofanyika kitaifa jijini Arusha.
- Nukta AI itasaidia upatikanaji wa taarifa na takwimu kama vile bei za hisa, viwango vya kubadili fedha na bei za mazao.
Dar es Salaam. Kampuni ya habari na teknolojia, Nukta Africa inatarajia kuzindua programu ya akili unde (AI) itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa na data zitakazowasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi kiuchumi na kijamii.
Daniel Mwingira, Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni hiyo amesema Nukta AI inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika kitaifa jijini Arusha, Aprili 28 hadi 30.
“Nukta Africa tumejipanga kuhakikisha tunatumia teknolojia ya AI kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa taarifa sahihi, kwa lengo la kumuwezesha mtanzania hususan kijana kupata maarifa yanayoweza kubadilisha maisha yake,” amesema Mwingira.

Nukta AI ni programu ya akili unde iliyobuniwa na Nukta Africa inayorahisisha upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi zenye muktadha wa Tanzania na Afrika ili kuwasaidia walaji wa taarifa hususan vijana hasa kufanya maamuzi bora ya kiuchumi na kijamii.
Nukta AI na taarifa za Tanzania
Kwa mujibu wa Mwingira, Nukta AI inakwenda kuwa miongoni mwa zana chache za AI zilizoandaliwa kwa kuzingatia muktadha wa Tanzania na Afrika kwa ujumla, hali itakayopunguza upotoshaji wa taarifa ambao kwa muda mrefu umekuwa changamoto katika majukwaa mengine ya AI ambayo hayana taarifa za ndani.
Ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kumkomboa kijana kiuchumi na kifikra, Nukta AI inauwezo wa kutoa taarifa muhimu kwa wakati, zikiwemo bei za hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), bei za mazao pamoja na viwango vya ubadilishaji fedha.
“Hii itarahisishia vijana kupata taarifa muhimu zitakazowawezesha kufanya maamuzi hususan wakati huu mabo wengi wamekimbilia kuwekeza kwenye masoko ya mitaji,” amebainisha Mwingira.

Mbali na hilo, Mwingira amesema kuwa Nukta AI ipo katika hatua za majaribio ambapo hivi karibuni itaweza kuwahudumia watumiaji kwa kutumia lugha za asili za makabila kupitia kipengele cha kamusi kilichojumuishwa ndani ya mfumo huo.
“Hata mtumiaji anayependelea kutumia lugha za makabila kama vile Kisukuma, Kichaga au Kihaya ataweza kupata huduma kupitia Nukta AI,” ameeleza.
Mkombozi wa habari za takwimu
Kwa takriban miaka nane tangu kuanzishwa kwake, Nukta Africa imeendelea kuwa mdau muhimu katika sekta ya habari na mawasiliano kupitia utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wanahabari yanayokwenda sambamba na mahitaji ya soko la sasa.
Mafunzo hayo ni pamoja na uthibitishaji wa habari (Fact-Checking), uandishi wa habari za takwimu (Data Journalism), ubunifu wa infografia (Infographics Design), pamoja na usimamizi wa maudhui ya kidijitali (Digital Content Management).
Nukta AI pia inatarajiwa kuongeza ufanisi kwa walaji wa taarifa kurahisisha uchakataji na uwasilishaji wa takwimu.

Hata hivyo, Mwingira amebainisha kuwa taarifa zaidi kuhusu AI hiyo na jinsi ya kutumia zitapatikana mara baada ya kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki ijayo.
“Endelea kutufuatilia kupitia nukta.co.tz pamoja na mitandao yetu ya kijamii ili kuweza kujua jinsi ya kuipata na kutumia Nukta AI” ameelekeza Mwingira.
Latest