Utalii wa kupiga mbizi washika kasi duniani

November 17, 2022 12:41 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Utakua kwa asilimia 5.9 ifikapo 2030.
  • Kuongezeka kwa mahitaji ya watu kuogelea kwachangia.
  • Maeneo unayoweza kupiga mbizi Tanzania ni pamoja na Pemba na Dar es Salaam. 

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu wenye mpango wa kuwekeza katika utalii wa kupiga mbizi kwenye maji basi wakati ni sasa kwa sababu tasnia hiyo inakuwa kwa kasi duniani. 

Utafiti wa soko uliofanywa hivi karibuni na kampuni ya utafiti ya ESOMAR ya nchini Netherlands umetabiri kuwa soko la utalii wa kupiga mbizi duniani litakua kwa asilimia 5.9 kati ya 2020 na 2030.

Kukua kwa utalii wa majini kunatarajiwa kubaki kuwa kichocheo kikuu cha ukuaji sekta hiyo.

Ongezeko la mahitaji ya michezo ya kusisimua na shughuli za majini limekuwa likichochea utalii huo kukua mwaka hadi mwaka huku likifungua fursa mbalimbali za uwekezaji zitakazoweza kuwafaidisha watu watakaoamua kuwekeza. 

Kwa sasa, watalii wanavutiwa zaidi kujionea viumbe wa baharini na mandhari yake na wakati mwingine hutumia kama njia mojawapo ya mazoezi.

Utafiti huo umeeleza kuwa ili wawekezaji wafaidike na utalii huo ushirikiano kati ya kampuni za kuongoza watalii uimarishwe ili kuifanya huduma ya kupiga mbizi kuwa endelevu.

Mkakati huo utaziwezesha kampuni kuvutia wateja wapya na kutoa huduma za kuridhisha kwa wateja wake wa mara kwa mara.

Ulaya inashikilia sehemu kubwa zaidi ya thamani katika soko la utalii la kupiga mbizi la kimataifa kwa sababu ya kuongezeka kwa ufahamu wa watumiaji na mkusanyiko mkubwa wa waendeshaji na tovuti za marudio katika ukanda huo. 

Upigaji mbizi ni moja ya njia y akujifunza zaidi kuhusu maisha ya baharini au ziwani. Picha | Tripsavvy.

Maeneo unayoweza kupiga mbizi Tanzania

1. Kisiwa cha Mafia

Maeneo maarufu unayoweza kupata huduma ya kupiga mbizi majini ni pamoja na kisiwa cha Mafia ambacho ni moja ya hifadhi kubwa za baharini ambacho kinapatikana katika bahari ya Hindi nje kidogo ya mkoa wa Pwani. 

2. Kisiwa cha Pemba 

Kama utapata nafasi ya kutembelea kisiwa cha Pemba utapata fursa ya kupiga mbizi katika bahari ya Hindi na kujionea matumbawe, miamba ya rangi ya kupendeza, na feni kubwa za baharini. 

Kuna maeneo mengi ya kupiga mbizi kuzunguka kisiwa cha Pemba. Hata hivyo, pembe ya Kaskazini ndiyo maarufu zaidi kwa kupiga mbizi kwa sababu ina papa  wengi.

Watoa huduma hukuwezesha kuzama ndani ya maji kati ya mita 20 hadi mita 40.


Zinazohusiana


 3. Leven, Zanzibar

Eneo la Leven linapatikana katika ncha ya kaskazini ya Zanzibar na ni kwa wapiga mbizi waliobobea kwa sababu ina kina kirefu na inahitaji uzoefu mkubwa wa kuogelea kwa sababu ya mawimbi makubwa bahari.

Eneo hilo ni nyumbani kwa samaki wakubwa wakiwemo Barracuda, Kingfish, Trevally na Moray Eels.

 

4. Ziwa Tanganyika

Kama hupendi kupiga mbizi kwenye maji ya chumvi, basi Ziwa Tanganyika litakupatia maji baridi na kufanikisha shughuli yako ya kupiga mbizi.

Ziwa hilo linalotenganisha nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi ni nyumbani kwa viumbe wa rangi ya ajabu, ambao kuwaona kunaongeza uzoefu na furaha ya uumbaji wa dunia.

Kuna maeneo mengi ya ajabu ya kupiga mbizi yanayopatikana kote Tanzania na visiwa vinavyoizunguka ni uchaguzi wako uende wapi kulingana na urefu wa mfuko wako. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW