Tanzania kuadhimisha siku ya utalii duniani ikihamasisha ukarimu

September 27, 2025 12:50 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Kauli mbiu ya mwaka huu yasisiitiza mchango wa sekta hiyo katika uchumi, jamii, tamaduni na uhifadhi wa mazingira.

Dar es Salaam. Tanzania leo imeungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism) likiitaja kuwa kinara barani Afrika kwa ongezeko kubwa la watalii lililofikia asilimia 48 mwaka 2024.

Siku hii huadhimishwa kila mwaka kwa mujibu wa maazimio ya Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) ikiwa na lengo la kutambua mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni na uhifadhi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 27, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amesema maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu inayosisitiza mchango wa sekta hiyo katika uchumi, jamii, tamaduni na uhifadhi wa mazingira.

“Tanzania, kama mwanachama kamili wa UN Tourism itaadhimisha Siku hii kwa kuhamasisha shughuli na huduma za utalii pamoja na ukarimu, wataalamu wa kisekta kukutana kwenye maeneo yao ili kujengeana uzoefu wa usimamizi wa sekta, na kuhamasisha uhifadhi wa maliasili zetu kwa kizazi cha sasa na cha baadae,” inaeeleza tarifa ya Chana.

Mtalii wa ndani akisoma baadhi ya vivutio vinavyopatikana nchini Tanzania ikiwemo hifadhi ya kijiolojia ya Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark. Picha/ Fatuma Hussein

Kulingana na hotuba ya bajeti ya mwaka 2025 ya Wizara ya Maliasili na Utalii sekta hiyo imeonesha ongezeko la mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 sawa na Sh3.39 trilioni mwaka 2021 hadi dola bilioni 3.9 sawa na Sh9.5 trilioni mwaka 2024 kwa watalii wa kimataifa.

Aidha, mapato ya utalii wa ndani yamepanda kutoka shilingi bilioni 46.3 mwaka 2021 hadi bilioni 209.8 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 353.1.

Hata hivyo, Waziri Chana ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuchukua hatua thabiti za kukuza utalii endelevu ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii kupitia filamu za The Royal Tour na Amazing Tanzania na kutumia majukwaa ya mikutano ya kimataifa, kuwekeza katika miundombinu, na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika shughuli za utalii.

Vilevile, Chana ameongeza kuwa Serikali inasisitiza utunzaji wa maliasili na kukuza mazao mapya ya utalii kama vile utalii wa fukwe, wa meli na wa kitamaduni.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi na wadau wote wa sekta ya utalii kushirikiana na Serikali kuhakikisha ukuaji wa utalii nchini unakwenda sambamba na uhifadhi wa maliasili, kuchochea ukuaji wa uchumi na kusaidia maendeleo ya sekta nyingine,” amesema Waziri Chana.

Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na wizara hiyo zinaonesha kuwa idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 9.2 kati ya Januari na Julai 2025, ambapo wageni walifikia milioni 1.27 ikilinganishwa na milioni 1.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Picha hii inaonyesha kibao chenye alama ya kuingilia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania, moja ya vivutio vya utalii maarufu barani Afrika kutokana na uwepo wa wanyama pori. Picha Fatuma Hussein.

Wito wa umoja wa mataifa

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametumia maadhimisho ya mwaka huu kutoa wito wa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa chachu ya mabadiliko endelevu.

 “Wakati dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa kukosekana kwa usawa, tunahitaji hatua za kijasiri, za haraka na endelevu ambazo huweka watu na sayari kwanza,” amesema Guterres.

Utabiri wa miaka 10 sekta ya utalii Tanzania

Katika miaka 10 ijayo Tanzania inatarajiwa kuendelea kuimarika kwa kasi kulingana na takwimu za kiuchumi zilizotolewa na World Travel and Tourism Council.

Takwimu hizo zinabainisha kuwa ,sekta ya utalii inakadiriwa kufikia thamani ya Sh30.9 trilioni ifikapo mwaka 2034, huku ikitarajiwa kutoa ajira milioni 2.25, ikijumuisha ongezeko la ajira mpya 710,000.

Hii ni sawa na kusema kuwa takribani kila mfanyakazi mmoja kati ya 15 nchini atakuwa akihusiana na sekta ya utalii.

Sanjari na hayo, maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani nchini yanatarajiwa kutoa fursa kwa wadau na wataalamu wa sekta kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuimarisha mshikamano katika kuendeleza utalii endelevu kwa manufaa ya taifa.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks