Corona haimalizwi kwa kunywa maziwa, maji ya moto

December 11, 2020 1:39 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Sio kweli ukinywa maji mara sita, maziwa au chai na kujifukiza unapona Corona ndani ya siku nne.
  • WHO bado haijathibitisha dawa yoyote itakayotumika kama tiba dhidi ya virusi vya Corona.

Dar es Salaam.  Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona ambavyo vimekua vikiutesa ulimwengu bado haujapata tiba sahihi mpaka sasa.

Pamoja na ukweli huo, kumekua na uzushi mwingi unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii ukijaribu kuaminisha watu kuwa tiba ya ugonjwa wa Corona imepatikana.

Moja ya taarifa hizo ni pamoja na taarifa kwa njia ya video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ukinywa maji ya moto mara sita kwa siku au maziwa mara nne kwa siku na kujifukiza mara nyingi iwezekanavyo ndani ya siku nne unaweza kuua virusi vya COVID-19 mwilini.

Madai hayo hayana ukweli wowote ni uzushi unaolenga kupotosha watu.

Mwonekano wa picha ya video iliyotumika kupotosha kuhusu tiba ya virusi vya Corona. Picha| Nukta Fakti

Shirika la Afya duniani (WHO) halijathibitisha kupatikana kwa dawa ya kutibu virusi hivyo na imeeleza kuwa bado wataalamu wa sayansi wanafanya tafiti wa tiba ya ugonjwa huo.

“Wanasayansi ulimwenguni bado wanafanya kazi kutafuta tiba ya Covid-19, WHO itaendelea kutoa taarifa pindi tiba itakapopatikana,” inaeleza WHO katika moja ya taarifa zake kuhusu Corona.


Zinazohusiana:


Vilevile, WHO imeeleza kwenye tovuti yake kuwa haishauriwi mtu kujitibu mwenyewe nyumbani kwa kutumia dawa yoyote bila kupata ushauri wa wataalam wa afya wanaotambulika.

“WHO haishauri tiba binafsi kwa kutumia dawa yoyote kama moja ya kinga au tiba dhidi ya virusi vya Corona”, imeeleza taarifa hiyo.

Njia ambazo zinapendekezwa kujikinga na ugonjwa huo ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kutumia tishu wakati wa kupiga chafya au kukohoa. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW