Hapana: Soda za Twist hazina virusi vya Ebola

October 25, 2022 8:35 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Uzushi huo umekuwa ukisambaa kwa miaka mitatu mtandaoni. 
  • TBS wakanusha uwepo wa kinywaji hicho nchini.
  • Wizara ya Afya yasema Ebola inaambukizwa kwa njia ya kugusa maji maji ya mgonjwa.

Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa kinywaji cha Sayona aina ya Twist wakawa na hofu kubwa mara baada ya  kusambaa kwa taarifa kuwa kinywaji hicho kina sumu ya ugonjwa wa Ebola na kimeua watu 1,800 nchini Nigeria.

Taarifa hiyo inayosambaa kwenye jamii na kwenye mitandao kama Whatsapp siyo za kweli.

Kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2019 kinywaji cha Sayona aina ya Twist kimekuwa kikihusishwa na uzushi wa aina mbalimbali.

Mara nyingi uzushi huo husambaa wakati aina fulani ya ugonjwa inapoibuka, licha ya mamlaka husika kukanusha kila wakati uzushi huo unaposambaa.

Kwa mwaka huu taarifa hiyo imeanza kusambazwa hivi karibuni baada ya kuzuka kwa ugonjwa Ebola nchi ya jirani ya Uganda.  

Hata hivyo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilikanusha uzushi huo kwa mara ya kwanza Julai 22, 2019 kupitia ukurasa wake wa Twitter wa shirika hilo.

Wizara ya Afya nchini katika taarifa yake iliyotolewa Septemba 22, 2022 imesema ugonjwa wa Ebola ni miongoni mwa magonjwa yanayosambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa kula au kugusa mnyama mwenye maambukizi.

“ Unaenea kutoka kwa binadamu mmoja hadi mwingine kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa kwa mfano mate, machozi, damu, matapishi, mkojo na kinyesi” imesema taarifa hiyo

Mpaka sasa hakuna taarifa Rasmi kutoka TBS au kutoka mtandao wa Kimataifa wa Mamlaka za Udhibiti Usalama wa Chakula (INFOSAN) ulio chini ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) juu ya tahadhari ya kinywaji hicho kinachodaiwa kupoteza maisha ya watu nchini Nigeria.


Soma zaidi


Njia za kujikinga na Ebola

Kinyume na taarifa hizo za uzushi zinazowataka watu kutogusa wala kunywa kinywaji cha Twist ili kuzuia maambukizi ya Ebola, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa njia za kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kuepuka kugusana na wagonjwa wa Ebola.

Kuva vifaa vya kujikinga wakati wa kumuhudumia mgonjwa wa Ebola pamoja na kuosha mikono baada ya kumuhudumia mgonjwa au kumtembelea.

Kuepuka kula nyama ambayo haijapikwa vizuri, kula nyama mbichi au mizoga na kugusa wanyama wenye maambukizi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...