Ulaghai wa mtandaoni waongezeka kwa asilimia 47 Tanzania
- Mkoa wa Rukwa waendelea kuwa kinara wa matukio ya ulaghai wa mtandaoni.
- Uelewa mdogo kuhusu masuala ya fedha na mitandao ya simu vyatajwa kama chanzo.
Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakatakiwa kujiongezea maarifa zaidi juu ya namna ya kujilinda na ulaghai wa mtandaoni ili wajiepushe na kupoteza mali au fedha kutokana na kuendelea kukithiri kwa vitendo vya ulaghai kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo ya pili (Aprili – Juni) ya mwaka 2023 matukio ya ulaghai yameongezeka na kufikia 23,048.
Hadi mwezi Machi 2023, kulikuwa na matukio ya ulaghai wa mtandaoni 12,044 tu.
Hivyo, kwa mujibu wa takwimu hizo ndani ya kipindi cha miezi mitatu matukio mapya 11,004 ya ulaghai wa mtandaoni yalifanyika ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 47.7.
Ulaghai huo huhusisha wizi wa fedha katika akaunti za mitandao ya simu au benki, ambapo wezi hao hutumia mbinu mbalimbali kama kuwataka watu watume kiasi fulani cha pesa kwa kujifanya wao ni watu wa karibu, walimu, wenye nyumba au taasisi za mikopo.
Wakati mwingine wezi hutumia mbinu ya kuwapigia watumiaji wa huduma za mitandao na kujifanya watoa huduma wa mitandao ya simu ambapo hulaghai na kuiba kiasi cha fedha.
Ingawa, mwaka 2021 Serikali iliwataka Watanzania wote kusajili laini zao kwa alama za vidole kwa kutumia vitambulisho vya Taifa, ili kukabiliana na ulaghai wa kifedha mtandaoni jambo ambalo bado halijafua dafu.

Rukwa kinara
Kwa mujibu wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2022 (Aprili-Juni 2023) mkoa wa Rukwa ndiyo kinara wa matukio hayo kwa asilimia 37. 8 ambapo jumla ya matukio 8,991 ya uhalifu wa mtandaoni yamefanyika mkoani humo.
Hiyo ni sawa na kusema katika makosa 10 ya ulaghai wa mtandaoni yaliyofanyika kati ya mwezi Aprili mpaka Juni 2023, matatu yalifanyika mkoani Rukwa.
Uchambuzi wa ripoti ya ulaghai wa mtandaoni uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa matukio yaliyofanyika mkoani Rukwa ni mara 1,646 zaidi ya mkoa wa Simiyu uliorekodi matukio 14 tu ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Hii ni mara ya pili ndani ya kipindi cha miezi sita kwa mkoa wa Rukwa kuongoza kwa matukio ya uhalifu mtandaoni ambapo mwezi Machi mkoa huo ulirekodi matukio 5,422.
Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 65.8 za matukio ya ulaghai kwa njia ya mtandao yaliyofanyika ndani ya miezi mitatu mkoani humo.
Mbali Rukwa mikoa mingine inayoongoza kwa ulaghai wa kimtandao ni Mkoa wa Morogoro uliorekodi matukio 6,535, ikifuatiwa na jiji Dar es Salaam (2,999), Mbeya (1,684), na jiji la Mwanza lililorekodi matukio hayo 496.
Soma zaidi
-
Dar es Salaam kinara matumizi huduma za simu Tanzania
-
Watumiaji wa huduma za simu wafikia milioni 64.1 Tanzania
Mtandao wa Airtel unatumika zaidi
Jumla ya matukio ya ulaghai 10,100 yamefanyika kupitia mtandao wa Airtel ambayo ni sawa na asilimia 44 ya matukio yote yaliyofanyika mwezi Juni.
Mtandao huo unafuatiwa na mtandao wa Tigo wenye matukio 7,802, Vodacom matukio 3,959 na Halotel matukio 560.
Wataalamu wa teknolojia waeleza sababu
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya teknolojia wamesema kuongezeka kwa matukio ya ulaghai nchini kunasababishwa na ufahamu mdogo wa masuala ya usalama kimtandao.
“Hao wanaofanya hivyo wanafanya kwa sababu wanajua watu hawajui kujiprotect (kujilinda) wanapotumia mtandao,”amesema mtaalamu wa teknolojia Clemence Kyara.
Clemence anasema kuongezeka kwa matukio ya kiulaghai katika mkoa wa Rukwa kunaweza pia kusababishwa na elimu na uelewa mdogo wa masuala ya mitandao na teknolojia pamoja na upatikanaji wa fedha za mkupuo zinazotokana na kilimo ambayo ndiyo shughuli kuu mkoani humo.
Sambamba na hilo mtaalamu huyo anashauri watumiaji wa simu kutumia nywila katika simu na laini pamoja na kuhakiki taarifa zozote wanazozipoea kabla ya kutuma pesa au kutoa taarifa za siri.

Matumizi ya nywila katika laini za simu husaidia kuzuia utapeli kwa njia ya simu unaofanyika mara baada ya simu ya mtumiaji kupotea au kuibiwa.Picha|Biometric Update.
Serikali yajipanga kupunguza ulaghai
Siku za hivi karibuni Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kudhibiti wimbi kubwa la ulaghai wa mtandaoni linaloendelea kuongezeka ikiwemo uhakiki wa laini za simu zilizosajiliwa kwa alama za vidole
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye aliyekuuwa akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2023/2024 amesema uhakiki huo utarahisisha upatikanaji wa wahusika wa utapeli na ulaghai mtandaoni.
“Nataka nitangaze kiama cha matapeli kwenye mitandao…tumejipanga vizuri na leo tutaomba msaada wa wenzetu wa polisi tuondoe huruma kwenye jambo hiili tulikomeshe tulifute kwenye nchi yetu,” amesema Nape mbele ya Wabunge.
Kwa mujibu wa Wizara hiyo hadi kufikia Aprili 30, 2023 laini 62,317,168, zimesajiliwa kwa alama za vidole huku zoezi la uhakiki wa laini hizo likiendelea.
Mbali na Serikali mitandao ya simu imeendelea kutoa elimu kwa kwa wateja wao kujiepusha naulaghai huo kwa njia ya matangazo, vipeperushi na ujumbe mfupi.
Latest