Rukwa, Morogoro, vinara majaribio ya ulaghai Tanzania

October 23, 2024 3:46 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mikoa hiyo imerekodi zaidi ya theluthi ya matukio yote Tanzania
  • Jumla ya majaribio 16,069 ya ulaghai yarekodiwa.

Arusha. Licha ya matokeo chanya yanayochagizwa na ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na kukua kwa uchumi wa kidijitali na kurahisisha mawasiliano, sekta hiyo imeendelewa kukabiliwa na changamoto ya ulaghai, hususan kupitia mitandao.

Ulaghai huo huhusisha wizi wa fedha katika akaunti za mitandao ya simu au benki, ambapo wezi hutumia mbinu mbalimbali kama kuwataka watu watume kiasi fulani cha pesa kwa kujifanya wao ni watu wao wa karibu, walimu, wenye nyumba au taasisi za mikopo.

Wakati mwingine wezi hutumia mbinu ya kuwapigia watumiaji wa huduma za mitandao na kujifanya watoa huduma wa mitandao ya simu ambapo hulaghai na kuiba kiasi cha fedha jambo linaloathiri shughuli za kiuchumi.

Takwimu za mawasiliano za  robo ya mwaka unaoishia Septemba 2024 zinazotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinabainisha kuwa, Tanzania ilirekodi majaribio 16,069 ya ulaghai.

Hata hivyo, matukio ya ulaghai yamepungua kwa asilimia 28 kulinganisha na robo mwaka iliyopita (Aprili – Juni ) ambapo Tanzania iliripoti ongezeko la asilimia 57 kutoka matukio 17,319 Mwezi Machi hadi matukio 22,257 mwezi Juni 2024.

Ripoti ya TCRA inabainisha kuwa mikoa ya Rukwa na Morogoro ndiyo inayoongoza kwa kurekodi idadi kubwa ya matukio ya utapeli ikiwa ni zaidi ya theluthi moja ya majaribio yote ya ulaghai nchini. 

Mkoa wa Rukwa umerekodi jumla ya matukio 5,571 katika robo ya mwaka inayoishia Septemba 2024, sawa na asilimia 34.7 ya matukio yote yaliyorekodiwa nchini katika kipindi hicho.

Aidha, zaidi ya asilimia 90 ya matukio hayo yalitokea katika Wilaya ya Sumbawanga, ambapo matukio 5,198 yalirekodiwa, Wilaya ya Nkasi matukio 250 na Kalambo matukio 122.

Mkoa wa Morogoro umeripoti jumla ya matukio 5,486 ambapo yamepungua kutoka matukio 7,355 yaliyorekodiwa katika ripoti ya robo muhula uliopita.

Mikoa Mingine iliyoongoza kwa kuripoti matukio ya ulaghai kwa njia ya mtandao ni Mbeya wenye matukio 1,112, Dar es Salaam (959), Arusha (351), na Kilimanjaro matukio 335.

Kwa upande wa mikoa ya Simiyu, Lindi, Mara, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Kusini Pemba ndio imerekodi idadi ndogo zaidi ya majaribio ambapo kila mkoa umerekodi chini ya asilimia 1 ya majaribio yote ya utapeli wa kimtandao yaliyoripotiwa nchini.

Tigo kinara majaribio ya ulaghai 

Mtandao wa Tigo umeongoza kwa kuwa idadi kubwa ya majaribio ya ulaghai ikirekodi matukio 6,608  ingawa yamepungua kutoka matukio 10,242 yaliyorekodiwa robo ya mwaka inayoishia Juni, 2024 sawa na upungufu wa asilimia 35.

TTCL imeshika nafasi ya pili kwa kurekodi matukio 2,127 katika robo ya mwaka unaoishia Septemba 2024 ambapo yameongezeka kwa asilimia 2 kutoka matukio 2,093 yaliyorekodiwa robo mwaka iliyopita.

Halotel nayo imerekodi ongezeko la majaribio ya ulaghai yakifikia 711 kutoka 469 sawa na ongezeko la asilimia 52.

Hata hivyo, baadhi ya mitandao imeripoti kupungua kwa majaribio ya ulaghai ikiwemo Airtel ambayo  imerekodi matukio 3,446 kutoka matukio 6,069 huku Vodacom ikirekodi matukio 3,177 yaliyopungua kwa asilimia 6 kutoka matukio 3,384 yaliyorekodiwa miezi mitatu iliyopita.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV