Morogoro kinara ulaghai wa mtandaoni Tanzania

July 31, 2024 2:31 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Yashika nafasi ya kwanza ikiwa na matukio 7,355.
  • Majaribio ya ulaghai yaongezeka kwa asilimia 57. 

Dar es salaam. Huenda Serikali pamoja na wadau wa mawasiliano wakatakiwa kuongeza juhudi za kutoa elimu ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni nchini Tanzania mara baada ya ripoti kuonesha ongezeko la majaribio ya matukio hayo kwa zaidi ya asilimia 50 huku mkoa wa Morogoro ukiwa kinara.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Mawasiliano iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA za robo ya pili ya mwaka (Aprili – Juni 2024 ) majaribio ya ulaghai mtandaoni yameongezeka kwa asilimia 57 kutoka matukio 17,319 Mwezi Machi hadi matukio 22,257 mwezi Juni 2024.

Mkoa wa Morogoro ndio wenye majaribio mengi zaidi ya ulaghai, yakifikia matukio 7,355 sawa na asilimia 33 ya matukio yote yaliyoripotiwa katika robo ya mwaka iliyoishia Mwezi Juni.

Maeneo mengine yaliyoripotiwa kuwa na majaribio mengi ya uhalifu ni pamoja na Rukwa yenye majaribio 7,198 , Mbeya majaribio 2,113, Dar es Salaam majaribio 1,151 pamoja na Arusha yenye majaribio 940.

Mfano wa jumbe zinazotumwa na watu wanaojaribu kufanya ulaghai. Picha l Esau Ng’umbi

Ulaghai huo huhusisha wizi wa fedha katika akaunti za mitandao ya simu au benki, ambapo wezi hao hutumia mbinu mbalimbali kama kuwataka watu watume kiasi fulani cha pesa kwa kujifanya wao ni watu wa karibu, walimu, wenye nyumba au taasisi za mikopo.

Wakati mwingine wezi hutumia mbinu ya kuwapigia watumiaji wa huduma za mitandao na kujifanya watoa huduma wa mitandao ya simu ambapo hulaghai na kuiba kiasi cha fedha.

Ingawa, mwaka 2021 Serikali iliwataka Watanzania wote kusajili laini zao kwa alama za vidole kwa kutumia vitambulisho vya Taifa, ili kukabiliana na ulaghai wa kifedha mtandaoni jambo ambalo bado halijafua dafu.

Mikoa iliyo na idadi ndogo zaidi wa makosa haya upande wa Tanzania bara ni Mtwara, Lindi, Manyara, Simiyu, na Njombe ambapo majaribio yaliyoripotiwa ni chini ya 100.

Kwa upande wa Zanzibar mkoa wa Mjini Magharibi ndio umeongoza kwa majaribio ya utapeli kwa njia ya mtandao ukiwa na jumla ya matukio 125 huku Mkoa wa Kaskazini Pemba ukiripoti tukio moja tu la jaribio la ulaghai wa mtandaoni.


Benki Kuu yatahadharisha udanganyifu wa fedha mtandaoni


Mtandao wa Tigo unatumika zaidi

Mtandao wa Tigo umetumika zaidi kufanya majaribio ya ulaghai wa mtandaoni katika robo mwaka ya Aprili – Juni ukiwa na Jumla ya majaribio 10, 242 sawa na asilimia 46 ya majaribio yote idadi ambayo imeongezeka kutoka asilimia 34.7 iliyoripotiwa Mwezi Machi.

Mtandao wa Tigo umefuatiwa na Mtandao wa Airtel wenye majaribio 6,069, Vodacom majaribio 3,384, TTCL majaribio 2,093 pamoja na Halotel yenye matukio 469.

Hata hivyo, TCRA imewasisitiza watumiaji wa mitandao ya simu kufuata maelekezo kutoka kwa watoa huduma kwa kutumia namba 100 pekee na sio namba binafsi za simu.

Aidha, Rolf Kibaja, Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma  wa TCRA ameiambia Nukta Habari kuwa wanashirikiana na watoa huduma za mtandao wa simu ili kuimarisha hatua za usalama mtandaoni kwa kutumia kampeni mbalimbali za mitandao ya kijamii.

“Watumiaji wa simu wanapaswa kuhakiki usajili wa laini zao ili kutambua namba zilizotumia vitambulisho vyao kufanya usajili na endapo hawazitambui namba hizo watoe taarifa kwa watoa huduma ili zifutwe,” amebainisha Kibaja.

Kibaja ameongeza kuwa watumiaji wa mitandao ya simu wanahimizwa kutoa taarifa za majaribio ya utapeli wanapokutana nayo kupitia namba 15040 ili zifuatiliwe na watoa huduma wao na kufungiwa endapo zitabainika kujihusisha majaribio ya ulaghai.

Itakumbukwa tarehe 19 Mei, 2023 aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alipokuwa akiwasilisha Bungeni  makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2023/2024 alisema wanakaribia kupata muarobaini wa tatizo hilo.

“Nataka nitangaze kiama cha matapeli kwenye mitandao…tumejipanga vizuri na leo tutaomba msaada wa wenzetu wa polisi tuondoe huruma kwenye jambo hiili tulikomeshe tulifute kwenye nchi yetu,” alisema Nape mbele ya wabunge.

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Mikakati ya Serikali kuhakikisha walimu wa VETA wanapata ajira na mikopo

Nukta TV

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Mama Salama alivyombana Wanu kuhusu maslahi ya walimu wanaojitolea

Nukta TV

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Kwanini uchafuzi wa mazingira ni tishio kwa afya ya binadamu na uchumi

Nukta TV