Matukio ya ulaghai wa mtandao yashuka kwa asilimia 25
- Mtwara yavunja rekodi ya kuwa na matukio machache zaidi ikiwa na matukio 25.

Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa mitandao wakaondokana na changamoto ya ulaghai mtandaoni baada ya kupungua kwa matukio hayo kwa asilimia 25 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ulaghai mtandaoni ni kitendo cha kutumia intaneti, simu au mitandao ya kijamii kuiba pesa, taarifa za siri, au kudanganya watu.
Ulaghai huu unaweza kufanyika kwa njia ya ujumbe wa uongo (kutumiwa SMS za kuomba fedha au kudanganya umeshinda zawadi), wizi wa nenosiri (kuombwa kutoa namba ya siri au namba ya uthibitisho – OTP) pamoja na kutumia viungo feki.
Takwimu za mawasiliano za robo ya mwaka inayoishia Juni 2026 zinazotolewa na TCRA, zinaonesha ulaghai umepungua kutoka matukio 9,816 yaliyoripotiwa robo mwaka inayoishia Machi 2026 hadi kufikia matukio 7,334 katika robo ya mwaka inayoishia Juni 2026.
Kulingana na takwimu hizi ni sawa na kusema matukio 2,482 hayajaripotiwa ndani ya miezi mitatu iliyopita suala linalotoa ahueni kwa wananchi.
Rukwa Kinara
Ripoti ya TCRA inabainisha kuwa mkoa ya Rukwa unaongoza kwa majaribio ya ulaghai ikiwa na matukio 2,495, zaidi ya robo tatu ya majaribio yote ya ulaghai nchini.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa mkoa huo umekuwa kinara kwa ulaghai kwa zaidi ya miaka mitano, ukipanda au kushuka kila baada ya miezi mitatu.
Licha ya kuwa kinara, takwimu za TCRA zinabainisha kuwa ulaghai mtandaoni katika mkoa wa Rukwa unapungua karibu kila mwezi suala lunalotoa ahueni kwa wakazi wa eneo hilo.
Mathalan, katika ripoti ya robo ya kwanza 2025 matukio 7,385 yalirekodiwa mkoani Rukwa, yaliyopungua na kufikia matukio 3,444 katika robo ya pili, 2025.
Mbali na Rukwa, mkoa wa Morogoro umeshika nafasi ya pili kwa kurekodi matukio 2,129 huku wilaya ya Kilombero ikiripoti matukio 1,781 ambayo ni zaidi ya nusu ya matukio yaliyorekodiwa na mkoa mzima.
Mikoa mingine iliyoongoza kwa kuripoti matukio ya ulaghai kwa njia ya mtandao ni Dar es Salaam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na matukio 615, ikifuatiwa na Mbeya yenye matukio 370.
Kwa upande wa mikoa iliyorekodi matukio machache zaidi ya ulaghai wa mtandaoni ni Shinyanga ikiwa na matukio 33, ikifuatiwa na Lindi matukio 31 na Mtwara ikishika mkia kwa kuwa na matukio machache zaidi ikiwa na matukio 25.
Kwa upande wa Zanzibar mkoa wa Mjini Magharibi ndio umeongoza kwa majaribio ya utapeli kwa njia ya mtandao ukiwa na jumla ya matukio 35 huku Mkoa wa Kusini Unguja ukifuata kwa kuwa na matukio 5.

Mtandao wa Yas waongoza
Ripoti ya TCRA inaonesha baadhi ya makampuni yanayo toa huduma za mawasiliano nchi yaliyorekodi kiwango kikubwa zaidi cha majaribio ya uhalifu.
Mtandao wa Yas ndiyo uliyorekodi idadi kubwa zaidi ya majaribio katika robo iliyoishia Juni, 2026 ikiwa na jumla ya matukio 2,306, sawa na asilimia 31.4 ya matukio yote.
Licha ya kuwa na idadi kubwa zaidi, Yas ilipunguza idadi ya matukio hayo kutoka 2,659 yaliyo rekodiwa miezi mitatu iliyopita hadi matukio 2,306, TTCL inafuata ikiwa na matukio 2,039, sawa na asilimia 27.8, huku Vodacom ikiwa na matukio 1,364, Airtel 1,053 na Halotel 572.
TTCL ilirekodi punguzo kubwa zaidi kwa asilimia, kutoka matukio 3,375 hadi 2,039, sawa na asilimia 39.59, kwa upande wa Vodacom matukio yalipungua kwa asilimia 27.56, huku Airtel matukio yakipungua kwa asilimia 24.73.
Wakati mitandao mingine ikirekodi kupungua kwa matukio, Halotel ndiyo iliyokwenda kinyume na mwenendo wa jumla, ikiripotiwa kuwa na matukio yaliyoongezeka kutoka 500 hadi 572 ikiwa ni sawa na ongezeko la matukio kwa na asilimia 14.4
Mapambano yanaendelea
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angellah Kairuki aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo amesema kupungua kwa matukio ya ulaghai wa mtandao nchini, kunatokana na jitihada za wazi za Serikali pamoja na wadau wa mawasiliano katika kukabiliananna tatizo hilo.
“Kupungua huku kwa matukio ya ulaghai kunatokana na upekuzi na ukaguzi mbalimbali zilizofanywa na TCRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na wadau wa mawasiliano katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mara zikiwalenga wahusika ambao wanafanya matukio ya ulaghai nchini…,” amesema Kairuki.
Kwa upande wa watumiaji wa mitandao ya simu amewahimiza kutoa taarifa za majaribio ya utapeli wanapokutana nayo kupitia namba 15040 ili zifuatiliwe na hatua za kisheria zipate kuchukuliwa ikiwemo kuzifungia namba hizo.
Aidha, Kairuki amesema Serikali inaendelea na kampeni mbalimbali zenye kuongeza uelewa na usalama kwa watumiaji wa huduma za kimawasiliano ikiwemo ‘futa au delete kabisa’ na ‘sambaza mchongo sio uongo’ inayosisitiza kutosambaza taarifa zisizo sahihi kwenye majukwaa ya kidigitali.
