Ugonjwa wa selimundu unavyowatesa watoto Kanda ya Ziwa
- Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando hupokea zaidi ya watu 300 kila mwezi.
- Robo tatu ya wagonjwa hutoka Kanda ya Ziwa.
- Serikali yaingilia kati kuwanusuru watoto.
Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ya jijini Mwanza hupokea zaidi ya watu 300 wakiwemo watoto kila mwezi wakiwa na vinasaba vya ugonjwa wa selimudu huku wadau wakitaka hatua zaidi zichukuliwe kudhibiti ugonjwa huo.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Ugonjwa wa Selimudu leo Juni 20, 2022, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa hospitali hiyo, Dk Bahati Wajange amesema wagonjwa hao hufikishwa hospitalini kwa kuchelewa.
“Tatizo la ugonjwa huo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ni kubwa tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 11,000 wanaozaliwa nchini hukutwa na vinasaba vya selimudu na kati yao robo tatu hutokea mikoa ya Kanda Ziwa,” amesema Dk Wajange.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniai (WHO) zinabainisha kuwa mtu mmoja kati ya wanne ana ugonjwa wa selimudu huku asilimia saba ya vifo vya watoto nchini husababishwa na ugonjwa wa selimudu.
Mtaalam huyo amesema katika zoezi la upimaji wa ugonjwa huo kwenye kiliniki zao lililoanza mwanzoni mwa mwezi huu, watoto 5,000 walipimwa na kati ya hao asilimia 26 waligundulika na tatizo hilo.
Mambo yanayochangia ugonjwa huo
Dk Emmanuela Ambrose, daktari bingwa wa watoto wa Bugando amesema kisababishi cha ugonjwa wa selimudu ni kurithi kutoka kwa wazazi na kuwa mtoto anapozaliwa anakuwa na dalili za kuvimba mikono na miguu, kuwa na njano, kuishiwa damu, kuvimba bandama, kuumwa mifupa na kupata kiharusi.
“Mtoto huyu anapata shida nyingi hadi za kushindwa kutembea kutokana na mifupa kulika kutoka na seli zinaenda kuziba katika sehemu tofauti tofauti za mwili,” amesema Dk Ambrose.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
-
Mikutano ilivyowazimisha viongozi wa ‘wasusa, twala’ Tanga
-
Vita mbichi: Wakazi wa Pangani wanavyohamasishana kupata chanjo ya Uviko-19
Mtaalam huyo amesema iwapo mgonjwa atafuata taratibu zote za matibabu mtoto mwenye ugonjwa wa sikoseli hupona.
Kwa sasa mgonjwa anapatiwa dawa za kutibu tatizo hilo huku juhudi zinazofanyika ni kutoa elimu kwa jamii kupima kabla ya kuingia kwenye mahusiano ili kila mmoja kugundua kama ni salama.
“Niwashauri wananchi waache kutafuta tiba za ugonjwa huo kwa waganga wa kienyeji kwani iwapo mtoto akiwahishwa hospitalini haraka na mzazi kufuata taratibu za matibabu mtoto huyo ataendelea vizuri,” amesema Dk Ambrose.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike ameitaka jamii kupima ugonjwa sikoseli kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kutambua vinasaba vinayochangia ugonjwa huo.
Amewataka wataalam wa afya kuhakikisha wanawapatia elimu ya kutosha wapenzi wanaogundulika na ugonjwa huo.
“Jambo hili lina ukakasi hasa wakati huu ambapo wapenzi wengi wanakutana mitandaoni lakini pia ni wakati ambapo huenda ndoa imeshatangazwa kanisani au msikitini, busara inatakiwa kutumika kuhakikisha watu hawa wanapewa elimu ya kutosha na inapotokea wameridhia hali zao au ya mmojawapo wajue namna ya kukabiliana kimalezi na kiuchumi pale mtoto anapozaliwa,” amesema Samike.
Latest
