Ugonjwa macho unavyowatesa wananchi Kanda ya Ziwa

November 6, 2021 6:15 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kugundulika katika kambi ya matibabu Mwanza.
  • Wadau kuanzisha taasisi maalum kupambana na ugonjwa huo.
  • Wananchi washauriwa kupima afya mara kwa mara ikiwemo macho.

Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando inatarajia kuanzia taasisi ndogo ya kuchunguza tatizo la ugonjwa wa macho baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mkoa wa Mwanza wanakabiliwa na tatizo hilo.

Kusudio hilo limejitokeza katika kilele cha utoaji wa huduma za kibingwa zinazotolewa na hospitali hiyo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 tangu hospitali hiyo kuanzishwa yaliyofanyika jana jijini hapa.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) na mwenyekiti wa shughuli hiyo, Profesa Costa Mahalu amesema katika kipindi hiki ambacho wamezunguka mikoa ya Kanda ya Ziwa kutoa huduma za kibingwa, tatizo kuu lilojitokeza kwa watu wengi waliowapima ni ugonjwa wa macho.

Profesa Mahalu amesema katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara na Simiyu walitoa huduma kwa wananchi 2,000 lakini nusu ya wagonjwa hao walibainika kuwa na tatizo la macho.

Tatizo kama hilo pia limeonekana katika Mkoa wa Mwanza ambapo kwa siku tatu za utoaji huduma, zaidi ya watu 1,800 wamejitokeza na nusu yao wamekuwa na tatizo la macho.

“Tatizo la macho ni janga kubwa si Mwanza tu hata mikoa ambayo tumepita tatizo hili limeonekana. Mfano kwa takwimu za hapa tu banda la wanaotoa huduma ya macho linaendelea kushughulika huku mengine yakiwa tupu,” amesema Prof Mahalu.

Ametaja takwimu hizo kwa siku  ya kwanza walihudumia wagonjwa 320, siku ya pili wagonjwa 219 na jana Novemba 5 ambayo nisiku ya mwisho hadi mchana walikuwa wamehudumia wagonjwa 259.

Magonjwa mengine yaliyobainika kuwatesa watu wengi ni ugonjwa wa koo na kifua.

“Kama hospitali tumeona ipo haja ya kuanzisha taasisi ndogo kwenye hospitali yetu itakayoshughulika na kuchunguza tatizo la macho ,” amesema  Prof Mahalu.

Mmoja wa madaktari akihojiana na mgonjwa aliyefika katika viwanja vya Furahisha kupata huduma mbalimbali za kibingwa zinazotolewa na hopsitali ya Rufaa ya Kanda Bugando. Picha |Mariam John.

Kwanini ugonjwa wa macho?

Daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Edwin Grayson amesema ugonjwa huo huusisha wagonjwa wenye tatizo la presha ya macho, aleji na mishipa ya fahamu ya kwenye macho.

Dk Grayson amesema wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na presha ya macho mara nyingi hupoteza uoni wao. 

“Mfano jana tulipokea wagonjwa wanne huko nyuma walibainika kuwa na presha ya macho wakaanzishiwa matibabu baadaye wakaacha tatizo limekuwa kubwa hali iliyosababisha kupoteza uoni wao,” amesema 

Dk Grayson amewashauri wananchi kujenga tabia ya kupima macho na afya zao mara kwa mara ili kujua afya na kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW