Kutana na mwanamke aliyeteswa na ugonjwa wa goita kwa miaka 12
- Ukosefu wa pesa kwa ajili ya matibabu wasababisha akae muda mrefu na ugonjwa huo.
- Afanyiwa upasuaji Oktoba kuondolewa uvimbe shingoni akisema “nimepata nafuu.”
- Wataalam wa afya washauri watu kwenda hospitali wanapohisi hali ya tofauti kwenye shingo zao.
Mwanza. Antonia Masanja ni mkazi wa Nansio wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza, alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa kuvimba shingo miaka 12 iliyopita.
Ugonjwa huo unaojulikana kwa jina la Goita alioupata ukubwani ulianza kwa uvimbe kidogo kujitokeza mbele ya shingo yake.
Antonia (43) ambaye ni mama wa watoto wanne anasema kadiri siku zilivyoenda uvimbe huo ulizidi kukua na kuongezeka kiasi cha kushindwa kuacha shingo yake wazi.
“Nilianza kuugua ugonjwa huu miaka 12 iliyopita, nilikuwa napata maumivu makali kwenye uti wa mgongo, napumua kwa shida, kichwa kuuma na wakati mwingine kulala kwa shida, lakini toka juzi (Oktoba 2, 2022) nilipofanyiwa upasuaji nimepata nafuu,” anasema Antonia akiwa katika hodi ya wagonjwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando mkoani hapa.
Mara ya kwanza alifika katika hospitali ya Rufaa Bugando mwaka 2015 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. Hata hivyo, hakufanyiwa upasuaji kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa.
Baada ya kufanyia upasuaji, hatakuwa na hofu tena kwa sababu uvimbe umeondolewa shingoni na anaweza kuendelea na majukumu yake mengine.
“Maumivu yapo lakini siyo sana kwa sasa nikirudi nyumbani naweza kufanya hata shughuli ndogo ndogo na kuondokana na utegemezi,” anasema.
Licha ya kuwa ugonjwa huo unatibika, watu wa Kanda ya Ziwa wana uelewa mdogo, jambo linalosababisha kutokuugundua mapema na kusababisha kutumia gharama kubwa wakati wa upasuaji.
Baadhi ya madaktari bingwa wa upasuaji wakiongezewa ujuzi na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani kufanya upasuaji wa magonjwa ya goita, pua na masikio hivi karibu katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando jijini Mwanza. Picha | Mariam John.
Fausta John ambaye anatibiwa katika hospitali hiyo, anasema alipata ugonjwa huo miaka mitano iliyopita.
Fausta ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Sengerema kabla hajafanyiwa upasuaji alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.
“Nilipofika hospitali niliwaonyesha madaktari na kueleza hali yangu baadae waliniandikia Kwenda hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi na baada ya kufika hapa nilitakiwa kufanyiwa upasuaj,” anasema Fausta.
Goita ni jina linalotumika katika kuliita tatizo la kuvimba kwa tezi ya thairoidi iliyo katika eneo la shingo.
Ugonjwa huu pia unaweza kutokea bila kuonekana uvimbe katika eneo hilo. Ugonjwa huu huwapata zaidi wanawake kuliko wanaume, hasa wale wanawake wasiopata muda wa kutosha wa kupumzika na kupata utulivu.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
-
Mikutano ilivyowazimisha viongozi wa ‘wasusa, twala’ Tanga
-
Vita mbichi: Wakazi wa Pangani wanavyohamasishana kupata chanjo ya Uviko-19
Wataalam waeleza undani wa ugonjwa huo
Daktari bingwa kutoka kitengo cha ‘Otolaryngology’ kinachojihusisha kutibu magonjwa ya koo, pua, kichwa, shingo na masikio katika hospitali ya Bugando, Dk Olivia Kimario anasema matatizo hayo yapo zaidi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Ugonjwa unaotesa zaidi ni wa goita kwa sababu ya kukosekana kwa madini ya chuma (Iodine).
Kwa mujibu wa ripoti ya ugonjwa huo katika Hospitali ya Rufaa Bugando ya kati ya mwaka 2020 hadi 2022, zaidi ya wagonjwa 200 wameshahudumiwa katika hospitali hiyo.
Dk Kimario anasema sababu kubwa inayochangia kuwepo kwa ugonjwa huo ni ukosefu wa madini ya chuma pamoja na tatizo la kurithi.
“Mara nyingi matatizo hayo pia yanabebwa na familia mfano ni haya magonjwa ya goita na mafindofindo ambapo unaweza kuta baba alikuwa na tatizo hilo miaka mingi ya nyuma tatizo hilo likaja kumpata mtoto wake au mjukuu,” anasema Dk Kimario.
Anasema tafiti zinaonyesha kuwa mtu mwenye tatizo la goita kwa kipindi kirefu cha miaka 10 hadi 15 kuna uwezekano wa ugonjwa huo kubadilika na kuwa kansa.
Amewashauri wananchi kuachana na imani potofu kuwa ugonjwa huo ni wa kulogwa bali wakimbilie hospitali ili kupata matibabu zaidi.
Hata hivyo, madaktari wa hospitali hiyo na wale kutoka Chuo Kikuu cha Weill Cornell cha nchini Marekani wametanua wigo wa kufanya utafiti zaidi kuhusu goita ili kuja na suluhu ya kudumu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
Tangazo:

Dalili za goita
Dalili kuu ya goita ni kuvimba au kuongezeka ukubwa kwa tezi ya thairoidi. Ukubwa wa tezi unaweza kuwa uvimbe mdogo katika tezi au uvimbe mkubwa kama nundu sehemu ya mbele ya shingo.
Kuvimba kwa tezi ya thairoidi kunaweza kusababisha mgandamizo katika njia ya hewa na mrija wa chakula, hali ambayo inaweza kusababisha shida katika kupumua, kikohozi, sauti kuwa ya mikwaruzo, kupata maumivu wa wakati wa kumeza chakula
Wakati mwingine, mishipa ya damu ya shingoni inaweza kuvimba pia na kusababisha mtu kujihisi kizunguzungu pindi anapoinua mikono yake juu.
Matibabu
Ili kuweza kutambua iwapo mgonjwa ana uvimbe kwenye tezi ya thairoidi, daktari huchunguza shingo ya mgonjwa pindi anapojaribu kumeza mate yake ili kuona kama kuna uvimbe unaopanda na kushuka wakati mgonjwa anapojaribu kumeza.
Daktari pia hupapasa sehemu za mbele za shingo ili kuchunguza iwapo kuna uvimbe wowote maeneo hayo. Baada ya vipimo mgonjwa atapatiwa matibabu.
Latest
