Tanzania yaimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya macho

April 7, 2022 9:12 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando yajenga yaanzisha taasisi ya macho.
  • Taasisi hiyo itatoa huduma za kibingwa za magonjwa ya macho. 

Mwanza.  Huenda wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wakapata uhakika wa matibabu ya macho baada ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kukamilisha ujenzi wa jengo jipya likalotumika kutoa huduma za kisasa kwa watu wenye matatizo ya macho.

Ujenzi wa jengo hilo umegharimu Sh2.4 bilioni ambapo litatumiwa na taasisi ndogo ya kuchunguza tatizo la magonjwa ya macho baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mkoa wa Mwanza wanakabiliwa na tatizo hilo.

Jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa  300 kwa siku na kulaza wagonjwa 50 kutoka wagonjwa 17 wa awali linatarajia kuanza kutoa huduma mapema mwezi Juni,  hatua itakayowapunguzia gharama baadhi ya wagonjwa waliolazimika kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kwa matibabu.

Akizungumzia ujenzj wa mradi huo, Meneja wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo, Anthony Mhanda amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 40,000 kwa mwaka ambao hupokelewa hospitalini hapo huku wagonjwa 50 wakilazwa na kupatiwa matibabu kwa siku.

“Ujenzi wa jengo umeshakamilika kilichobakia ni kuweka vifaa tiba na kumalizia miundombinu mingine ikiwemo kuweka vitanda, milango na Lifti ambayo nayo yatafanyika ndani ya mwezi huu,” amesema Mhanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Alicia Masenga amesema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika kliniki ya macho iliyoko katika hospitali hiyo.

“Kutokana na ufinyu wa eneo katika jengo la wagonjwa wa macho hospitalini hapa, baadhi ya wagonjwa hulazimika kusimama na kusubiria huduma lakini kuanzia Juni mwaka huu wagonjwa wanaokuja kutibiwa macho watakuwa na jengo lao maalum,” amesema Dk Masenga.


Soma zaidi: 


Wazo la kujenga jengo hilo lilijitokeza katika kilele cha utoaji wa huduma za kibingwa zinazotolewa na hospitali hiyo katika maadhimisho ya miaka 50 tangu hospitali hiyo kuanzishwa yaliyofanyika Novemba 21, 2021 jijini Mwanza.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Profesa Costa Mahalu alisema walizunguka mikoa ya Kanda ya Ziwa kutoa huduma za kibingwa, tatizo kuu lilojitokeza kwa watu wengi waliowapima ni ugonjwa wa macho.

Profesa Mahalu alisema katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara na Simiyu walitoa huduma kwa wananchi 2,000 lakini nusu ya wagonjwa hao walibainika kuwa na tatizo la macho.

Tatizo kama hilo pia lilionekana katika Mkoa wa Mwanza ambapo kwa siku tatu za utoaji huduma, watu 1,800 waliotibwa,  nusu yao waligundulika kuwa na tatizo la macho.

Mratibu wa miradi kutoka Chama cha Wasioona Mkoa wa Mwanza, Meshack Masanja amesema jengo hilo litapunguza usumbufu kwa wagonjwa wa macho Kanda ya Ziwa.

Amesema hivi sasa wagonjwa hulazimika kukwepa msongamano na kusafiri umbali wa kilometa 1,100 kufuata matibabu hayo katika hospitali ya Muhimbili na CCBRT jijini Dar es Salaam.

 

Sababu za gonjwa wa macho?

Daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Edwin Grayson amesema ugonjwa huo huusisha wagonjwa wenye tatizo la presha ya macho, aleji na mishipa ya fahamu ya kwenye macho.

Dk Grayson amesema wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na presha ya macho mara nyingi hupoteza uoni wao. 

“Mfano jana tulipokea wagonjwa wanne huko nyuma walibainika kuwa na presha ya macho wakaanzishiwa matibabu baadaye wakaacha tatizo limekuwa kubwa hali iliyosababisha kupoteza uoni wao,” amesema.  

Dk Grayson amewashauri wananchi kujenga tabia ya kupima macho na afya zao mara kwa mara ili kujua afya na kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW