Ufahamu ugonjwa wa hantavirus

May 15, 2026 10:26 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kundi la virusi vinavyoenezwa na panya, vilivyogunduliwa rasmi mwaka 1976 karibu na Mto Hantan nchini Korea Kusini.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kuishi na kumbukumbu za athari za janga la Uviko 19, watalaamu wa afya wanaonya kuhusu wimbi jipya la virusi vya ‘hantavirus’  vinavyoenezwa na panya.

Taarifa za ugonjwa huo ziligonga vichwa mbalimbali duniani kuanzia mwanzoni mwa mwezi Mei 2026 na kuwaacha maelfu kwenye sintofahamu ya ugonjwa huo na hatari ya kuzuka kwa janga jipya.

Mei 4, 2026 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilithibitisha vifo vya watu watatu kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo ulioripotiwa ndani ya meli ya kitalii MV Hondius iliyokuwa ikisafiri katika Bahari ya Atlantiki kutoka Argentina kuelekea Cape Verde.

Taarifa hiyo ya WHO ilithibitisha watu sita kutoka katika meli hiyo kuambukizwa ugonjwa huo huku watatu tayari wakiripotiwa kupoteza maisha.

Ufahamu ugonjwa wa ‘hantavirus’

Hantavirus ni kundi la virusi vinavyoenezwa na panya, vilivyogunduliwa rasmi mwaka 1976 karibu na Mto Hantan nchini Korea Kusini vikiwashambulia mamia ya wanajeshi waliokuwa wakifanya kazi mashambani  kati ya mwaka 1950 hadi mwaka 1953.

Kadri miaka ilivyosogea, wataalamu wa afya waliendelea kugundua aina mbalimbali za virusi hivi katika maeneo tofauti duniani, hasa Asia, Ulaya na bara la Amerika. 

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, wastani wa maambukizi ya hantavirus duniani hufikia kati ya watu 10,000 hadi zaidi ya 100,000 kila mwaka huku kiwango cha vifo kikikadiriwa kufikia asilimia 20 hadi 40.

Ingawa hantavirus si maarufu kama Covid-19, (Uviko -19) wataalamu wa afya duniani wanautazama kwa umakini mkubwa ugonjwa huo kutokana na uwezo wake wa kusababisha madhara makubwa katika mfumo wa upumuaji, moyo pamoja na figo za binadamu. 

Dalili za ugonjwa wa ‘hantavirus’

Kwa mujibu wa WHO, Dalili za hantavirus huanza kujitokeza kati ya wiki moja hadi nane baada ya mtu kuambukizwa. 

Mara nyingi mgonjwa huanza kuhisi homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli pamoja na uchovu mkubwa. 

Wengine hupata maumivu ya tumbo, kichefuchefu na kutapika hali inayoweza kufanana na magonjwa mengine ya kawaida kama mafua au Covid-19.

Kadri ugonjwa unavyoendelea, hali ya mgonjwa inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kupata kikohozi kikali, shida ya kupumua pamoja na maji kujaa kwenye mapafu. 

Katika baadhi ya wagonjwa, presha hushuka, damu inaweza kutoka sehemu mbalimbali za mwili na figo kushindwa kufanya kazi vizuri. 

Licha ya dalili hatari za ugonjwa huo, WHO inasema kwa sasa hakuna matibabu  ya moja kwa moja ila msaada wa haraka wa kitabibu huweza kutolewa ili kuokoa maisha ya mgonjwa kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mfumo wa upumuaji, moyo na figo.

Hantavirus huambukizwaje?

Hantavirus huambukizwa zaidi kutoka kwa panya kwenda kwa binadamu kupitia mkojo, mate au kinyesi cha panya walioambukizwa.

Mtu anaweza kupata maambukizi kwa kuvuta hewa yenye chembechembe za uchafu wa panya hao, hasa wakati wa kusafisha maeneo yaliyofungwa kwa muda mrefu kama maghala, vyumba vya kuhifadhia vitu au nyumba zisizotumika.

Maambukizi yanaweza pia kutokea kwa kugusa vitu vilivyochafuliwa na panya au kung’atwa na panya mwenye maambukizi. 

Watu wanaofanya kazi mashambani, misituni au wanaoishi katika mazingira yenye panya wengi huwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Uhusiano kati ya hantavirus na Corona (Covid-19)

Ingawa hantavirus na Uviko 19 ni magonjwa tofauti kabisa, yote mawili yanafanana katika baadhi ya dalili za mwanzo. 

Mgonjwa wa hantavirus anaweza kupata homa, uchovu, maumivu ya misuli na shida ya kupumua, dalili ambazo pia huonekana kwa wagonjwa wa Covid-19. 

Kutokana na kufanana huku, wakati mwingine madaktari hulazimika kufanya vipimo maalumu ili kutofautisha ugonjwa mmoja na mwingine.

Tofauti kubwa ni kwamba Covid-19 husambaa kwa urahisi sana kutoka mtu mmoja kwenda mwingine kupitia hewa, wakati hantavirus huambukizwa zaidi kutoka kwa panya kwenda kwa binadamu.

Aidha, vipimo vya damu pamoja na vipimo vya maabara kama RT-PCR hutumika kuthibitisha uwepo wa virusi hivyo mwilini.

Namna ya kujikinga

Njia bora ya kujikinga dhidi ya hantavirus ni kudhibiti mazingira yanayoweza kuvutia panya. 

Watu wanashauriwa kuweka nyumba na maeneo ya kazi katika hali ya usafi wakati wote pamoja na kuziba mianya inayoweza kuruhusu panya kuingia ndani.

Pia ni muhimu kuhifadhi chakula vizuri ili kutowavutia panya na kutumia njia salama wakati wa kusafisha maeneo yenye kinyesi au mkojo wa panya.

Wataalamu wanashauri maeneo hayo yanyunyiziwe maji au dawa maalumu kwanza badala ya kufagia moja kwa moja, ili kuepuka kusambaza chembechembe za virusi hewani.

Kunawa mikono mara kwa mara na kutumia vifaa vya kujikinga wakati wa usafi pia ni hatua muhimu za kujilinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

Nukta TV