Nusu ya kidato cha nne 2021 wapata daraja la IV
- Watahiniwa 248,966 sawa na asilimia 51.5 ya watahiniwa wote wamepata daraja la IV.
- Wanafunzi 61,432 wapata daraja sifuri.
Dar es Salaam. Wakati wazazi na wanafunzi wakiendelea kufanya tathmini ya matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2021, matokeo hayo yanaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamepata daraja la nne huku asilimia 12.7 wakifeli kabisa.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa leo Januari 15, 2022 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), watahiniwa wa shule 422,388 sawa na 87.3 kati ya watahiniwa 483,820 wenye matokeo ya kidato cha nne wamefaulu mitihani yao muhimu kuingia katika elimu ya kidato cha tano.
“Ufaulu wa watahiniwa umeongezeka kwa asilimia 1.46 ikilinganishwa na mwaka wa 2020,” amesema Dk Msonde.
Licha ya ufaulu huo kuongezeka, uchambuzi wa matokeo hayo uliofanywa na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) umeonyesha watahiniwa 248,966 sawa na asilimia 51.5 ya watahiniwa wote wamepata daraja la IV.
Hiyo ni sawa na kusema kwa kila wanafunzi 10 waliofanya mtihani huo, watano wamepata daraja la IV, hivyo wanaweza kukosa fursa ya kwenda kidato cha tano licha ya daraja hilo kuwa sehemu ya watahiniwa waliofaulu kwa mujibu wa Necta.
Soma zaidi:
-
Shule 10 bora matokeo ya kidato cha nne 2021
-
Mwanafunzi bora kidato cha nne 2021 ataja siri za ushindi
-
Matokeo kidato cha nne 2021 hadharani
Wakati zaidi ya nusu ya watahiniwa wakipata daraja la IV, wanafunzi 61,432 sawa na asilimia 12.7 wakipata daraja sifuri au sawa na kusema watahiniwa 12 katika ya 100 waliofanya mtihani huo wamefeli kabisa.
Kwa ufaulu huo, watahiniwa 310,398 sawa na asilimia 64.2 wamepata madaraja mawili ya IV na 0 ambayo ni ya chini katika mpangilio wa ufaulu katika mtihani wa kidato cha nne.
Ufaulu huo, wanafunzi hao wanaweza kukosa fursa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita ambalo ni daraja muhimu kuelekea elimu ya juu.
Wanafunzi hao watakuwa na uchaguzi wa kurudia mitihani au kwenda katika elimu mbadala ikiwemo ya ufundi stadi.
Wakati watahiniwa hao wakikosa fursa ya kwenda kidato cha tano, wenzao 81,371 waliopata daraja la I hadi la III wana uhakika wa kuchaguliwa kujiunga na ngazi hiyo ya elimu kwa sababu ufaulu wao unaridhisha.
Latest



