Naibu Spika Zungu awashangaa wanaolalamikia tozo miamala ya simu
- Asema kwa nini hawalalamiki gharama wanazokatwa na makampuni ya simu na benki.
- Adai gharama hizo ziko juu kuliko tozo ya Serikali.
- Ashauri gharama hizo zipitiwe upya ili kupunguza malalamiko ya wananchi.
Dar es Salaam. Naibu Spika Mussa Azzan Zungu amewashangaa baadhi ya wananchi wanaolalamikia tozo za miamala ya simu na benki na kuachwa kuzungumzia fedha wanazokatwa na makampuni ya simu wanapotoa au kutuma pesa.
Amesema makato ya makampuni hayo ni makubwa kuliko tozo ya Serikali.
“Jana Serikali imetangaza kupunguza gharama za miaamala, lakini wananchi wengi wanalalamikia kodi ya Serikali, hawatazami mapato yanayokatwa na mabenki na makampuni ya simu,” amesema Zungu leo Septemba 21, 2022 Bungeni jijini Dodoma.
Naibu Spika Zungu ambaye pia ni Mbunge wa Iala amehoji kwa nini Serikali “ipigwe madongo” kwa tozo ambazo zinatumika kuboresha huduma za kijamii na kuacha hoja ya fedha wanazotozwa wananchi wakati wanafanya miamala ya fedha kwa njia za kielektroniki ikiwemo simu.
“Lazima hii iwe regulated (isimamiwe), benki unatuma pesa wanachukua pesa nyingi zaidi ya Serikali, lakini Serikali inayojenga madarasa na vituo vya afya ndiyo inalaumiwa.
“Kwa hiyo kuna ki-syndicate (mtandao) kinatengenezwa kuipiga dongo Serikali wakati pesa wanachukua watu wengine, hili litazamwe ni namna gani mta regulate (mtasimamia) mapato ya benki kupunguza gharama za service charge (huduma) zao pamoja na gharama za simu,” amesema Zungu wakati akihitimisha kipindi cha maswali na majibu.
Amesema mchanganuo wa makato wakati wa kutoa au kutuma pesa kwa njia ya simu yanaonyeshwa kabla mtu hajakamilisha muamala, “utaona makato ya Serikali yapo chini sana na mapato wanayochukua makampuni ya simu na taasisi za kifedha yapo juu zaidi.”
April 2021, akiwa Bungeni, Zungu aliishauri Serikali kuanzisha kodi ya uzalendo ambayo itakauwa inakatwa katika mitandao ya simu kwa siku kama chanzo kipya cha mapato.
“TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) msidumae kukamata Bakhresa, Mohammed Dewji sijui Enterprises tafuteni vyanzo vipya kuna hela nyingi kwenye simu,” alisema Zungu.
Julai 1 mwaka huo huo, Serikali ilianza kukata tozo ya miamala ya simu na baada ya hapo kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuwa tozo hizo zinawaongezea ukali wa maisha na kuwapunguzia kasi ya ujumuishaji wa kifedha.
Soma zaidi:
-
Tozo miamala ya simu kupunguzwa Tanzania
-
Ahueni: Serikali ikipunguza, kufuta baadhi ya tozo za simu, benki
-
Tozo miamala ya simu bado “pasua kichwa”
Jana Septemba 20, 2022, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali imefanya mabadiliko ya tozo za miamala simu na benki kwa kufuata na kupunguza baadhi ya tozo hizo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi.
Dk Nchemba aliyekuwa akitoa taarifa ya Serikali kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya mwaka 2021, bungeni jijini Dodoma leo Septemba 20, 2022 alisema Serikali imepunguza tozo ya miamala ya simu na benki kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kwa kuzingatia makundi na gharama za miamala husika.
Pia imefuta tozo ya miamala kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu, kuhamisha fedha ndani ya benki moja na kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.
Iimetoa msamaha wa tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na mashine za kutolea na kuweka fedha (ATM) kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh30,000.
Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa Oktoba 1, 2022.
Latest