Ahueni: Serikali ikipunguza, kufuta baadhi ya tozo za simu, benki

September 20, 2022 8:07 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imepunguza tozo ya miamala ya simu kwa asilimia 10 hadi asilimia 50.
  • Imefuta tozo ya baadhi ya miamala ya benki ikiwemo kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mtandao wa simu.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imefanya mabadiliko ya tozo za miamala simu na benki kwa kufuata na kupunguza baadhi ya tozo hizo ili kuwaletea unafuu wananchi wa Tanzania. 

Huenda hatua hiyo itatoa ahueni kwa Watanzania ambao wamekuwa wakilalamikia gharama za miamala hiyo ikiwemo kukatwa mara mbili, licha ya Serikali kusisitiza kuwa tozo hizo zimekuwa na manufaa makubwa katika uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya.

Dk Nchemba aliyekuwa akitoa taarifa ya Serikali kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Tozo za Miamala ya Simu ya Kutuma na Kupokea kwa njia ya Kielektroniki ya mwaka 2021, bungeni jijini Dodoma leo Septemba 20, 2022 amesema Serikali imepunguza tozo ya miamala ya simu na benki kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kwa kuzingatia makundi na gharama za miamala husika.

“Asilimia hizo zitazingatia makundi ya miamala na gharama zilizopo kwenye miamala katika makundi hayo,” amesema Nchemba mbele ya Wabunge. 

Tangu kuanzishwa kwake, kiwango cha tozo kilipunguzwa kwa asilimia 30 mwezi Septemba 2021 na kikapunguzwa tena Julai mwaka huu na hivyo kufanya punguzo la jumla la asilimia 60 ya kiwango cha kilichowekwa awali.

Na sasa kimepunguzwa tena ikiwa ni hatua ya kuwaletea wananchi unafuu wakati wakitumia huduma za kifedha na kujibu malalamiko yao kuhusu tozo hizo.

“Kufuatia malalamiko hayo Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan ilielekeza Serikali kufanya mapitio ya miamala kwa kuzingatia maoni ya wananchi.

“Wizara ya fedha ilipitia tozo hizo na kufanya mapitio kama ifatavyo: kupunguza wigo kwa tozo kwa jamii, kuchochea matumizi ya miamala kwa ajili ya kupunguza fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia utozaji wa tozo husika mara mbili,” amesema waziri huyo. 

Mabadiliko hayo yataanza kutekelezwa Oktoba 1, 2022.


Soma zaidi:



Ahueni hadi kwa watumiaji wa benki

Serikali imefuta tozo ya miamala kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu, kuhamisha fedha ndani ya benki moja na kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine.

Pia imetoa msamaha wa tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na mashine za kutolea na kuweka fedha (ATM) kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh30,000.

Walengwa hapa ni wananchi wanaotoka katika kaya maskini na wanaopokea fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).


“Tutabana matumizi”

Kutokana na punguzo na kufuta baadhi ya tozo za miamala ya simu na benki, Waziri Nchemba amesema fedha zitakazopungua katika tozo hizo zitafidiwa kwa kubana matumizi ya Serikali  ikiwemo mafungu ya chai, vitafunwa, misafara kwenye safari/ziara, mafunzo, semina, warsha na matamasha.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa tozo za miamala zimeendelea kuwa na manufaa makubwa katika maendeleo ya nchi ikiwemo kuchagiza ujenzi wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji.

“Serikali ilitumia jumla ya Sh147.7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo kati ya fedha hizo, Sh117 bilioni sawa na asilimia 81.4 zilitokana na tozo ya miamala,” amesema Mwigulu. 

Nyongeza na Daniel Samson

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW