Tanzania, Indonesia kuimarisha ushirikiano
- Ni katika nyanja za biashara, utalii, nishati na teknolojia
- Ni fursa kwa Tanzania kupata fedha za kigeni kupitia biashara
Dar es Salaam. Tanzania na Indonesia zimekubaliana kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina yao katika nyanja za biashara, utaliii, nishati na teknolojia kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa yote mawili.
Indonesia ni miongoni mwa mataifa ya awali kuanzisha ushirikiano na Tanzania mara baada ya kupata uhuru ambapo ilifungua ubalozi nchini mwaka 1963.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza na waaandishi wa habari Ikulu leo Agosti 22, 2023, amewaambia Watanzania kuwa wamekubaliana kudumisha ushirika na urafiki uliopo katika nyanja za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya nchi zote mbili.
“Licha ya uhusiano wetu wa kidiplomasia, tumekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi yaani Public-Public and Public Private Partnership,” amesema Rais Samia jijini Dar es Salaam.
Rais Samia ameongeza kuwa wameridhia kuimarisha zaidi ushirikiano katika viwanda, kilimo, nishati, utalii, sekta za ukarimu na kubadilishana teknolojia.
Soma zaidi
-
Teknolojia ya vifuu vya nazi itakavyo waokoa wachimbaji na madhara ya zebaki
-
Ujuzi wa kidijitali unaoweza kuwatoa vijana kimaisha
Kwa upande wake Rais wa Indonesia Joko Widodo ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili amesema tutafanya kwa vitendo kuhakikisha ushirikiano thabiti.
“Tupo hatua za mwisho kuandaa mpango wa maendeleo wa miaka mitano kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupitia uhuishaji wa kituo cha mafunzo ya kilimo na vijijini kwa mkulima mkoani Morogoro”
Aidha Rais Widodo amesema amependekeza kuanzishwa kwa mkataba wa pande mbili ili kuhakikisha makubaliano hayo ambayo Indonesia imeridhia kuwa sehemu ya uboreshaji uchumi wa Tanzania.
Ziara ya Rais Widodo ni ya pili kufanywa na kiongozi kutoka taifa hilo ambalo lina wananchi milioni 273 baada ya rais Surhato
Mahusiano ya kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili yalianza mwaka 1955 kupitia mataifa yasiofungamana (NAM) na kisha yaliendelea kukomaa baadae ambapo wataalamu wa kilimo kutoka Indonesia walikuwa wakitoa mafunzo ya kilimo mkoani Morogoro.
Ni faida kwa Watanzania
Maggid Mjengwa mwanadiplomasia kutoka Tanzania ameiambia Nukta Habari kuwa ushirikiano huo ni fursa kwa Watanzania kufanya biashara na kupata fedha za kigeni kwa kuwa Indonesia ina soko kubwa la watu kutokana na idadi ya watu wengi waliopo nchibi humo.
Kwa mujibu wa kanzi data ya UN Comtrade ya mwaka 2022, Indonesia ilivuna Dola za Marekani milioni 78 kutokana na mafuta ya mchikichi wakati Tanzania ikivuna Dola za Marekani milioni 28 kutokana na bidhaa za kakao, tumbaku na karafuu.
Latest
