Tanzania na Ujerumani kuendeleza ushirikiano

October 31, 2023 11:46 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ushirikiano huo ulianza miaka 60 iliyopita.
  • Wafanyabiashara, wajasiriamali kukutana na Rais Steinmeier.

Dar es Salaam.Tanzania na Ujerumani zimefungua ukurasa mpya katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii uliodumu kwa zaidi ya miaka 60.

Uhusiano baina ya nchi hizo mbili ulianza miaka kadhaa baada ya Tanzania kupata uhuru katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo,utalii, michezo, udhibiti wa fedha, utamaduni pamoja na shughuli za kiuchumi ikiwemo biasahara na uwekezaji.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Oktoba 31, 2023 jijini Dar es Salaam baada ya kumpokea Rais wa Shirikisho la Ujerumani Frank Walter Steinmeier, aliyepo nchini Tanzania kwa ziara ya siku tatu.

Amesema katika mazungumzo aliyofanya na kiongozi huyo wamekubaliana  kuendeleza uhusiano baina ya nchi hizo kupitia timu za wataalamu kutoka nchi zote mbili.

 “Katika hili tumezielekeza timu za wataalamu kutoka Tanzania na Ujerumani kuendelea na mazungumzo pamoja na mashauriano ya mara kwa mara yanayolenga kuimarisha mahusiano na kuibua maeneo mapya yanayolenga kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili,” amesema Rais Samia.


Soma zaidi: Udumavu, mimba za utotoni, kuwaweka wakuu wa mikoa kikaangoni


Huenda ziara hiyo ya siku tatu ya Rais Steinmeier nchini Tanzania ikakuza shughuli mbalimbali za kiuchumi zilizokuwa zikifanyika kati ya Tanzania na Ujerumani ikiwemo biashara.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Sh105 bilioni sawa na Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka. 

Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni pamoja na kahawa, tumbaku, pamba, asali, samaki, nta na vito vya thamani.

Naye Rais Steinmeier, amemshukuru Rais Samia kwa kumualika nchini Tanzania na kuahidi kuwa ziara yake nchini Tanzania itaongeza uwekezaji utakaofanyika katika maeneo mbalimbali.

“Urafiki huu uliokuwepo kwa miaka kadhaa sasa utaendelea kuwepo kwasababu ya uaminifu ambao tunao baina ya nchi hizo mbili…tuko hapa kuahidi kwamba tutaendelea kuwekeza katika ukadha huu,” amesema Rais Steinmeier.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanahabari kuhusu ziara ya  Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Frank Walter Steinmeier nchini Tanzania.Picha|Ikulu.

Wafanyabiashara,wajasiriamali kukutana na Rais Steinmeier

Katika kuendeleza na kukuza shughuli za biashara nchini Rais Steinmeier na Rais Samia wanatarajiwa kutashiriki katika jukwaa la biashara  litakalohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa kushirikiana TIC.

Kwa mujibu wa Rais Samia kupita jukwaa hilo wafanyabiashara wa Ujerumani na Tanzania watapata nafasi ya kuzungumza na kutambua fursa za uwekezaji na shughuli nyingine za kibiashara zilizopo.

“Huko ndipo fursa zote za uwekezaji na biashara zitaelezwa na pengine watakaokubaliana wataingia mikataba ya makubaliano,” amesema Rais Samia.

Pia, Rais Steinmeier atakutanana kuzungumza na vijana wajasiriamali wa Kitanzania wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia ikiwemo matumizi ya akili bandia ambaounafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW