Ujuzi wa kidijitali unaoweza kuwatoa vijana kimaisha
- Miongoni mwa ujuzi ni kuweza kutumia mitandao vizuri kuuza wasifu.
- Ni vizuri vijana wakajifunza matumizi ya akili bandia, uwezo wa kuchambua data na kutafuta masoko mtandaoni.
Wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya kimataifa ya vijana, nchini Tanzania kundi hili linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ukosefu wa ajira, mitaji na ujuzi wa kutosha kuweza kufaidi fursa za kiuchumi zilizopo.
Hadi sasa Tanzania ina zaidi ya vijana milioni 20.53 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 34 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na kufanya kuwa kundi kubwa katika taifa hili la Afrika Mashariki likiwa ni theluthi ya watu wote.
Hata hivyo, tofauti na miaka ya nyuma kundi hili linaishi katika zama za mabadiliko ya kasi ya teknolojia yanayochochea ukuaji wa mapinduzi ya nne ya viwanda hasa uchumi wa kidijitali unaoibua fursa lukuki za kimaendeleo.
Licha ya kuwepo fursa za kidijitali bado vijana wengi hawana ujuzi maridhawa utakaowafanya waweza kushindana katika soko la ajira ama kuanzisha na kuendesha biashara zao.
Soma zaidi
-
Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
-
Sarufi AI teknolojia ya akili bandia inayorahisisha mawasiliano
Baadhi ya wadau wa masuala ya uchumi wa kidijitali wameiambia Nukta Habari kuwa kwa sasa ujuzi unaohitajika zaidi kwa vijana ni matumizi ya akili bandia, ubunifu, kusimba (coding), usalama wa mtandao, elimu ya kidijitali, utengenezaji wa maudhui, uchambuzi wa data, masoko ya mitandaoni, masoko ya kidijitali.
Mkurugenzi wa kampuni ya habari na teknolojia ya Ona Stories Technologies Princely Glorious anasema awali ujuzi wa kidijitali ulionekana kama jambo la siku za usoni sana lakini mtazamo huu hauwezi kutoboa kwa sasa.
Kwa nini vijana wajikite katika ujuzi wa kidijitali
“Ujuzi wa kidijitali ni hitaji la sasa…kutoka ujuzi wa kimsingi wa kusoma na kuandika hadi teknolojia ya hali ya juu zaidi, kujua na kutumia ujuzi wa kidijitali ndio tofauti kati ya kukua na kufa katika nguvu kazi leo,” anasema Glorious ambaye kampuni yao huzalisha na kufundisha vijana matumizi ya kuzalisha maudhui kidijitali kwa teknolojia ya uhalisia pepe (Virtual Reality).
Glorious anasema kwa kijana mtaalamu wa uuzaji ambaye ni mjuzi katika uchanganuzi wa data na majukwaa ya utangazaji mtandaoni anaweza kulenga soko kwa usahihi, kuboresha kampeni na kuchanganua vipimo vya utenda kazi kwa wakati halisi.
Utengenezaji wa fursa za ajira kwa vijana katika uchumi wa sasa unahitaji bidii hasa katika mambo matatu msingi: uimarishaji wa sera wezeshi, upatikanaji wa mtandao wa intaneti yenye gharama nafuu na uhakika wa upatikanaji wa ujuzi wa kidijitali.
Vijana wawili kati ya watatu hawana ujuzi kidijitali
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 67% ya vijana ulimwenguni wakiwemo wa Tanzania hawana ujuzi wa kidijitali kutokana na kutokuwa na rasilimali wezeshi kama intaneti na kompyuta. Hii ina maana kuwa vijana wawili kati ya watatu duniani hawana kabisa ujuzi wa kidijitali, jambo linalowanyima fursa za kiuchumi ambazo zingewatoa kwenye lindi la umaskini.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri soko la ajira zote kwa asilimia 40. Mamlaka zinajikita katika kuboresha hali hii kwa matumizi ya nishati na kilimo mbadala.
Licha ya baadhi ya vijana kuwa na shauku ya kujifunza zaidi masuala ya kidijitali kufurahia fursa za kijamii na kiuchumi, ni wachache wanafahamu namna ya kuanza na wapi wazipate fursa husika.
Jenga wasifu wako mtandaoni, jifunze matumizi ya ‘Artificial intelligence’
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Vodacom Tanzania Annette Kanora ameiambia Nukta Habari kuwa vijana wanaweza kuanza na vitu vya msingi kama ufasaha wa kutumia kompyuta na kutengeneza wasifu mzuri.
Katika safari hiyo ya kujifunza, anasema wasisahau kujinoa namna sahihi ya matumizi ya akili bandia maarufu kwa kimombo kama Artificial Intelligence kwa kuwa yana faida kubwa siku hizi tofauti na awali.
“Serikali inafanya jitihada nyingi lakini tusibweteke kuisubiria…simu za mkononi zimekua sehemu ya mapinduzi katika kujifunza masuala ya kidijitali, mambo yote yako mtandaoni, kuna maktaba tele…
“Soko la ajira ni shindani kila siku na ujuzi ndio unaokuweka mbele na wewe ni chapa binafsi unatakiwa kufahamu namna ya kujiweka mbele ya wenzio.” Anasema Annette.
Teknolojia za dijitali zinabadilisha uchumi
Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2021 inasema teknolojia za kidijitali zimebadilisha uchumi wa dunia kwa haraka na inatarajiwa kuendelea kufanya hivyo kwa kuongeza kasi, ubunifu, viwanda vipya katika mchakato huo ambazo zitaongeza fursa za kutengeneza ajira mpya, kuongeza tija na mapato na kupunguza umaskini.
Kuongezeka kwa idadi ya kazi zilizopo na karibu kazi zote mpya huko usoni kunaitahitaji ujuzi wa dijitali ambapo zaidi ya kazi milioni 230 Kusini mwa Jangwa la Sahara zitahitaji ujuzi wa dijitali ifikapo 2030. Watu ambao watakua hawana ujuzi huu unaohitajika, wana hatari ya kupunguza uwezo wao katika ajira kwa siku zijazo na kufaidika mapinduzi ya kidijitali.
Katika nyakati tofauti Serikali ya Tanzania imeonyesha nia ya kuboresha mazingira ya biashara ili kukuza fursa za kidijitali ikiwemo kuongeza upatikanaji wa huduma ya intaneti yenye kasi baada ya juzi kuzindua mkongo wa taifa wenye kasi ya 5G.
Septemba 2022 Tanzania yenye watumiaji wa intaneti milioni 34 kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikuwa nchi ya pili Afrika Mashariki kuwa na mtandao wenye kasi ya 5G baada ya Vodocom kuzindua huduma hiyo jijini Dar es Salaam. Hadi sasa kampuni nyingine za Tigo na Airtel zimezindua mtandao wa kasi hiyo.
Licha ya hatua hizo, bado Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikikosolewa vikali kwa kushindwa kudhibiti gharama za vifurushi vya intaneti ambayo inatumika zaidi na vijana kujitafutia ridhiki kupitia kutengeneza maudhui na shughuli nyingine za kidijitali.
Vijana wanatakiwa kila mara kujifunza vitu vipya vinavyoendana na mahitaji ya sasa.PichalNukta Africa
Latest



