Teknolojia ya vifuu vya nazi itakavyo waokoa wachimbaji na madhara ya zebaki

Esau Ng'umbi 0455Hrs   Agosti 05, 2023 Habari
  • Inaitwa ‘Activated carbon’ inayotengenezwa kwa kutumia vifuu vya nazi.
  • Itasaidia kupunguza athari za mazingira na kiafya zitokanazo na matumizi ya zebaki.
  • Itaokoa zaidi ya Sh15 bilioni zinazotumika kuagiza activated carbon kutoka nje ya nchi.


Dar es Salaam. Huenda wachimbaji wadogo wa madini Tanzania wakaepukana na athari za afya pamoja na uchafuzi wa mazingira ikiwa wataasili matumizi ya bidhaa mpya ya kusafishia madini (Activated carbon) inayozalishwa nchini.

Bidhaa hiyo inayotengenezwa kwa kutumia vifuu vya nazi itachochea uzalishaji wa madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa  kwa kuwa itapatikana kwa urahisi jambo litakaloongeza kasi katika shughuli za uchenjuaji huku mazingira na wachimbaji wakwa salama.

Upatikanaji wa bidhaa hiyo mbadala wa zebaki katika shughuli za uchechuaji itakuwa mkombozi kwa wachimbaji pamoja na jamii ambayo inaweza kuathirika kwa kwa kuvuta hewa, kula chakula au maji yaliyo na sumu ya zebaki.

Shirika la Afya Duniani (WHO), linabainisha kuwa athari za kiafya zitokanazo na zebaki ni pamoja na kuharibiwa kwa mifumo ya neva, kuharibiwa kwa mfumo wa upumuaji, mmeng’enyo, mifumo ya kinga, figo, mapafu na wakati mwingine husababisha kifo.

WHO wamesisitiza kuwa sumu hiyo inaweza kusababisha magonjwa katika mfumo wa fahamu ikiwemo kifafa, kupoteza uwezo wa kuona au kusikia, udumavu pamoja na kupoteza kumbukumbu

Mpango Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki 2020/25 unabainisha kuwa zebaki ni miongoni mwa kemikali hatarishi inayosababisha athari kwa afya ya binadamu na mazingira duniani.

Activated carbon hutumika kwenye shughuli za uchenjuaji madini, kuchuja maji pamoja na kutibu maji taka.PichalEsau Ng'umbi/Nukta

Kwa mujibu wa muongozo huo, sekta ya wachimbaji wadogo ndio inaongoza kwa matumizi ya kemikali hiyo hatari jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya uchafuzi wa mazingira unaotokana na zebaki.

Tiberius Mario, Mkurugenzi wa Kampuni ya Timasu inayojihusisha na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na nazi, ameiambia Nukta Habari kuwa alipata wazo la kutengeneza activated carbon baada ya kufanya utafiti wa namna gani vifuu vya nazi vinaweza kutengeneza bidhaa nyingine.

Uhaba wa teknolojia hiyo nchini Tanzania ulimsukuma zaidi kujikita katika uzalishaji wa bidhaa hiyo ambayo hutumika pia kusafisha maji viwandani pamoja na kutibu maji taka.

“Tulibaini Tanzania tunaagiza activated carbon kwa asilimia 100, tunapoteza zaidi ya Dola milioni 6.7 za Marekani sawa na Sh15.9 bilioni kila mwaka,” amesema Mario.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya Trend Economy inayochapisha taarifa za uchumi na data mwaka 2022, Tanzania iliiingiza bidhaa zinazohusiana na activated carbon zilizo kundi namba 3802 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 13.2 ambayo ni sawa na Sh32.4 bilioni.


Soma zaidi


Mario ameongeza kuwa kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi husababisha kupanda kwa bei yake hasa pale inapoadimika. Mathalani mwaka 2022 activated carbon ilipanda kutoka Sh15,000 kwa kilogramu hadi Sh25,000 jambo linalochochea matumizi ya kemikali zisizofaa ikiwemo zebaki.

Takwimu zinabainisha kuwa watu milioni 8.4 wamepata ajira za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja kupitia sekta ya uchimbaji mdogo ambao hutumia tani 13.2 hadi 24.4 za zebaki kila mwaka.

Idadi ya watu wanaojihusisha na uchimbaji mdogo ni sawa na asilimia 13 ya watu waliopo Tanzania kwa sasa kwa mujibu wa Sensa ya watu ya mwaka 2022.

Hii ina maana kuwa katika watu 100 nchini, 13 kati yao wanajihusisha na uchimbaji mdogo hivyo wapo hatarini kiafya au wanachafua mazingira iwapo aina ya uchimbaji wao kama wa dhahabu utatumia zebaki.

Tanzania imekalia utajiri

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, mpaka mwaka 2020 Tanzania ilikuwa nafasi ya 10 kwa uzalishaji wa nazi duniani, huku ikishika nafasi ya kwanza barani Afrika ambapo ilikuwa inazalisha tani 530,000 za nazi kwa mwaka.

Hata hivyo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (Tari) inakadiria kwamba uzalishaji huo unaweza kufikia hadi tani 800,000 ikiwa Tanzania itaongeza mikakati madhubuti ya uzalishaji wa zao hilo.

Mario ameiambia Nukta Habari kuwa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 50,000 za vifuu vya nazi ambavyo vikichakatwa vinaweza kutoa tani tisa za  activated carbon kiwango ambacho kinatosha kusambaza katika soko la Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Mario ambaye ni mwanzilishi kwa kampuni ya Timasu  hivi sasa wanafanya utaratibu wa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili  kusambaza bidhaa hiyo katika vituo vya madini vinavyosimamiwa na shirika hilo.

Kiunzi cha kuruka

Ikiwa watafanikiwa kupata tenda hiyo ya kusambaza activated carbon maana yake watatakiwa kuongeza uzalishaji wa kufikia angalau tani 100 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya bidhaa hiyo, kwani kwa sasa wanauwezo wa kuzalisha kilogram 120 pekee kwa siku.

Ili kuongeza uzalishaji, Mario anawaomba wadau kuwashika mkono kuwawezesha kupata mashine itakaongeza uzalishaji wa kufikia angalau tani moja kwa siku kukidhi mahitaji ya soko.

“Mahitaji ya activated carbon kiujumla ni tani 1,500 lakini sekta ya madini pekee inahitaji wastani wa tani 200 kwa mwaka, hivyo tukipata mtambo wa kuzalisha tani moja kwa siku, tutakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 300 kwa mwaka,” amesisitiza Mario.


Related Post