Tanapa: Tunaendelea kudhibiti moto uliozuka Mlima Kilimanjaro

October 22, 2022 2:24 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Moto huo uliwaka ndani ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ukitokea eneo la Karanga kuelekea Baranco.
  • Askari zaidi 300 wapelekwa kuzima moto huo.
  • Chanzo bado hakijajulikana. 

Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limesema jitihada za kuzima na kudhibiti moto uliozuka jana Mlima Kilimanjaro zinaendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali likiwemo Jeshi la Zimamoto.

 Afisa Uhifadhi Mwandamizi – Mawasiliano wa Tanapa, Catherine Mbena katika taarifa yake iliyotolewa leo mchana Oktoba 22, 2022 amesema moto uliwaka jana usiku ndani ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ukitokea eneo la Karanga kuelekea Baranco. 

“Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na jitihada za kuzima zinaendelea,” amesema Mbena. 

Amesema askari wa Tanapa wakishirikiana na Jeshi la Zimamoto, polisi, mgambo, Chuo cha Wanyamapori-Mweka na wafanyakazi wa kampuni ya Zara Tours wako eneo la tukio kuudhibiti moto huo.

Hii ni mara ya pili kwa sehemu ya mlima huo kuwaka moto baada ya moto kama huo kuzuka Oktoba 2020 katika ukanda wa nyasi na vichaka na kuteketeza vibanda 15 vya kulala wageni na mifumo ya umeme wa jua na miundombinu ya maji taka.


Soma zaidi:


Gazeti la Mwananchi limemnukuu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kuwa mpaka sasa moto huo haujasababisha madhara kwa shughuli za utalii na wanaendelea kuudhibiti.

Babu amesema askari zaidi ya 300 wamepelekwa katika eneo la Karanga lililopo mita 3,963 kutoka usawa wa bahari.

“Tunachokifanya sasa tunazuia moto usiingie kwenye msitu mkubwa na tayari taratibu zote zinaendelea kuudhibiti moto huu,” amesema Babu wakati akiongea na gazeti la Mwananchi. 

Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kujua ni kitu gani kinachosababisha moto huo kutokea katika mlima huo.

Mlima huo wenye urefu wa mita 5,895 (futi 19,340) ni sehemu ya hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro. Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilometa za mraba 755 na iko umbali wa kilometa 45 kutoka Moshi mjini. 

Mlima huo unaopatikana katika mkoa wa Kilimanjaro ni moja kati ya milima ambayo kilele chake hufikiwa kwa urahisi na hivyo kuwa kivutio kikubwa kwa wapanda milima kutoka kila pande za dunia. 

Mamlaka zinaeleza kuwa wastani wa watu 50,000 hupanda mlima huo kila mwaka.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV