Matukio yaliyotikisa Tanzania mwaka 2023
- Ni pamoja na maporomoko ya matope Hanang na mkataba wa Bandari ya Dar es Salaam.
- Yanaufanya mwaka 2023 kukumbukwa kwa namna tofauti.
Dar es Salaam.Tupo ukingoni kabisa mwa mwaka 2023, mwaka ambao umegubikwa na matukio mbalimbali ya kuumiza na kufurahisha na kuacha kumbukumbu zisizofutika kwa Watanzania.
Nukta Habari imefanya upembuzi na kuainisha matukio yaliyotikisa zaidi nchini Tanzania mwaka 2023 kwa kuzingatia athari, na mapokeo katika jamii, yapo ambayo yametokea kwa mara ya kwanza huku mengine yakijirudia.
1.Mafuriko ya matope Hanang
Usiku wa kuamkia Disemba 3, 2023 ulikuwa wa kutisha kwa wakazi wa Hanang, mara baada ya mawe makubwa, magogo pamoja na matope kufurika katika makazi ya watu wilayani Hanang, mkoani Manyara na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na upotevu wa mali.
Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Mohbare Matinyi, mpaka Disemba 11, 2023 jumla ya watu 89 walipoteza maisha huku 139 wakijeruhiwa kutokana na tukio hilo.
Tukio hilo lilimfanya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufupisha ziara yake ya kikazi ambapo alikuwa anahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) uliokuwa unafanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E).
Disemba 7, 2023 Rais Samia aliwatembela na kuwapa pole wakazi wa maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo ya tope, mawe na magogo yaliyotokana na kumeguka kwa sehemu ya mlima Hanang kutokana na mvua kubwa za El Nino zilizonyesha mkoani humo.
2. Vifo vya Watanzania wawili Israel
Oktoba 7, 2023 ulimwengu ulishtushwa na taarifa za vikosi vya wanamgambo wa Hamas kuivamia Israel, wakifanya mashambulizi kwa njia ya anga na ardhini.
Licha ya kwamba pande hizo mbili zimekuwa katika mapigano ya mara kwa mara, awamu hii imeleta machungu nchini mara baada ya kusababisha vifo kwa vijana wa Kitanzania waliokuwa Israel kwa ajili ya mafunzo ya vitendo katika masuala ya kilimo.
Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilibainisha kuwa vijana hao Joshua Mollel pamoja na Clemence Mtenga walipoteza mawasiliano na ubalozi wa Tanzania tangu Oktoba 7, 2023 Hamas walipovamia na kuteka mamia ya raia.
Hata hivyo, ni Mtenga ndiye aliyethibitika kupoteza maisha awali, ambapo mwili wake ulirejeshwa nchini Novemba 27, 2023 na mazishi kufanyika siku iliyofuata Rombo, mkoani Kilimanjaro.
Wakati juhudi za kumtafuta Mollel zikiendelea, Disemba 14, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba, alibainisha kuwa wamepokea taarifa ya kifo cha Joshua Mollel na mwili wake bado unashikiliwa na wapiganaji wa Hamas.
Vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas wanaopigania ukanda wa Gaza, ni miongoni mwa vita mbaya ambayo huibuka na kufifia ambapo mpaka sasa vimeshapiganwa vita saba baina yao huku zaidi ya watu 30,000 wakitajwa kupoteza maisha.
Soma zaidi : Rais Samia kurejea nchini kufuatia zaidi ya vifo 50, Katesh
3. Kutoonekana kwa Makamu wa Rais kwa siku 40
Watanzania hawakumtia machoni Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango kwa takriban muda wa siku arobaini ikidaiwa alikuwa nje ya nchi kwa kazi maalumu.
Kutoonekana kwake kuliibua taharuki, hususan katika mitandao ya kijamii ambapo watu mbalimbali wakiwemo wanaharakati na wanasiasa walihoji na kuitaka Serikali kutoa majibu ya alipo kiongozi huyo wa pili kwa madaraka nchini.
Pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kueleza mbele ya umma kuwa kiongozi huyo yupo katika majukumu bado baadhi ya watu hawakumuamini, wakihusianisha na kauli kama hiyo aliyoitoa siku chache kabla ya kutangazwa kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Hata hivyo, uvumi na maneno ya chini chini kuhusu alipo Dk. Mpango yalizimwa Disemba 10, 2023 kiongozi huyo aliposhiriki misa ya asubuhi katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, lililopo Kiwanja cha Ndege mjini Dodoma.
Pamoja na kubainisha kuwa alikuwa nje ya nchi kwa kazi maalumu, Makamu wa Rais aliwataka Watanzania kutumia vema mitandao ya kijamii kwa kutoeneza habari potofu kwa kuwa zinasababisha taharuki kwa jamii.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Mpango alionekana kwa mara ya mwisho Oktoba 31, 2023 alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa dharura wa wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao.
4. Kujiuzulu kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Ilianza kama fununu au maneno ya chini chini, lakini ikaja kuthibitika Novemba 29, 2023 mara baada ya Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM Paul Makonda kuutangazia umma kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ameridhia ombi la kujiuzulu kwa Daniel Chongolo kama Katibu Mkuu wa chama hicho.
Chongolo amejiuzulu mara baada ya kuhudumu kwenye wadhifa huo kwa muda wa siku 942 kwa kuwa alichaguliwa na Halimashauri Kuu (NEC) ya CCM Aprili 30, 2021 akirithi mikoba ya mtangulizi wake Dk Bashiru Ally ambaye hivi sasa ni mbunge wa kuteuliwa.

Barua ya kujiuzulu inayodaiwa kuandikwa na aliyekuwa Katibu wa CCM Daniel Chongolo iliyoenea kwenye mitandao ya kijamii. Pichal Abroad TV
Vuguvugu la kung’atuka kwa Chongolo katika nafasi hiyo, liliibuka kupitia barua inayodaiwa kuwa ameiandika Novemba 27 mwaka huu, kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii.
Barua hiyo inaeleza sababu za kung’atuka katika nafasi hiyo kuwa ni “kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii,” huku msingi mkuu wa uamuzi huo kwa mujibu wa barua hiyo ni “kuwajibika kama kiongozi kwa masilahi ya chama” wakati wote anapotuhumiwa au kuhusishwa na jambo lolote.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa mtu mwenye wadhifa mkubwa kutoka CCM kujiuzulu, Januari 6, 2022 Job Ndugai aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Kongwa kwa tiketi ya CCM alijiuzulu nafasi hiyo ambayo sasa inakaliwa na Tulia Ackson Mwansasu.
5. Mkataba wa ushirikiano wa kuendesha bandari
Juni 10, 2023 Bunge la Tanzania liliridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai wa ushirikiano katika uendeshaji na uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini Tanzania.
Hatua hiyo iliibua hisia mchanyato miongoni mwa Watanzania, baadhi wakiunga mkono na baadhi wakipinga, wakitaka ama yafanyike marekebisho kwanza katika baadhi ya vipengele vya mkataba huo na wengine wakitaka ufutwe kabisa.
Soma zaidi : DP World kuendesha bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 30
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanalitaja jambo hilo kuwa miongoni mwa mijadala iliyochukua muda mrefu zaidi nchini Tanzania ukihusisha makundi mbalimbali nyeti ikiwemo taasisi za dini, na viongozi wa kisiasa.
Licha ya makundi mbalimbali kutokuunga mkono ushirikiano huo wakiwemo Baraza la Maaskofu Kanisa Katoliki (TEC) Oktoba 22, 2023 Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World zilitia saini mikataba mitatu ya uwekezaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Yapo matukio mengine mengi yaliyowafanya watu wapigwe bumbuwazi, ikiwemo uteuzi wa Paul Makonda kuwa Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, mgao wa umeme pamoja na tuhuma za unyanyasaji zilizokuwa zinamkabili Mbunge wa Babati Mjini Pauline Gekul yanaufanya mwaka 2023 kuwa wa kukumbukwa kwa namna tofauti.
Latest