Athari zilizotokea mlima Kilimanjaro kuwaka moto
- Moto huo ulizuka Oktoba 21 usiku eneo la Karanga kuelekea Baranco.
- Wateketeza kilomita za mraba 33 za uoto wa asili na hofu kwa wananchi.
- Jitihada za kuuzima zinaendelea.
Dar es Salaam. Serikali imesema moto uliozuka Mlima Kilimanjaro umesababisha hasara mbalimbali ikiwemo kuharibu ukanda wa juu wa mandhari wa hifadhi ya mlima huo, licha ya kuwa zoezi la kuuzima zinaendelea.
Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, moto huo uliwaka usiku wa Oktoba 21, 2022 ndani ya Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ukitokea eneo la Karanga kuelekea Baranco.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Novemba 3, 2022 Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu amesema tukio hilo limesababisha hofu na hasara mbalimbali.
“Tukio hili limesababisha hasara, hofu na kuteketea kwa kilomita za mraba 33 na uoto wa asili, uharibifu wa ukanda wa juu wa mandhari wa hifadhi na kuteketeza viumbe mbalimbali,” amesema Majaliwa.
Hata hivyo, kutokana na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali, amesema wamewezesha kuokoa maeneo muhimu ya utalii kwa kupanda mlima ambayo yamebaki salama na hivyo shughuli za utalii kuendelea kama kawaida.
Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuchunguza chanjo cha moto huo ili kuchukua hatua stahiki huku zoezi la uzimaji linaendelea na moto umedhibitiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo korofi.
Soma zaidi:
Kinachochelewesha kuudhibiti moto
Majaliwa aliyekuwa akitoa tamko la Serikali kuhusu moto huo amesema zoezi la uzimaji linaendelea vizuri kwa mafanikio makubwa pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa ikiwemo upepo mkali unaobadilisha mwelekeo.
Changamoto nyingine ni uwepo wa miiinuko mikali na makongoro makubwa, mlundikano wa mboji ambao huifadhi moto muda mrefu na uoto wa asili wa mimea ya rika ambayo inashika moto kwa urahisi na hivyo kusababisha moto kusambaa kwa kasi.
Moto huo umeendele kudhibitiwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo askari wa Tanapa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (TPDF ambalo limetoa helikopta mbili na askari 878 kuongeza nguvu katika zoezi la uzimaji moto.
Ni zaidi ya moto
“Wakati zoezi la uzimaji moto katika bonde la Karanga linaendelea, matukio mengine ya moto yaliyobainika kwenye Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ni kwenye msitu wa asili katika eneo la Ubetu Samanga wilayani Rombo na eneo la Mandara wilayani Marangu,” amesema Waziri Mkuu na kueleza kuwa moto huo ulidhibitiwa na kuzimwa na vikosi.
Tangazo:

Maagizo mazito
Ili kuhakikisha matukio ya moto kwenye hifadhi za taifa yanadhibitiwa au hayatokei, Serikali imeagiza kuundwa kwa kitengo ndani ya Tanapa na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) cha kukabiliana na majanga au maafa yanayotokea ndani ya hifadhi.
“Kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa hususan katika tahadhari, utambuzi na uzimaji moto. Kuimarisha shughuli za doria na uokoaji kwa kushirikisha jamii na wadau,” amehitimisha Majaliwa kauli ya Serikali kuhusu moto huo.
Latest