CAG afichua intaneti inavyokwamisha ukuaji sekta ya utalii Tanzania

April 29, 2023 10:19 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema baadhi ya hifadhi hazina huduma hiyo.
  • Hali hiyo imekuwa ikileta usumbufu kwa watalii hasa wakati wa usajili.
  • TTCL yalaumiwa kwa huduma zisizoridhisha za intaneti hifadhini.

Dar es Salaam. Licha ya sekta ya utalii kuwa moja ya chanzo kikuu cha mapato nchini, bado huduma zisizoridhisha katika hifadhi za Taifa unakwamisha sekta hiyo kutoa mchango wake kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebaini utoaji mbovu wa huduma za intaneti unaofanywa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika baadhi ya  hifadhi za Taifa, jambo linalotishia maendeleo ya sekta hiyo hiyo nchini.

Mbali na huduma za intaneti zisizoridhisha, shirika hilo pia linalalamikiwa kushindwa kutoa huduma shindani za mawasiliano ya simu za mkononi nchini.  jambo ambalo Rais Samia Suluhu Hassan wakati anapokea ripoti ya CAG Machi 29, 2023 alishauri TTCL kujikita katika kusimamia mkongo wa Taifa ili kupunguza hasara inalopata kila mwaka. 

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa mashirika ya umma katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, TTCL ilishindwa kutoa huduma bora za intaneti katika baadhi ya hifadhi za Taifa na kusababisha shughuli za kusajili watalii kidijitali kukwama.

Sambamba na hilo matengenezo ya mtandao wa intaneti yaliyotolewa katika hifadhi hizo yalichukua muda mrefu kati ya saa mbili  hadi siku nane na kusababisha kero kwa watoa huduma na watalii wanaotembelea hifadhi hizo. 

Baadhi ya hifadhi zilizopata changamoto ya kukosa huduma ya intaneti kwa muda ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Tarangire iliyokosa intaneti na wakati mwingine kusubiri huduma za matengenezo kwa saa 15.

“Katika hifadhi ya Tarangire kukatika kwa intaneti kulichukua saa mbili hadi saa 15 bila marekebisho na hivyo kuleta usumbufu katika uendeshaji wa shughuli za hifadhi,” amesema CAG katika ripoti hiyo. 

Huenda changamoto hiyo ya upatikanaji wa huduma za uhakika za intaneti katika hifadhi za Taifa kukasababishia usumbufu kwa watalii hivyo kuikosesha nchi mapato kwa ajili ya maendeleo.


Zinazohusiana


Katika kutatua changamoto hiyo ya intaneti Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ililazimika kuweka mtandao mbadala ili kuwezesha upatikanaji wa huduma hususan katika malango ya hifadhi ambapo usajili hufanyika na kusababisha shirika hilo kuingia gharama zaidi.

Ripoti hiyo ya CAG imekuja wakati Serikali ikifanya jitihada mbalimbali kuboresha upatikanaji wa huduma bora za intaneti katika vituo vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro.

Desemba 13, 2022, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye alizindua huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa watalii wanaofika katika hifadhi hiyo. 

CAG atoa mapendekezo 

CAG ametoa mapendekezo kwa TANAPA kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti katika hifadhi mbalimbali nchini hususan katika mageti ya hifadhi yenye shughuli nyingi ikiwemo usajili.

“Ninapendekeza kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ihakikishe mageti na hifadhi zote yana mtandao wa intaneti wa uhakika ili kurahisisha shughuli za hifadhi za kuhudumia watalii kwa ufanisi,” amesema CAG.

Sambamba na hilo CAG amependekeza ukukusanya taarifa zote zinazoonyesha kukatika kwa huduma ya intaneti kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 na kuchukua hatua stahiki kwa mtoa huduma.

Enable Notifications OK No thanks