Wanne kati ya 10 hawajaandikishwa darasa la kwanza, awali jiji la Mwanza
- Halmashauri hiyo ilipanga kuandikisha wanafunzi 20,750 lakini walioandikishwa ni 12,122.
- Baadhi ya wazazi jijini Mwanza wamesema uwepo wa shule nyingi za binafsi pia umechangia Serikali kutofikia malengo ya uandikishaji.
Mwanza. Wakati wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakianza muhura mpya wa masomo wiki hii, Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeandikisha asilimia 58.4 ya wanafunzi wa darasa la kwanza na awali kwa mwaka 2023.
Awali jiji hilo lilijiwekea lengo kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza na awali 20,750 lakini hadi zoezi linafungwa ni wanafunzi 12,122 ndiyo walioandikishwa.
Hiyo ni sawa kusema wanafunzi 6 kati ya 10 ndiyo wameandikishwa kuanza masomo mwaka huu.
Kwa darasa la kwanza, jiji hilo lilipanga kuandikisha wanafunzi 13,376 wakiwemo wavulana 6,417 lakini mpaka zoezi linafungwa walikuwa wameandikisha wanafunzi 8,345 sawa na asilimia 62.3.
Madarasa ya awali, halmashauri ilipanga kuandikisha watoto 7,374 wakiwemo wasichana 3,818 lakini hadi sasa ni wanafunzi 3,777 sawa na asilimia 37.7 ndiyo wameandikishwa.
Afisa Elimu Msingi Jiji la Mwanza, Mussa Lwambe amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapitia elimu ya awali kabla hawajajiunga darasa la kwanza.
“Kuna siku zinakuja ambapo Serikali haitaruhusu kuandikisha mtoto ambaye hajapitia elimu ya awali, hivyo ni vyema kila mzazi anatakiwa amwandikishe mtoto wake elimu ya awali,” amesema Lwambe
Kuhusu suala la miundombinu, Afisa elimu huyo amekiri kuwa halmashauri ya jiji la Mwanza na upungufu wa vyumba vya madarasa 1,766 katika shule za msingi, jambo linaloweza kuchangia baadhi watoto kurundikana madarasani na hivyo kuathiri ufundishaji.
“Pamoja na changamoto hizo, Halmashauri inachukua hatua mbalimbali kukabiliana nazo mfano, mpaka sasa imefanikiwa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa 26 ambayo yapo kwenye hatua za ukamilishaji ambapo yamefikia asilimia 95 wakati huo huo Serikali Kuu imetoa fedha za ujenzi wa vyumba 9 ambavyo pia vimefikia asilimia 90,” amesema Lwambe.
Bila kutaja idadi ya madawati yanayohitajika, Lwambe amesema isiwe kikwazo kwa wazazi kushindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa kuwa kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na awali wanaweza kusoma hata kama wakiwa wamekaa chini.
Baadhi ya wazazi jijini Mwanza wamesema uwepo wa shule nyingi za binafsi pia umechangia Serikali kutofikia malengo ya uandikishaji.
“Huenda wazazi wengi wamepeleka watoto wao shule za binafsi ndiyo maana uandikishwaji ni hafifu lakini pia ni vema Serikali ikaendele kuboresha miundombinu ili wazazi wawe na ari ya kupeleka watoto wao huko,” amesema Petro Paul, mkazi wa Mkuyuni jijini hapa.
Tangazo

Latest