Supu ya pweza, vumbi la kongo vyamuibua Rais Samia

September 30, 2022 11:05 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ataka tafiti zifanyike zaidi kuhusu tatizo la lishe nchini.
  • Asema nchi isipokuwa makini itazalisha Taifa goi goi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wataalamu wa masuala ya lishe kufanya utafiti na kuja na majibu ya uhakika kuhusu mzizi wa tatizo la lishe lililopo nchini.

Amesema karibu makundi yote kwenye jamii wakiwemo wajawazito, watoto, vijana na wazee wanakabiliwa na tatizo la lishe, jambo linaloathiri afya ya akili, mwili na ukuaji wa watoto.

Rais Samia aliyekuwa akihutubia katika halfa ya utiaji saini wa mikataba ya usimamizi wa shughuli za lishe jijini Dodoma leo Septemba 29, 2022 amesema lishe bora ni muhimu ili kuwa na jamii yenye afya.

“Hebu tufanyeni utafiti kwanini tunakuwa na lishe mbovu, kwanini tunakuwa na hizo gaps (pengo) za kuwa na watoto ambao wako vizuri kiafya je ni masuala yalioingia ya mitindo?,” amehoji Rais Samia.

Akiwa kwenye hafla hiyo Rais Samia ameizungumzia changamoto inayowakabili vijana ya afya ya uzazi, jambo linalosababisha kutafuta njia mbadala ikiwemo kutumia supu ya pweza na dawa za kuongeza nguvu za kiume ikiwemo ‘mkongo’ ambao umepigwa marufuku nchini. 

“Wakifika wakati wa kuwajibika kuja kuongeza Society (jamii) wanahangaika…tuna tatizo na mnalijua mnalificha watafiti fanyeni utafiti,” ameongeza Rais Samia.


Zinazohusiana


Lishe bora ni muhimu kwa afya ya makundi yote kuanzia watoto, vijana na  wazee, huku kundi la vijana likitiliwa mkazo kwani kundi hilo ndilo linategemewa kama nguvu kazi ya Taifa katika ukuaji wa uchumi. 

Kuhusu wajawazito, Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) imesema ukosefu wa lishe bora wakati wa ujauzito huweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile  mama kutoongezeka uzito, upungufu wa damu wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ambao huweza kusababisha hata kifo, uwezekano wa mimba kuharibika na mtoto kufia tumboni.

Changamoto nyingine ambazo anaweza kuzipata mama mjamzito kutokana na ukosefu wa lishe ni pamoja na  kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu, kuzaa mtoto njiti au kuzaa mtoto mfu na kuongezeka kwa magonjwa kwa sababu ya mfumo wa kinga kuwa dhaifu.

Kama changamoto hizi za lishe zisiposhughulikiwa kwa wakati zinaweza kuleta madhara si tu kwa mtu mmoja mmoja lakini kwa kizazi kinachokuja baadae.

“Nilishasema hapa kwamba tukiacha hali ikienda hivi tunaenda kuwa na Taifa  goi goi, Taifa lenye watu lakini siyo rasilimali watu, ni watu ambao ni mzigo kwa Taifa sio watu watakaoenda kuzalisha kwa ajili ya Taifa,” amesema Rias.

Mbali na ukosefu wa lishe bora, Rais Samia amesema kuna tatizo la lishe inayopitiliza linalosababisha vitambi na uzito uliopitiliza, hivyo kuna haja wataalamu kwenda kufanyia kazi na kupata suluhisho ya changamoto hiyo.

“Kwa upande mwingine kuna matatizo yanayotokana na lishe iliyopitiliza kuna vitambi (obesity)…tuna tatizo hilo pia wataalamu mnapaswa kulitekeleza,” amesema Rais Samia.


Tangazo


Halmashauri zilizofanya ubadhilifu wa fedha za lishe zichukuliwe hatua

Rais Samia amesema fedha za bajeti  zinazotolewa kwa ajili ya lishe zitumike ipasavyo ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya lishe.

“Mnaweza kusema Fedha za lishe zimeshatoka lakini zimetumika wapi, suala ni zimetumika wapi, ziende zikatumike kwenye makusudi yaliyodhamiriwa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amemtaka  Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Innocent Bashungwa kuandaa ripoti ya Halmashauri zilizofanya ubadhilifu wa  fedha za lishe ili wachukuliwe hatua.

“Kwa wale wote waliozitumia vibaya fedha za lishe ambao fedha imeingizwa kwenye lishe ikaingia upande mwingine, hatua zinazopaswa zichukuliwe kwa sababu huu ni ukosefu wa nidhamu,” amesema Rais.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW