Rais Samia aitaka jamii kutunza wazee, majambazi ‘kutojaribu kina cha maji’
- Aitaka jamii iwalee watoto kuwa na maadili kwa wakubwa zao.
- Amewasihi makonda kuhakikisha wazee wanapata “siti” wanapoingia kwenye gari.
- Kuhusu kujenga nyumba za kulelea wazee, amesema atalifanya japo hafurahii.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii ya Watanzania kurudi katika misingi ya malezi ili kuwa chachu ya maendeleo ya nchi na kujenga Tanzania ambayo ni bora kwa kila mtu kuishi ikiwamo kuwaheshimu na kuwatunza wazee.
Mama Samia ambaye alikuwa akizungumza na Wazee jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa Mei 7, 2021) ameitaka jamii kuweka mazingira bora kwa wazee ambao wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Kauli ya Rais huyo imekuja baada Mwenyekiti wa Baraza la Wazee mkoa wa Dar es Salaam, Salum Matimbwa kumueleza masuala wanaoyoiomba Serikali iwasaidie ikiwemo huduma bora za matibabu na kupatiwa nafasi maalumu za wazee katika vyombo vya usafiri wa umma.
Wakati akijibu maombi hayo, Rais Samia amesema hadi kufikia hatua ya wazee kuomba nafasi za kukaa katika vyombo vya usafiri ni ishara kuwa kuna shida katika malezi na maadili katika jamii ya Watanzania.
“Kama mtoto ameleleka vizuri ameingia kwenye basi na anakuta mzee ameingia amesimama yeye anathubutu kukaa kwenye kiti, tuna dosari. Tuna dosari wazee wangu na dosari hii sijui niseme imeanzia wapi,” amesema Rais Samia ambaye yeye amesema leo hii anaweza kumpisha mzee akae pale atakapo mkuta amesimama katika usafiri.
Soma zaidi:
- Rais Samia aeleza sababu barakoa kutawala mkutano wa wazee Dar
- Nane mbaroni kwa wizi wa vifaa vya ujenzi daraja la Magufuli
- Bajeti wizara ya maji yashuka Tanzania, fedha za miradi ya maendeleo juu
Amewasihi Watanzania kurudi kwenye malezi mazuri kwani viti vya kwenye vyombo vya usafiri ni vichache sana na viti hivyo ni vya wazee, hivyo vijana wenye nguvu wasimame kuwapisha wazee.
“Niongee na wahudumu wanaotoa huduma kwenye vyombo vya usafiri jina maarufu makonda. Wale ndio wanatakiwa kuhakikisha mzee ameingia amepata kiti amekaa na kijana kama yupo amwambie kijana simama umpishe mzee,” amesema Samia akiongeza kuwa endapo utaratibu huo utafanyika na kuzoeleka, vijana watazoea kiasi cha kutokusubiri kukumbushwa.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa nchi amegusia uwepo wa tabia za wizi, uporaji na ujambazi katika jiji la Dar es Salaam akieleza kuwa matukio hayo ni matokeo ya ukosefu wa maadili kwa kuwa licha ya uchumi kuwa mgumu, haimpi mtu sababu ya kuwa jambazi na kuibia wenzake.
“Nimesoma mtandaoni kuwa Dar es Salaam sasa wanajaribu kina cha maji viujambazi jambazi vimeanza kuja juu, naomba nitoe meseji wasijaribu kina cha maji,” amesema Rais Samia.
Katika suala la makazi ya wazee, Rais Samia amesema atafanya jitihada ya ujenzi na ukarabati wa makazi yaliyopo na kuwataka Watanzania kuchukua nafasi katika malezi ya wazee hao ambao anaamini wote wana watoto wao na wale ambao hawajabahatika kuwa na watoto, wana ndugu.
Amesema uwepo wa nyumba za kulelea wazee ni tabia za Kimagharibi na kwa Afrika hasa Tanzania, ni jukumu la watoto na ndugu kuwalea wazee.
Mazungumzo ya wazee na Rais Samia yamekuja siku mbili tangu amalize ziara ya siku mbili nchini Kenya ambayo alikutana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kuzungumzia masuala ya kimaendeleo yakiwemo ujenzi wa miungombinu na fursa za kibiashara baina ya nchi hizo.
Latest