Rais Samia: Lishe bora kwa watoto ni ustawi mzuri wa mwili na akili

August 20, 2024 8:27 pm · Hemed Suleman
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema lishe bora itawafanya watoto wafanye vizuri darasani.
  • Wazazi watakiwa kuwajibika kutoa michango itakayosaidia matunzo ya shule.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema lishe bora kwa watoto ndani ya siku 1,000 za mwanzoni husaidia ukuaji mzuri wa mwili, kiakili na kuwawezesha kufanya vizuri darasani.

Rais Samia amesema hayo leo Agosti 20,2024 wakati akifungua Skuli ya Maandalizi Tasani iliyopo Makunduchi, visiwani Zanzibar na kusisitiza umuhimu wa lishe hiyo kwa watoto wenye umri mdogo.

“Siku elfu moja baada ya mtoto kuzaliwa ni miaka, karibu miaka mitatu na hapa ndio kituo cha watoto hao, kuanzia miwili, miwili na nusu mpaka mitatu na kuendelea kama sera inavyotuelekeza, sasa kwanini siku hizi ni muhimu? Ni muhimu kwanza mtoto kupata chakula bora kitakachojenga na afya, afya ya mwili na afya ya akili…

….Sasa watoto watakaoletwa hapa wenye umri wa miaka miwili na nusu, mitatu na kuendelea, hapa kwa jengo hili lilivyo watatunzwa wapate makuzi ya kimwili, kuitengeneza akili ijitayarishe na masomo ya baadae lakini pia afya ya miili yao kwasababu bwalo la chakula lipo hapo,” amesema Rais Samia.

Lishe bora kwa watoto ni miongoni mwa masuala ya muhimu yanayopaswa kutupiwa jicho ili kukabiliana na tatizo la udumavu na utapiamlo linaloikumba Jamii nyingi nchini hususani mikoa ya nyanda za juu kusini.

Ripoti ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto (THDS-MIS) ya mwaka 2022 inaitaja mikoa ya Iringa kuwa udumavu kwa asilimia 56.9, Njombe asilimia 50.4 na mkoa wa Rukwa kwa 49.8 huku ukipungua kwa asilimia nne kitaifa.

Hiyo inamaanisha zaidi ya nusu ya watoto katika mikoa hiyo walikosa lishe bora wakiwa kwenye miezi sita hadi miezi 24 ya mwanzoni kwa Mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

WHO inasema miongoni mwa madhara yatokanayo na udumavu ni pamoja na kifo, kutokufanya vizuri darasani na kupunguza ufanisi wa kazi watakapokuwa watu wazima 

Wazazi wajibikeni

Licha ya Wizara ya Elimu kuwa tayari kutoa chakula kwa ajili ya wanafunzi hao kwa ruzuku ya Serikali, Rais Samia amewataka wazazi kuwajibika kwenye matunzo ya shule kwa kutoa michango ili shule ibakie katika ubora wake.

“Haya naambiwa kuna ruzuku ya uji kwa hiyo hilo limenusurika kwa wazazi lakini bado kuna matunzo ya shule lazima wazazi tuchangie ili shule hii ibakie hivi hivi inavyoonekana,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongezea kuwa kupitia Skuli ya Maandalizi ya Tasani ambayo ni mojawapo ya mradi wa maendeleo uliotekelezwa kupitia Tamasha la Kizimkazi linalofanyika kila mwaka Zanzibar, watoto wataandaliwa vyema kwa kupata maadili mazuri yatakayo wawezesha katika masomo yao ya baadae.

Rais Samia ameeleza utekelezaji wa mradi huo umetokana na kauli mbiu ya mwaka jana ambayo ni ‘Tuwalinde kimaadili watoto wetu kwa maslahi ya Taifa’, kupitia kauli mbiu hiyo juhudi zimefanyika mpaka mradi huo wa shule kutimia.

Enable Notifications OK No thanks