Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi-2

July 19, 2020 5:30 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Pamoja na kupata elimu bila malipo, Mabindo hawezi tena kwenda shule kwa sasa kwa sababu hana fedha za kumudu familia.
  • Uzee wake haujapunguza nidhamu kwa walimu, wanafunzi wenzie.

Babu, rafiki wa kila mtu

Mwanafunzi ambaye wengi walimhofia taratibu aligeuka kuwa rafiki wa kila mtu. Walimu wanampenda na wanafunzi wenzie wanaomuita babu nao wamekuwa karibu naye na hivi sasa wamemkumbuka kwa kutokumuona shuleni kwa wiki mbili sasa. 

“Amekuwa rafiki wa kila mmoja anapenda kucheza na wanafunzi wenzake, anapenda ushirikiano na hata anapokuwa na jambo anakuwa muwazi,” anaelezea mwalimu huyo.

Baada ya maelezo hayo, walimu walimchukulia kama mwanafunzi wao na alitii sheria zote na kushiriki shughuli zote za shule kama wanafunzi wengine jambo lililomjengea urafiki wa karibu na wanafunzi wenzake.


Maendeleo yake toka aanze shule yapoje?

Anasema bidii na juhudi za kujifunza zilimfanya apate matokeo ya wastani shuleni. 

Darasa la kwanza alifanikiwa kushika nafasi ya 35 kati ya wanafunzi 56 huku darasa la pili akapanda kidogo hadi kuwa wa 18. 

Alipofika darasa la nne mwaka jana, Mabindo alifanikiwa kupenya baada ya kupata wastani wa kuingia darasa la tano katika mtihani wa Taifa mwaka 2019.

“Niliendelea kusogea taratibu huenda kutokana na elimu ya ukubwani huku nikikabiliwa na changamoto za kifamilia,”anasema Mabindo.

Abdallah Mabindo akiwa na wanafunzi wenzake shuleni hapo. Mwanafunzi huyo mwenye miaka 53 aliamua kwenda shule ili kujifunza kusoma na kuandika na kuondoa ujinga. Picha| Mariam John. 

Kwanini Mabindo ametoweka shuleni?

Pamoja na mafaniko ya kujua kusoma na kuandika na hatimaye kupata alama ‘C’ katika mtihani wa Taifa wa darasa la nne, safari yake ya elimu imeanza kupigwa na mawimbi. 

Kuna hatari kubwa mzee huyo asifikie ndoto zake iwapo changamoto zinazomkabili hazitatuliwa mapema. 

“Likizo ya corona huenda imebadili kabisa mfumo wa maisha hasa katika kipato na darasani hajaonekana ikiwa ni zaidi ya majuma mawili baada ya shule kufunguliwa Juni 29 mwaka huu. 

“Tumemkumbuka mwanafunzi mwenzetu…tunajiuliza ameenda wapi, labda anaumwa lakini hamna mbona hatumuoni akihudhuria masomo?” anahoji Amina Abdallah, binti anayesoma pamoja na mzee huyo huku akionyesha nia ya kufahamu alipo Mabindo.  

Amina anasema akiwa shuleni Mabindo ambaye wanashirikiana pamoja kujifunza wakati wa mapumziko hupenda kuwasimulia hadithi mbalimbali. 


Zinazohusiana:


Anaposhindwa kwenye masomo yake, mzee huyo hupata wasaa wa kuhojiana na kina Amina ili wamwelekeze vema. 

“Alikuwa mwanafunzi mtiifu, hakuonyesha dharau alikubali kujishusha na hata aliposhindwa kupata ‘marks’ (alama) za juu aliumia na alikuwa tayari kutuulizia,”alisema Lukas Nehemia mwanafunzi wa darasa la tano shuleni hapo anamwelezea Mabinda. 

Kwa mujibu wa Lukas katika mtihani wa majaribio wa somo la Sayansi, Mabindo alipata alama 40 huku wenzake wakipata 80 na kuendelea kitendo hicho kilimuumiza na kuomba msaada aelekezwe pale alipokosea.

“Nilimuona jinsi alivyokuwa anajihisi vibaya, ila nilimsaidia kwa kuwa alikuwa tayari kujifunza,” Lukas ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz).

Dawati analokalia mwanafunzi Mabindo sasa li wazi hata rafiki yake wa karibu aliyekuwa anakaa naye toka wakiwa darasa la kwanza kwa sasa anakaa peke yake.

Uongozi wa shule nao bado unamsubiri iwapo Mabindo atarejea kuendelea na masomo ama la kwa kuwa hawana fununu zozote kumhusu. 

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Waston Gwivaha anasema toka shule zifunguliwe hawajamuona mwanafunzi huyo na hawajapata taarifa zake zozote.“Huenda anakabiliwa na changamoto za kifamilia kwa kuwa yeye ni baba na anatakiwa atimize majukumu ya kifamilia,”anasema Gwivaha. 

Hadi sasa mwalimu huyo anasema wanaendelea kumsubiri na asiporipoti shuleni watatafuta taarifa kujua aliko na anafanya nini.

Jambo hawajui ni kuwa Mabindo kwa sasa anapambana mjini apate mkate wake wa kila siku kabla ya kurudi kuendelea na elimu ya msingi iwapo “mambo yatakaa sawa”. 

Wanaomtafuta Mabindo yuko sokoni kuuza nguo ili apate fedha kwa ajili ya familia yake lakini amesema anatamani kurudi shuleni mapema. Picha| Mariam John. 

Nidhamu “kiwango cha lami”

Gwihava ameiambia Nukta kuwa mwanafunzi huyo toka ajiunge na shule hiyo hajaonyesha tofauti yoyote na kwamba ni mcheshi na mwenye ushirikiano.Anasema amekuwa rafiki wa wanafunzi wenzake na wanafunzi huwa wanamwita “babu”.

“Hakupenda kujitenga na alishirikiana nao katika shughuli zote za shule zikiwemo kufanya usafi wa mazingira na kusafisha choo, michezo…na kazi nyingine zote alifanya bila kushurutishwa,” anasema Mwalimu Gwihava.

Mabindo na harakati za kujitafutia maisha

Katika soko la mitumba la Mlango Mmoja maarufu hapa jijini Mwanza kwa jina la Langolango, Mabindo ametingwa na biashara akitafuta riziki. 

Tofauti na akiwa darasani, hapa Mabindo anasikia zaidi kelele za wafanyabiashara ambao wanawaita wateja angalau wauze chochote. 

Mwanafunzi huyu, tofauti na wenzie wenye wastani wa umri wa miaka 11 wanaotegemea kila kitu nyumbani, yeye anategemewa kwenye familia yake. Ana majukumu ya kutosha ikiwemo kumtunza mkewe. 

“Niko hapa Mlango Mmoja sijaenda shule kwa sababu ya kiuchumi, nimekuja hapa kuona kama nitaweka msingi utakaolea familia kisha baada ya wiki tatu au nne nitarudi kuendelea na shule,”anasema Mabindo.

Isingekuwa ukata, mwanafunzi huyo, anaeleza kuwa angeendelea na masomo vizuri bila kushinda siku hizi za awali tangu shule zifunguliwe lakini kwa sasa anategemewa na familia. 

“Kwa maisha ya sasa unatakiwa uondoke nyumbani umeacha angalau Sh7,000 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani lakini sasa naendaje shuleni wakati msingi wa kuacha hiyo hela sina,” anasema. 

Awali aliwezaje kusoma?

Miaka miwili iliyopita, Mabindo hakuwa na changamoto kubwa sana ya kipato kiasi cha kumzuia kwenda shule kwa kuwa alikuwa ana sehemu ambayo inaweza kumpatia angalau fedha za kumudu mahitahi ya familia. 

Hata hivyo, kifo cha mdhamini wake ambaye hakutaka kumtaja huenda ndiyo sababu kubwa inayomfanya kwa sasa aingie mtaani kutafuta riziki kwa ajili ya familia yake.

Mabindo anasema zamani alikuwa na mfadhili katika moja ya viwanda mkoani hapo aliyekuwa amemwezesha kibarua baada ya kutoka shule. 

Alikuwa akitoka shule anaenda kiwandani kwake kumsaidia kazi na hata kama akifanya kazi saa mbili bado alimpatia Sh20, 000, fedha ambayo inamfanya ahudumie familia. 

Kiwango hicho cha malipo kilikuwa kikubwa, juu ya wastani wa wafanyakazi wa kawaida katika kiwanda hicho. 

Familia, ndugu na jamaa wana mtazamo gani kuhusu Mabindo kurudi shuleni? Serikali imejipangaje kuwasaidia wanafunzi kama Mabindo kupata elimu bora? Usikose sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala haya yatakayokujia kesho Julai 19, 2020. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW