Mfahamu bata Bukini mwenye kilo 14 anayeuzwa Sh2 milioni
- Bata huyo anaitwa kwa kimombo anafahamika kama African Goose.
Dar es Salaam. Umeshawahi kuona bata mwenye kilo 14? Kwa wengi hii inaweza kuwa ndoto au suala la kusadikika lakini hivyo sivyo wanavyoamini mamia ya Watanzania waliotembelea banda la mifugo katika maonyesho ya 50 ya kimataifa ya biashara Dar es salaam (sabasaba).
Mbona bata huyu mkubwa hivi?, ni mzito hadi mkono wangu unashindwa kumshika, analiwa kweli? Nyama yake ni tamu kama bata wengine? Anauzwa Shilingi ngapi?
Waliuliza baadhi ya Watanzania waliofika kujionea bata huyo katika viwanja vya saba saba akitaka kujua zaidi kuhusu ndege huyo.
Bata huyo ambaye tunamzungumzia hapa anaitwa bata bukini ama kwa kimombo African Goose
Kwa hali ya kawaida hata wewe ungevutiwa, kwanza ana rangi nyeupe na kijivu angavu inayomfanya aonekane vyema hata akiwa mbali.
Mwendo wa madaha, urefu na sauti ya kuvutia kama king’ora inayomfanya yeyote anayepita karibu na banda hilo kusimama kidogo.
Uzito mkubwa matunzo ya kawaida
Sebastiani Massawe mfugaji wa bata huyo huyo anasema kuwa wanaeza kufikia uzito wa hadi kilo14 kwa bata dume huku jike akikadiriwa kufikia uzito wa kilo 12.
Bata hao wakinyonyolea na kuandaliwa kwa ajili ya kupika huweza kufikia hadi kilo 9.5 suala linaloweza kuwa kicheko kwa walaji wa aina hiyo ya kitoweo.
Kilo hizo zake akiwa mzima au akiwa ameshaandaliwa kwa ajili ya kupikwa ni mara mbili au zaidi ya zile zinazopatikana kwa bata wa kawaida wa kufungwa nyumbani.
Mbali na nyama tovuti ya livestock concervacy inabainisha kuwa bata hao wanauwezo wa kuishi miaka 10 hadi 20 kama utaweza kuwatunza vyema huku wataga hadi mayai 40 makubwa kwa mwaka.
Massawe anasema licha ya sifa hizo kede kede matunzo yake hayatofautiani na bata wa kawaida
“Utunzaji wake ni kama bata wa kawaida kama una shamba lako unamuachia anajitafutia chakula mwenyewe na anapata chanjo kama bata wa kawaida, japo hawaathiriwi kirahisi na magonjwa kutokana na uwezo wao wa kuishi katika mazingira tofauti wanaweza kuishi majini na nchi kavu..
…Anatumia vyakula vya kawaida tu kama pumba, mahindi kama bata wengine, yeye pia anaogelea ni bata kama bata wengine,” anasema Sebastiani kwa kujiamini.
Tovuti ya Chikago suntime, inabainisha kuwa bata hao hupendelea kula vyakula vya nafaka na Mbegu, mboga za majani, vyakula vya kiwandani lakini hupendelea zaidi kula majani mabichi na mimea laini, ambayo huchangia takriban asilimia 50 ya mlo wote wa siku pamoja na maji mengi.
Ili kumpata bata huyo utalazimika kutoboa mfuko wako hadi Sh2 milioni huku vifaranga vikiuzwa kwa Sh200,000 na mayai Sh30,000
Kufuatia bei hiyo, baadhi ya wakazi na wafanyabiashara wa chakula jijini Dar es Salaam wamesema si rahisi kwa watu wa kipato cha chini kumudu gharama.
“Mimi siwezi kununua bata wa namna hiyo, maana thamani bata na milioni mbili ni vitu viwili tofauti, lakini inawezekana kwa mtu ambae anahela, kuna watu wana ela na hawana cha kufanyia kazi, kununua bata ya milioni mbili haoni kazi ila mimi siwezi kununua” alisema Imani Jafari dereva bodaboda kutoka Kinondoni studio.
Kwa upande wake Catherine Robert mkazi wa Kinondoni yeye anasema kununua bata bukini kwa ajili ya kitoweo ama shughuli yoyote ile ni uharibifu wa bajeti.
“Kununua bata kwa milioni mbili me kwa upande wangu naona kama ni uharibifu wa bajeti, labda kama nikipewa zawadi hata kama ni mchumba wangu amenipa zawadi ya bata wa milioni mbili yaani hatuelewani.” alisema Catherine
Sebastian pia anasema, soko lao ni kubwa na wateja wao wengi hutoka mikoani na wachache wanatoka hapa jijini Dar es salaam, wengi wao wakiwa wanahitaji vifaranga na mayai.
Ni chanzo cha protini
Bukini hufugwa kwa ajili ya nyama, mayai na hata manyoya katika nchi nyingi duniani. Nyama yake huliwa kama kitoweo na inajulikana kuwa na ladha tofauti na ya bata wa kawaida au kuku.
Katika baadhi ya nchi za Ulaya, Amerika Kaskazini na Asia, nyama ya bata bukini ni mlo maarufu hasa wakati wa sikukuu kama Krismasi.
Shirika la chakula duniani (FAO) linaeleza kuwa nyama ya bukini ina kiwango kikubwa cha protini pamoja na madini muhimu kama chuma na zinki.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa nyama nyingine, inashauriwa ipikwe vizuri na kuliwa kwa kiasi kutokana na kuwa na mafuta mengi zaidi kuliko nyama ya kuku.
Tofauti na nyama ya kuku, nyama ya bata bukini ina madini mengi ya chuma ambayo ni muhimu sana katika kuongeza damu mwilini na kuzuia uchovu.
Pia, mayai yao makubwa yana virutubisho vinavyosaidia kuboresha uwezo wa ubongo na kufanya kumbukumbu yako iwe vizuri zaidi.
Mbali na kuwa chanzo cha kitoweo, bata bukini pia ni walinzi wazuri wa mashamba. Wana uwezo mkubwa wa kugundua hatari mapema kupitia macho na masikio yao makali, kisha hutoa sauti kubwa ya tahadhari inayowaonya wengine.