Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 1

March 6, 2021 9:30 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Watoto saba wa mama mmoja wakatwa miguu wakiwemo watoto wadogo.
  • Bado familia hiyo imebaki njiapanda kwa kuwa hawajapata majibu ya ugonjwa huo unaozidi kutishia mustakabali wa maisha yao na uhusiano na ukoo na marafiki

Mwanza. Kwa takribani miongo mitatu mfululizo maisha ya Amina Kalazi (60) mkazi wa kijiji cha Igayaza wilayani Muleba yamekuwa yakitawaliwa na machozi baada ya familia yake kukumbwa na ugonjwa uliofanya sehemu kubwa ya familia yake kukatwa miguu.

Amina, mama wa watoto 14, alizaliwa mzima akiwa na viungo vyote vya  mwili lakini kwa sasa historia ya maisha yake imebadilika baada ya kujikuta yeye na watoto wake saba kupoteza viungo vya miguu yote miwili kutokana na “ugonjwa wanaouita wa ajabu”.

Mbali naya na watoto wake, watu wanne kutoka kwenye ukoo upande wa mama yake Amina nao walishakatwa miguu.

Kukatwa kwa miguu kwa ndugu hao wa familia moja kumeifanya wapate ulemavu wa kudumu kiasi cha kushindwa kufanya shughuli za kujiingizia kipato. Mbali na ulemavu, familia imejikuta kila kipindi ikisaka fedha kwa ajili ya kuwatibu ndugu walioanza kupata ugonjwa huo.


Nini chanzo cha tatizo? 

Pamoja na mateso hayo ya muda mrefu, bado familia hiyo imebaki njiapanda kwa kuwa hawajapata majibu ya ugonjwa huo unaozidi kutishia mustakabali wa maisha yao na uhusiano na ukoo na marafiki. 

“Bado hatujafanikiwa kujua tatizo la ugonjwa huu. Awali daktari anayetufanyia upasuaji alipima na kubaini hakuna dalili zozote za kansa wala kisukari, ” amesema Amina. 

Amina anasema hata yeye hajui chanzo cha tatizo hilo na anaiomba Serikali kusaidia kufanya uchunguzi ili kupata kinga itakayonusuru kizazi kijacho ambacho pia kimeanza kushambuliwa. 

Hata hivyo, madaktari wameiambia Nukta Habari kuwa ugonjwa huo ni Gangrene ambao husababisha uzalishaji duni wa tishu za ngozi na kusababisha eneo lilioathirika kukauka na kuoza. 

Kwa sasa Amina anaishi katika mtaa wa Lumala jijini Mwanza kwa takribani mwezi mmoja pamoja na baadhi ya wanawe baada ya kupata msamaria mwema kumuita kwa ajili ya kutatiwa miguu ya bandia na matibabu.

Akisimulia namna wanavyoanza kuugua,  Amina anasema akiwa darasa la pili  alianza kuugua ugonjwa huo ambao ulisababisha kukatwa vidole vyote vya miguu yake. 

Baadhi ya wanafamilia ambao miguu ya imekatwa kutokana na tatizo ugonjwa wa ajabu ambao hawaufahamu mpaka sasa. Picha| Mariam John. 

Kwa mujibu wa Amina anasema ugonjwa huanza kwa kidole kimoja kuwasha  kama funza tatizo ambalo huambatana na maumivu makali kama mtu anayeungua na moto. 

Baada ya siku chache ugonjwa husambaa kwenye vidole vyote na hubadilika

kwa haraka na kusinyaa. Baadaye ngozi hubadilika rangi na kuwa nyeusi huku nyama za miguu pamoja na mifupa hushikana pamoja na kukauka.

“Tatizo hilo husambaa kwa haraka sana mifupa na nyama hushikana na kukauka kabisa na kuoza…kadiri siku zinavyoenda ugonjwa hupanda kuelekea juu ya magoti,” anasimulia Amina huku akiinama chini. 


Je, tatizo lilianzia wapi? 

Historia inaonyesha si kizazi cha kwanza kwenye familia ya Amina  kilichokatwa miguu, marehemu mama yake pamoja na ndugu wengine nao walikumbwa na kadhia hiyo. 

Kwa mujibu wa Amina alimkuta mama yake akiwa tayari amekatawa vidole vyote 10 vya miguu,  tatizo ambalo pia lilikuwepo kwa ndugu  wengine wa mamaye.

“Nilifikiria huenda tatizo litaishia kwenye kizazi cha mama yangu pekee matokeo yake limefuata hadi kizazi changu inaniuma sana,” anasema Amina huku akiangua kilio. 


Zinazohusiana:


Ugonjwa unavyowashambulia watoto

Kila usiku ukiingia Rahma Mathias binti wa Amina huwa na hofu kwamba huenda asiione kesgo. Hutawaliwa na mamivu makali anayoyapata ikiwa ni miezi 10 tangu akatwe miguu yake kutokana na ugonjwa huo.

Rahma bado anakumbuka namna alivyofanyiwa upasaji huo mara tatu akiwa una ujauzito wa  miezi nane na hata baada ya kujifungua. 

Huku akibubujikwa na machozi Rahma, mama wa watoto wawili, anasema hali hiyo inamuumiza kwa kuwa hajui hatima ya watoto wake. 

“Nilianza kwa kuwashwa kama funza nilipomtumbua baadaye nilishtukia malengelenge  kama nimeungua na moto,  siku chache baadae miguu ilibadilika rangi na kuwa myeusi huku nikipata maumivu makali sana, ” anasema na kuongeza; 

“Tatizo hili lilinitesa na hata waliponipeleka hospitali  ya wilaya daktari alinieleza mishipa haipeleki damu kwenye vidole hivyo inatakiwa kukatwa.”

Licha ya kufanyiwa upasuaji bado anahisi maumivu makali yanayosababisha ashindwe kupata usingizi. Wapo waliomshauri awe anaweka miguu kwenye maji.

“Sikutarajia kama siku moja historia yangu ingebadilika kuwa namna hii, inaniuma sana hasa kwa wakati huu nikiwafikiria wanangu kwakuwa ugonjwa unafuata damu,” anasema Rahma. 

Anasema wakati anafikishwa hospitali daktari alibaini mishipa haipeleki damu kwenye vidole vyote viwili na imekauka kabisa hivyo hakuna namna yoyote zaidi ya kukatwa.

Sehemu miguu ya wanafamilia hao baada ya kukatwa walipopata ugonjwa wa ajabu. Picha| Mariam John.

Ndoto za kutoka nje kwenda kujitafutia zilianza kufifia, akili ya kuanza kuwa tegemezi ilimujia hasa akiwaangalia ndugu zake wanne waliopo nyumbani ambao kula yao ni kutoka kwa wasamalia wema.

Akiwa bado na mamivu makali, miezi miwili baada ya vidole kukatwa madaktari walibaini mishipa haipeleki damu kwenye nyayo hivyo ikalazimika kukatwa kwa mara ya pili. 

“Nitofauti na ndugu zangu ambao walikatwa vidole na sehemu kidogo ya nyayo kwani licha ya daktari kunikata mara mbili, bado nyama ziliendelea kuoza hali iliyomlazimu mama kumtafuta daktari aliyekuwa anawafanyia upasuaji ndugu zangu wengine,” anasema Rahma. 

“Maumivu ninayopata ni makali sana,  siwezi kulala na kufunikwa miguu yote nitajifunika mwisho kwenye magoti,  kuna wakati usiku usingizi sipati, ” anaongeza. 

Kwa sasa, anasimulia kuwa mme wangu ndiye hufua nguo za mtoto,  anapika,  anachota maji,  anawatafutia chakula na kukamilisha shughuli zote za nyumbani na kuwasafisha wanapojisaidia. 

Kabla ya kukabiliwa na ugonjwa huo, Rahma alikuwa akijishughulisha na uzalishaji mali na alikuwa akimsaidia mama yake na nduguze wengine lakini sasa historia yake imebadilika na anasema amekuwa tegemezi kwa kila kitu.

“Siwezi kutembea kazi yangu imebaki kula na kulala,” anasema huku akibubujikwa na machozi. 

Kadhia hii si kwa Rahma pekee. Furaha ya familia nzima ya Amina Kalazi imetoweka wamebaki watu wa kuomba misaada kwa wasamaria wema ili waweze kupata huduma za chakula malazi na mavazi. 

Kukatwa kwa miguu ya Rahma kunakamilisha idadi ya watoto saba wa Amina waliokumbwa na ugonjwa huo ambao mpaka sasa  haujajulikana.

Ni watoto wawili tu wa mama huyo ndio bado wanamiguu yao miwili ingawa nao kuna wakati wanaweweseka wakihofia huenda siku moja wakakumbwa na tatizo hilo ingawa mtoto pekee wa kiume wa mama huyo naye ameanza kuugua mguu kwenye nyonga. 

Usikose sehemu ya pili ya ripoti hii ambayo itamulika kwa undani madhira wanayopata wanafamilia hao na wataalam wa afya wanavyouelezea ugonjwa huo na tiba yake.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

PART 2: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta.

Nukta TV

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

PART 1: Yafahamu magari 10 yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV