Shule 13 mkiani, matokeo ya darasa la saba, 2026
- Necta yaeleza sababu ni kubadilika kwa mfumo wa uulizaji maswali katika mitihani, kutoka majibu ya kuchagua hadi majibu yanayopima uelewa.
Dar es Salaam. Idadi ya shule zilizopata ufaulu wa daraja E katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) imeongezeka kutoka shule nne mwaka 2025 hadi 13 mwaka 2026.
Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa leo Novemba 3, 2026 na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), idadi hiyo ni kubwa zaidi kurekodiwa ndani ya miaka mitatu.
Mwaka 2026, jumla ya shule 20,010 zilifanya mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi ambapo shule 18,584 sawa na asilimia 92.87 zilipata daraja A hadi C kiwango kinachashiria ufaulu mzuri.
Shule 13 sawa na asilimia 0.06 zilipata daraja E, kiwango cha chini katika ufaulu.
Uchambuzi ulifanywa na Nukta Habari, umebaini kuwa idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 225, mara nne zaidi kutoka shule nne zilizorekodiwa mwaka 2025 baada ya kupungua kutoka shule sita mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Necta, shule kupata daraja hilo hakumaanishi kuwa kila mwanafunzi aliyefanya mtihani katika shule husika amepata daraja E.
Baadhi ya wanafunzi wanaweza kuwa wamepata madaraja ya juu kabisa ya ufaulu.
Ufaulu wa shule hupatikana kwa kuzingatia wastani wa matokeo ya watahiniwa wake, hivyo hata kama baadhi ya wanafunzi wamefanya vizuri, matokeo ya jumla yanaweza kuiweka shule katika ufaulu wa chini.
Mfumo wa uulizaji maswali chanzo
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said Mohamed, akitangaza matokeo hayo leo amesema ongezeko la shule zilizopata daraja E linachangiwa na mabadiliko ya muundo wa mitihani yaliyoanza kutumika mwaka 2024.
Kwa mujibu wake, baraza lilibadilisha mfumo wa uulizwaji wa maswali kutoka kwenye majibu ya kuchagua kwenda kwenye mfumo unaopima uelewa, matumizi ya maarifa na uwezo wa wanafunzi kujibu maswali kwa kutumia ujuzi walioupata.
“Kwa hiyo, baada ya kubadilisha hii format, tumeona sasa mchujo wa shule unavyobainika. Tunaanza kuona zile shule ambazo zina ubora wa chini,” amesema Profesa Mohamed.
Licha ya shule zilizopata daraja E kuongezeka, takwimu za matokeo ya mwaka huu zinaonyesha ufaulu wa jumla umeongezeka hadi asilimia 85.22 mwaka 2026 kutoka asilimia 81.80 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 3.42.
Hata hivyo, Profesa Mohamed amesema licha ya ongezeko hilo, baraza kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu linafanya utafiti kubaini kama shule zinazopata daraja E ni zilezile zinazojirudia kila mwaka au ni shule tofauti.