Necta yatangaza matokeo ya kidato cha nne 2024 ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 3
Arusha. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba, 2024, ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo Januari 23, 2025 amesema kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia tatu kulinganisha na ufaulu wa mwaka 2023.
“Takwimu zinaonesha kuwa ufaulu wa jumla umepanda kwa asilimia tatu na hivyo kufikia asilimia 92.37 ambapo watahiniwa 477,262 kati ya watahiniwa 516,695 wenye matokeo wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza, la pili, la tatu na la nne,” amesema Dk Said.
Mwaka 2023 jumla ya watahiniwa 471,427 sawa na asilimia 89.36 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne waliofaulu mtihani huo.
Kwa mujibu wa Necta, jumla ya watahiniwa wa shule 529,329 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambapo asilimia 98 sawa na watahiniwa 517,460 walijitokeza kufanya mitihani hiyo Novemba 11 hadi 29 mwaka 2024.
Watahiniwa 11,869 sawa na asilimia mbili hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali licha ya kuwa walisajiliwa.
Ubora wa ufaulu waongezeka
Dk Said amewaambia wanahabari kuwa ubora wa ufaulu kwa mwaka 2024 umeongezeka kwa asilimia 5.6 kulinganisha na ule wa mwaka 2023.
Ubora wa ufaulu hupimwa kwa kuangalia idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ambapo kwa mwaka 2024 watahiniwa 221,953 sawa na asilimia 43 walipata madaraja hayo.
Mwaka 2023 waliopata ufaulu wa daraja ya kwanza hadi daraja la tatu walikuwa 197,426 sawa na asilimia 37.4.
Kwa mujibu wa Necta katika kipengele cha ubora wa ufaulu wavulana wamefanya vizuri zaidi kulinganisha wasichana.
“…Wavulana ni 119,869 sawa na asilimia 54 na wasichana 102,084 sawa na asilimia 46 hivyo Wasichana wamefaulu wengi zaidi wakati wavulana wamefaulu vizuri zaidi,”amesema Dk Said.