Serikali yaunganisha mashirika, taasisi 16 za umma, nne zafutwa
- Ni pamoja na iliyokuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Wakala wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
- Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS) zafutwa.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetangaza kuunganishwa kwa mashirika na taasisi 16 ambapo mashirika na taasisi za umma nne zimefutwa ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
Kufutwa au kuvunjwa na kuunganishwa kwa mashirika hayo ni matokeo ya mapendekezo, baada ya tathmini ya utendaji uliofanywa na timu ya wataalamu iliyoundwa na Serikali.
Agosti 19, 2023, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akifungua mkutano wa Wakurugenzi wa mashirika ya umma aliagiza ifanyike tathimini ya kina kwenye mashirika ya umma na yale yasiyo na tija yaondolewe.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo, Ijumaa Desemba 15, 2023, jijini Dar es Salaam amebainisha kuwa sasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Wakala wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) yanaunganishwa na kuunda taasisi moja itakayohusika na utambuzi wa matukio muhimu maishani.
“Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) imeunganishwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), ili kuwepo na taasisi moja itakayohusika na mikopo na ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini,” amesema Mkumbo.
Soma zaidi : Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Taasisi nyingine zinazounganishwa ni Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania, na badala yake itaundwa bodi moja kushughulikia majukumu ya taasisi hizo.
Aidha, Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo ya nyama na maziwa.
“Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMARTEC), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja,” amebainisha Mkumbo.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kitaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje ya nchi.
Sambamba na hilo, Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Mashirika/taasisi zilizovunjwa
Pamoja na mashirika yaliyounganishwa, yaliyofutwa kabisa ni pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS) na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili kuunda Shule ya Sekondari Kibaha na Chuo cha Ufundi.
“Kwa uamuzi huu, Hospitali ya Tumbi Kibaha haitakuwa tena sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha, bali hospitali ya Mkoa wa Pwani,” amesema Mkumbo.
Kwa mujibu wa Mkumbo, tayari Msajili wa Hazina ameshaelekezwa kukamilisha taratibu husika za makabidhiano na Wizara ya Afya.
Mahirika mengine yanayofutwa ni Bodi ya Pareto na shughuli zake zitahamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
Soma zaidi : Ujuzi wa kidijitali unaoweza kuwatoa vijana kimaisha
Hakuna atakayepoteza ajira
Profesa Mkumbo amebainisha kuwa katika mchakato huo hakuna mtumishi atakayepoteza ajira yake na maslahi yao yote yatalindwa na kuzingatiwa kikamilifu.
“Izingatiwe kuwa katika mashirika na taasisi nyingi za umma na Serikali kwa ujumla kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa umma. Kwa hivyo, watumishi wote ambao mashirika na taasisi zao zinaguswa na shughuli hiyo watapangiwa kazi nyingine katika utumishi wa umma na maslahi yao yatazingatiwa ipasavyo,” amesisitiza Mkumbo.
Latest
