Kutoka NIDA hadi Jamii Namba: Safari ya utambulisho wa kidijitali Tanzania
- Jamii Namba ni namba moja ya utambulisho kwa kila Mtanzania, itakayotumika katika huduma zote muhimu.
- Kazi ya kuunda Jamii Namba ilitakiwa ikamilike Desemba 2025.
Dar es Salaam. Mwaka 2023, Serikali ya Tanzania ilitangaza ujio wa ‘Jamii Namba’ iliyobeba matumaini makubwa ya kuboresha maisha ya wananchi katika upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za kijamii.
Jamii Namba ni namba moja ya utambulisho kwa kila Mtanzania, itakayotumika katika huduma zote muhimu. Ilikuwa ni ahadi ya kupunguza usumbufu, urasimu na mkanganyiko wa namba nyingi.
Wakati bado tuko Januari 2026, swali ni moja tu. Mchakato wa Jamii Namba umefikia wapi? wananchi wameanza kuitumia kupata huduma?
Ahadi ya Jamii Namba ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya uzinduzi wa mkongo wa mawasiliano wa baharini Agosti 9, 2023 jijini Dar es Salaam ambapo alizitaka wizara husika kutekeleza kwa wakati mpango huo ili kuepusha ulazima wa kuwa na vitambulisho vingi vyenye taarifa kinzani.
“Niseme na watoa huduma ndani ya Tanzania, mabenki, Wizara ya Elimu inayoandikisha Watanzania wakiwa wadogo, lakini Wizara ya Afya inayotibu Watanzania na wizara nyingine zote zinazotoa huduma, hebu sasa twendeni tukatumie namba moja tu ya Mtanzania.
“Namba moja tu ya Mtanzania. Anapoambiwa Samia Suluhu ni namba 20 ndani ya Tanzania basi taarifa zangu zote, taasisi zote zikivuta namba 20 awe Samia Suluhu mmoja yule yule taarifa zile zile,” alieleza Rais Samia.
Pia agizo hilo limekuwa likirudiwa na watendaji wa Serikali kwa nyakati tofauti katika majukwaa mbalimbali ili kutekeleza agizo la Rais.
Namba Jamii itatumika kupata huduma za afya, elimu, bima, benki, ajira na huduma za Serikali. Lengo ni kuondoa utegemezi wa namba nyingi kama ya kuzaliwa, Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Namba ya Mlipa Kodi (TIN), Bima ya Afya (NHIF) na nyinginezo.

Kitambulisho cha Taifa, kinamwezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali za kijamii. Ujio wa Jamii Namba huenda ukamilisha zaidi utambulisho wa Kila Mtanzania na kuchangia katika shughuli za maendeleo. Picha | NIDA.
Ujenzi wa Jamii Namba umekamilika?
Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA Wizara ya Fedha, Dk John Sausi akizungumza katika mkutano wa taasisi za kifedha jijini Arusha Machi 08, 2024 alisema kazi ya kuunda Jamii Namba ingekamilika Desemba 2025.
“Tunavyoongea sasa hivi (Machi 8, 2024) tayari wataalamu wameshamaliza kuandaa muundo wa namba hiyo, hii inafanyika kwa mashirikiano kati ya RITA, NIDA na Zanzibar ID. Tunategemea kazi hii itaisha mwishoni mwa mwaka 2025,” alieleza Dk Sausi.
Hata hivyo, kazi hiyo bado haijakamilika kama ilivyoahidiwa na hakuna taarifa rasmi za kuanza kutumika kwa namba hiyo mpaka January 2026.
Nini kimefanyika mpaka sasa?
Hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ikishirikiana na wadau ili kutimiza ahadi hiyo muhimu kwa Watanzania. Serikali imeamua kutumia Namba ya NIDA kama msingi wa Jamii Namba.
Aliyekuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akifunga Kongamano la Nane la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) jijini Dar es Salaam Oktoba 18, 2024 alieleza wazi kuwa NIDA ndiyo itakuwa mhimili wa mfumo huu mpya wa utambulisho.
“Serikali imeelekeza kuwa namba ya NIDA ndiyo namba jamii itakayotumika katika utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali hapa nchini. Kwa msingi huo, niwahimize Watanzania wenzangu kuhakikisha wanapata namba ya NIDA ambayo ndiyo namba jamii,” alisema Majaliwa.
Majaliwa alisema namba hiyo itawezesha mifumo kusomana, na kufanya iwe rahisi kupata huduma mahali popote, ikiwemo kununua tiketi, huduma za kifedha, na ununuzi wa bidhaa.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeongeza juhudi za kutoa vitambulisho. Serikali imenunua magari na vifaa vipya ili kufikia wananchi wengi zaidi na kupunguza malalamiko ya muda mrefu ya foleni na ucheleweshaji wa kadi.
Serikali pia imeanza mkakati wa kusajili watoto chini ya miaka mitano katika mfumo wa utambulisho wa Taifa kwa kutumia alama za nyayo zao. Hii ni hatua muhimu kwa Jamii Namba ili kurahisisha utoaji huduma kwa makundi yote kwenye jamii.
Licha ya hatua hizo, mchakato wa utekelezaji wa Jamii Namba huenda ukachukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa awali.
Kibarua kilichopo mbele
Wananchi bado wanatumia namba tofauti wanapohitaji huduma tofauti. Pili, changamoto za usahihi wa taarifa bado zipo. Kumekuwepo ripoti za majina yanayojirudia, taarifa zisizokamilika na tuhuma za udanganyifu katika baadhi ya usajili wa NIDA.
Ili Jamii Namba ifanye kazi, mifumo ya taasisi za umma na binafsi lazima iunganishwe. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kujenga mfumo wa Jamii X-Change kwa ajili ya kubadilishana taarifa.
Hata hivyo, utekelezaji wake bado haujaenea nchi nzima, hasa vijijini ambako mtandao na mifumo ya Tehama ni dhaifu.
Changamoto nyingine kubwa ni upande wa sheria. Tanzania ina Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2023, lakini bado utekelezaji wake sio wa kuridhisha.
Baadhi ya wadau likiwemo shirika la Media and Tech Convergence (TMC) katika ripoti yake ya mwaka 2025 wanaeleza kuwa bila usimamizi imara wa data, wananchi wanaweza kupoteza imani na mfumo huo mpya.
Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa nchi za Afrika zilizopiga hatua katika utambulisho wa kidigitali ikiwemo Kenya ambapo mpango wa Maisha Namba unampa kila raia namba moja ya utambulisho inayorahisisha kupata huduma za Serikali na kupunguza urasimu.
Ghana kupitia GhanaCard imefanikiwa kuunganisha utambulisho na huduma muhimu kama benki, afya na uchaguzi. Mifumo hii imeongeza ufanisi, uaminifu na ushirikishwaji wa wananchi.

Wakati Watanzania wakiendelea kusubiri kukamilika kwa mchakato wa uundaji wa Jamii Namba, wanakumbushwa kuendelea kujisajili na kupata vitambulisho vya Taifa. Picha | NIDA.
Nini kifanyike?
Ili kutimiza dhamira ya Jamii Namba, TMC inapendekeza kurekebisha na kuoanisha mfumo wa kisheria kwa kufanya marekebisho ya sheria zilizopo na kuanzisha Sheria Maalum ya Utambulisho wa Kidijitali ili kuunga mkono mfumo mmoja wa utambulisho, kuhakikisha ulinganifu na ulinzi wa taarifa.
Shirika hilo linasema uzinduzi wa miradi ya majaribio ya Jamii Namba ufanyike ili kupima ufanisi wake kabla ya utekelezaji wa kitaifa. Hii itasaidia kupima, kuboresha, na kukusanya mrejesho, kuhakikisha mfumo unakidhi mahitaji ya jamii. Utekelezaji mfumo wa utambulisho huru wa mtumiaji (Self-Sovereign Identity – SSI) ili kuwawezesha wananchi kudhibiti vitambulisho vyao vya kidijitali, kuwezesha kushirikisha taarifa kwa hiari na kulinda faragha.
Kipaumbele pia kiwekwe kuzuia udanganyifu na kuimarisha usalama wa mtandao ikiwemo matumizi ya akili bandia kugundua mienendo isiyo ya kawaida na teknolojia ya blockchain, ili kuzuia udanganyifu, uvujaji wa taarifa, na matumizi yasiyoidhinishwa.
Ili Jamii Namba ifanikiwe, watunga sera, taasisi za Serikali, na wadau wa sekta binafsi wanapaswa kushirikiana kwa karibu kutekeleza mapendekezo hayo.
Kwa kuchukua hatua madhubuti za marekebisho ya sheria, uwekezaji wa miundombinu, na uimarishaji wa usalama wa mtandao, Tanzania inaweza kujenga mfumo salama, wenye ufanisi, na jumuishi wa utambulisho wa kidijitali utakaoboresha utoaji wa huduma na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
Latest