Rais Samia anavyoendelea kuyakomalia mashirika ya umma Tanzania

August 29, 2024 6:19 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ayataka kuongeza ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa ndani na kuvuka mipaka ya Tanzania.
  • Mashirika yatakiwa kufanya maamuzi ya busara na kuepuka miradi isiyo na tija.

Dar es Salaam. Mapema Agosti 28 wakati Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anafungua mkutano wa viongozi na watendaji wa mashirika ya umma jijini Arusha alionekana kuendeleza jambo lake. 

Jambo hilo ni uwepo wa mashirika lukuki ya umma yanayojiendesha kwa hasara kiasi cha kuendelea kunyonya mapato ya Serikali yanayotokana na walipa kodi ili kuendesha shughuli zao. 

Tangu aingie madarakani, Rais Samia na Serikali wamekuwa wakisaka mikakati madhubuti itakayosaidia kuongeza ufanisi ndani mashirika ya umma ikiwemo kuyapunguza au kuyaunganisha baadhi yaliyokuwa na shughuli zinazofanana. 

Katika hotuba yake ya Jumatano, Rais Samia alieleza kuwa kunahitajika mageuzi makubwa ndani ya mashirika ya umma kwa kuwa Serikali imewekeza kati ya Sh76 trilioni na Sh77 trilioni. 

“Tunaposisitiza mabadiliko, ufanisi, mashirika yachangie na yalete faida ni kulinda rasilimali za wananchi ambazo zimewekezwa ndani ya mashirika hayo…yameundwa ili Serikali ipate nusra ya kwenda kutafuta fedha nje ili mashirika yachangie na mambo yaende vizuri,” amesema Rais Samia.

Baadhi ya mashirika ya umma ya kibiashara kama Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Shirika la simu Tanzania (TTCL) kwa nyakati tofauti ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikibainisha kuwa yamekuwa yakipata hasara kwa miaka isiyopungua mitano sasa.

Rais Samia alieleza kuwa Afrika kuna nchi kama Angola, Botswana, na Mauritius zinaongoza katika kufanya biashara nje ya nchi zao na Tanzania inahitaji kujiunga na mkondo huo ili kukua kiuchumi.

Katika miaka mitatu ya utawala wake alimteua aliyekuwa bosi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Nehemiah Mchechu kuwa Msajili wa Hazina kusimamia mashirika hayo ambaye amekuwa akishinikiza mabadiliko makubwa.  

Desemba mwaka jana Serikali iliyafuta mashirika manne ya Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS) ,Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Shirika la Elimu Kibaha (KEC) pamoja na Bodi ya Pareto na kuyaunganisha mengine 16.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama kwa ajili ya kuimba wimbo wa taifa pamoja na viongozi na watendaji wakuu wa mashirika na taasisi mbalimbali za umma. Picha| Ikulu.

Mabadiliko yaanza kulipa

Kwa mujibu wa Rais Samia sehemu ya mabadiliko hayo imeanza kulipa baada Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ambalo awali lilikuwa likisuasua na kuingiza hasara, lakini mwaka wa fedha uliopita lilipata faida na kutoa gawio la Sh9 bilioni kwa Serikali. 

“Kwa nini kila siku tuchukue serikalini wakati mashirika yametengenezwa yazalishe, tujitegemee tusimame, angalau kwa hatua ya kwanza jitegemee tu kama TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania), lipa mishahara yako, gharama zako, utakua polepole utafika pahali uweze kufanya faida kubwa na utoe gawio serikalini,” amesema Rais Samia

Kwa mujibu wa Rais Samia shirika la TPHPA lililoundwa kwa kuunganisha Taasisi ya Viuatilifu vya Ukanda wa Kitropiki na Kitengo cha Huduma za Afya ya Mimea limeiwezesha Tanzania kupata vyeti vya viwango vya kimataifa na kuanza kutoa gawio serikalini.

Hata hivyo, ameonya kuwa si mashirika yote yanastahili kuendelea kuwepo ikiwa hayazalishi kwa tija akitolea mfano wa Kampuni ya Maendeleo ya Taifa (NDC) kuwa ni miongoni ya yasiyofanya vema. 

“Shirika tuliloliunda wenyewe kama halifanyi vizuri basi liondoke tu, hatuwezi kwenda kulinda nafasi za watu na mashirika hayazalishi, hayana tija haiwezekani, madhumuni yetu mashirika yafanye kazi,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo wa juu wa nchi amesisitiza umuhimu wa mashirika ya umma kufanya tafiti za kutosha kabla ya kuanzisha uwekezaji ili kuhakikisha faida inarudishwa na kutoa wito kwa mashirika hayo kufanya maamuzi ya busara ili kuepuka miradi isiyo na tija aliyoiita ‘ghost investments’ (Miradi hewa) ambayo imekwama na haijarudisha pesa za wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks