Undani bajeti ya Serikali 2023-24
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta jambo na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, baada ya kuwasilishwa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, ukumbi wa Pius Msekwa, bungeni jijini Dodoma.
- Serikali ya Tanzania inapanga kutumia Sh44.3 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2023/24.
- Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh31.4 trilioni sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.
- Sh10.9 trilioni ni kwa ajili ya mishahara ikiwemo upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inapanga kutumia Sh44.3 trilioni katika mwaka wa fedha wa 2023/24 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7 ya bajeti ya mwaka huu.
Bajeti hiyo inajumuisha Sh29.2 trilioni sawa na asilimia 65.5 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kiasi kilichobaki kitaelekezwa katika shughuli za maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha kwa wabunge Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, Machi 13 amesema bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 7 ikilinganishwa na bajeti ya 2022/23 ya Sh41.5 trilioni.
Mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh31.4 trilioni sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote.
Kati ya mapato hayo, mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 13 hadi Sh26.7 trilioni kutoka makadirio ya Sh23.7 trilioni mwaka 2022/23.
“Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo inatarajiwa kufikia Sh5.4 trilioni, sawa na asilimia 12.3 ya bajeti yote,” amesema Dk Nchemba.
Dk Nchemba amesema Serikali inatarajia kukopa Sh5.4 trilioni kutoka soko la ndani ambapo Sh3.5 triioni ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh1.9 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Pia Serikali inatarajia kukopa Sh2.1 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Soma zaidi: Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
Matumizi yatakua hivi
Dk Nchemba amesema kuwa kati ya fedha hizo, Sh29.2 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha Sh12.8 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za Mfuko Mkuu.
Pia matumizi ya kawaida yatajumuisha Sh10.9 trilioni kwa ajili ya mishahara ikiwemo upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya, na Sh6.4 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC).
“Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh15.1 trilioni ambapo kati ya kiasi hicho, Sh11.9 trilioni ni fedha za ndani, sawa na asilimia 78.3 ya bajeti ya maendeleo na Sh3.2 trilioni ni fedha za nje,” amesema.
Dk Nchemba amesema kuwa ukomo wa fedha za maendeleo upo ndani ya wigo wa kati ya asilimia 30 na 40 ulioanishwa kwenye Mpango Elekezi wa Muda Mrefu (2011/12 – 2025/26).
Pia utengaji wa fedha za maendeleo umezingatia miradi inayoendelea ikiwemo miradi ya kimkakati na ya kielelezo pamoja na utekelezaji wa miradi kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi ya maendeleo kwa utaratibu uliozoeleka.
“Aidha, bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kufuatia kukamilika kwa miradi ya maendeleo hususan kwenye sekta za huduma za jamii ambazo kwa sasa zinahitaji fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji”, amesema Nchemba.
Mikakati kutunisha bajeti ya Serikali
Serikali inatarajia kuongeza ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha wa 2023/24 ili kugharamia sehemu kubwa ya matumizi yake na kuendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 pamoja na sheria nyingine kwa lengo la kubana matumizi na kuelekeza fedha kwenye utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa.
Kwa mujibu wa waziri huyo, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 pamoja na Mfumo na Ukomo na Bajeti ya mwaka 2023/24, unatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuimarisha sekta za uzalishaji.
Hiyo itasaidia kutoa mchango zaidi katika ukuaji wa uchumi, kuongeza mapato ya Serikali, fursa za ajira na maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kijamii kama vile elimu, afya, maji na barabara.
Latest
