Bajeti ya Tanzania 2022-23 yafikia Sh41.48 trilioni
- Asilimia asilimia 36.2 ya bajeti yote itatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
- Bajeti hiyo imeongezeka kwa zaidi ya Sh3 trilioni ndani ya mwaka mmoja.
Dar es salaam. Serikali ya Tanzania inapanga kukusanya na kutumia Sh41.48 trilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23 ikiwa ni ongezeko la Sh3.5 trilioni kutoka bajeti inayoishia Juni mwaka huu huku takriban theluthi mbili ikitumika kwa ajili
Katika mwaka wa fedha wa fedha 2021/22 unaoishia mwezi huu, Serikali inakadiria kukusanya na kutumia Sh37.98 trilioni.
Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango amewaeleza wabunge kuwa kati ya fedha wanazopendekeza katika mwaka ujao wa fedha, Sh26.48 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 63.8 ya bajeti yote huku matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh15 trilioni.
Kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kuanzia Julai 2022 ni sawa na asilimia 36.2 ya bajeti yote ambayo imesomwa bungeni leo.
Katika matumizi ya kawaida, Dk Nchemba amesema Sh11.5 trilioni zitatumika kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali na gharama nyingine za mfuko mkuu huku Sh9.8 trilioni ni kwa ajili ya mishahara pamoja na nyongeza ya mshahara na upandishaji wa madaraja kwa watumishi na ajira mpya.
Dk Mwigulu ameongeza kuwa Sh5.3 trilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ikijumuisha Sh200 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi na wazabuni.
Fedha za Matumizi ya maendeleo zitatumika wapi
Kupitia hotuba hiyo ya bajeti aliyeisoma kwa saa 2:28, waziri huyo amesema katika Sh15 trilioni zinazokusudiwa kutumika katika miradi ya maendeleo, Sh1.1 trilioni itatumika kugharamia mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge na Sh1.4 trilioni kwa ajili ya kugharamia mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere.
Mbunge huyo wa Iramba Magharibi ameongeza kuwa Sh1.1 trilioni inakusudiwa kutumika kwa ajili ya mfuko wa barabara na Sh944.1 bilioni kwa ajili ya mifuko ya reli, maji na REA pamoja na Sh570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
“Kati ya kiasi hicho kilichopangwa kwa ajili ya maendeleo, Sh12.31 trilioni ni fedha za ndani sawa na asilimia 82 ya bajeti ya maendeleo na Sh 2.7 trilioni ni fedha za nje,” amesema Dk Nchemba.
Pesa zitatoka wapi?
Serikali inakusudia kupata ya Sh28 trilioni kutoka kwenye mapato yake ya ndani ambapo kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanakusudia kupata Sh23.6 trilioni huku kupitia mapato yasiyo ya kikodi wakitarajia kukusanya Sh3.3 trilioni.
Kwa mara ya kwanza, mapato ya halmashauri yamefikia Sh1 trilioni yakivuka ngazi ya bilioni kwa miaka yote.
Aidha kupitia misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo Serikali inakusudia kupata Sh4.6 trilioni na kupitia mikopo ya ndani na nje Serikali inakusudia kupata Sh8.8 trilioni.
Latest