Serikali kuwarejesha Watanzania waliopo Israel, Iran
- Ni kufuatia mashambulizi ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili yanayozidi kuongezeka siku hadi siku.
- Mpaka sasa Watanzania wote waliopo maeneo hayo wapo salama na tayari baaadhi wameanza kujiandikisha kurejea.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeanza mchakato wa kuwarejesha nyumbani raia wake walioko nchini Israel na Iran, kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi baina ya mataifa hayo mawili.
Tangu Juni 13, 2025, hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati imezidi kuwa tete, kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya anga na kulipiza kisasi kati ya Tehran na Tel Aviv.
Mashambulizi hayo yalianza mara baada ya Israel kuanzisha ilichokiita oparesheni ya kuzuia uzalishaji wa silaha za nyuklia nchini Iran (Operation Rising Lion) iliyosababisha vifo vya makamanda wa juu wa Jeshi la Iran pamoja na wataalamu wa nyuklia.
Iran imejibu mashambulizi kwa makombora nchini Israel na kuanzisha vita na kugharimu maisha ya watu zaidi ya 200 nchini Iran na 24 Israel
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Watanzania waliopo katika nchi hizo wapo salama kwa sasa, huku taratibu za haraka za kiutendaji zikianza kuchukuliwa ili kuhakikisha wanarejea nyumbani salama.
Hadi sasa, wizara hiyo imesema kuna Watanzania 168 nchini Iran wakiwemo wanafunzi 134 wanaosoma mjini Qom na wengine 34 walioko Tehran kwa shughuli mbalimbali.
50 wajiandikisha kurudi Tanzania
Kwa upande wa Israel, takriban Watanzania 200 wapo nchini humo, wakiwemo wafanyakazi wa ubalozi, wanafunzi na wataalamu wa taaluma mbalimbali ambapo kati yao, 50 tayari wamejiandikisha kurejea nchini.
Mapema jana asubuhi (Juni 19, 2025) Iran ilishambulia kwa makombora eneo la Ramat Gan ambalo lipo karibu na balozi mbalimbali ukiwemo Ubalozi wa Tanzania uliopo jijini Tel Aviv nchini Israel.
Taarifa hiyo imesema jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Israel halikuaathirika na mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran.
“Wakati mashambulizi hayo yalipotokea, hapakuwa na mtu yeyote ndani ya jengo hilo, na maafisa wa ubalozi pamoja na familia zao wote wapo salama,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa jioni ya Juni 19, 2025.
Balozi za Tanzania nchini Misri, Israel, Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo ndipo Iran inawakilishwa kidiplomasia zimeelekezwa kusimamia orodha ya Watanzania waliopo maeneo hayo na kuratibu mipango ya usafiri wao wa kurejea.
Tukio hili linajitokeza chini ya miaka miwili tangu Watanzania wawili, waliokuwa masomoni nchini Israel, kupoteza maisha baada ya kushambuliwa na kundi la Hamas mwezi Oktoba mwaka 2023.
Mashambulizi hayo yalianza baada ya Hamas kuvuka mpaka kutoka Gaza na kushambulia maeneo ya kusini mwa Israel, hatua iliyozua vita kati ya Israel na Palestina.
Hata hivyo, Serikali imeelekeza Watanzania walioko katika maeneo hayo kuchukua tahadhari zote za kiusalama.
Hatua hii ya Tanzania imekuja wakati ambapo jumuiya ya kimataifa inatoa wito wa utulivu, huku baadhi ya nchi ikiwemo China tayari zimetoa maelekezo kwa raia wao kuondoka haraka katika maeneo yaliyoathiriwa.Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuwarejesha raia wake katika maeneo yanayotokea vita kama ilivyofanya mwaka 2022 nchini Ukraine na Sudan Kusini mwaka 2023.
Latest
