Vita vya Iran inavyoweza kuathiri uchumi wa Tanzania

March 2, 2026 6:00 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Huenda bei ya bidhaa ikapanda kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
  • Wachambuzi wa uchumi wasema hali hiyo itatokea iwapo vita itadumu kwa muda mrefu. 
  • Kutokana na kufungwa kwa baadhi ya viwanja vya ndege vya kimataifa, Tanzania inaweza kuathirika katika uuzaji wa dhahabu ambayo soko lake kubwa liko Dubai.

Dar es Salaam. Mwishoni mwa wiki iliyopita dunia imeshuhudia mapigano makali yanayoendelea Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyofanyika Februari 28, 2026.

Mashambulizi hayo ya anga yaliilenga Tehran, mji mkuu wa Iran, na kusababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1989 huku takriban maafisa 40 wakipoteza maisha, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Iran.

Katika kulipiza kisasi, Iran ilitangaza kushambulia maeneo kadhaa katika Ghuba ya Uajemi, ikilenga miji ya Dubai na Abu Dhabi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambaye ni mshirika wa Marekani pamoja na kushambulia miundombinu ya kijeshi ya Marekani katika nchi za Bahrain, Qatar na Kuwait.

Hata hivyo, mbali na athari za kibinadamu na mvutano wa kidiplomasia kwa mafahari hao, mapigano hayo pia yamesababisha kusimama kwa shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo kusitishwa kwa maelfu ya safari za ndege kutokana na kufungwa kwa viwanja vya ndege vya kimataifa vya Dubai, Abu Dhabi na Doha.

Athari nyingine zimeanza kuonekana katika soko la dunia hususan katika mafuta ambayo ni kiashiria kikubwa cha kasi ya mfumuko wa bei na uimara wa uchumi wa nchi zinazoagiza nishati hiyo kutoka nje kama Tanzania. 

Bei ya mafuta yapanda soko la dunia

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la habari la Reuters, bei ya mafuta imepanda kwa asilimia 9 baada ya njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Hormuz kuathiriwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran.

Bei ya mafuta ghafi ya Brent ilipanda hadi kufikia Dola 82.37 kwa pipa moja Machi 2, 2026, sawa na ongezeko la asilimia 13 la bei, kiwango cha juu zaidi kurekodiwa tangu Januari 2025.  Bei hiyo ilishuka kidogo hadi Dola za Marekani 79.78 kwa pipa saa chache badae. 

Inakadiriwa kuwa takriban moja ya tano ya mafuta yanayohitajika duniani kutokea Saudi Arabia, UAE, Iraq, Iran, na Kuwait husafiri kupitia njia bahari ya Hormuz, zikibeba dizeli, mafuta ya ndege, petroli. Picha | DW.

Hali hiyo inatokana na mfululizo wa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyopelekea kuharibiwa kwa takriban meli tatu za mafuta na kusababisha changamoto ya usafirishaji kupitia njia au mlango bahari wa Hormuz unaounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Uarabuni.

Inakadiriwa kuwa takriban moja ya tano ya mafuta yanayohitajika duniani kutokea Saudi Arabia, UAE, Iraq, Iran, na Kuwait husafiri kupitia njia bahari ya Hormuz, zikibeba dizeli, mafuta ya ndege, petroli na bidhaa nyingine kutoka kwenye viwanda vyao kwenda sokoni.

Kuongezeka kwa hatari za kijeshi katika eneo hilo huongeza gharama za mafuta ghafi katika soko la dunia kutokana na kuongezeka kwa gharama za bima ya meli, na kuvurugika kwa ratiba za usafirishaji jambo ambalo lina athari kubwa kwa nchi zinazoagiza mafuta kwa wingi kama Tanzania.

Tanzania na utegemezi wa mafuta kutoka nje

Kama ilivyo kwa mataifa mengi yanayoendelea, Tanzania hulazimika kuagiza mafuta ikiwemo petroli, dizeli na mafuta ya ndege ili kuendesha sekta ya usafirishaji, viwanda, uzalishaji wa umeme katika baadhi ya maeneo, na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi. 

Kwa Tanzania nishati hiyo ndiyo mhimili wa uchumi katika kusafirisha chakula kutoka mashambani, huendesha mitambo viwandani na kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo.

Kwa mujibu wa ripoti ya fedha iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Huduma za Maji (EWURA) ya mwaka 2023/2024, Tanzania iliingiza zaidi ya lita bilioni 4.3 za mafuta kutoka nje huku matumizi yakiongezeka kwa asilimia 10.9 kulinganisha na mwaka uliopita.

Kwa Tanzania kutegemea zaidi kuagiza mafuta kutoka nje ni kiashiria kwamba mabadiliko yoyote ya bei za mafuta katika soko la dunia yanaweza kuleta athari za moja kwa moja katika uchumi. Picha | TASAC.

Mafuta ni miongoni mwa bidhaa zinazoongoza kwa thamani ya uagizaji, zikichukua zaidi ya asilimia 20 ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje katika miaka ya karibuni.

Hii ni kiashiria kwamba mabadiliko yoyote ya bei za mafuta katika soko la dunia au migogoro katika maeneo yanayozalisha nishati yanaweza kuleta athari za moja kwa moja katika uchumi.

Ripoti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa hata wakati bei kuu ya mafuta ilipokuwa ikipungua mwaka 2025, sehemu kubwa ya mfumuko wa bidhaa za bidhaa na huduma ulichangiwa na shinikizo kutokana na athari katika soko la dunia.

Huenda bei za bidhaa zikapanda

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa iwapo vita hiyo itaendelea kwa kipindi kirefu, bei ya mafuta katika soko la dunia itazidi kupanda kama ilivyoanza kuonyesha dalili siku mbili baada ya kuanza mapigano. 

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Alfred Kinyondo ameiambia Nukta Habari kuwa bidhaa zinaweza kupanda bei kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji katika katika shughuli muhimu za kiuchumi kama vile viwanda na usafirishaji.

“Mafuta ni bidhaa muhimu sana kwenye uchumi…mafuta yakipanda bei karibu kila kitu kingine kinapanda bei,” amesema Prof Kinyondo.

Kufuatia kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji kunakotokana na kupanda kwa bei ya mafuta, bei ya bidhaa inaweza kjuongezeka. Picha | Habari Leo.

Athari za kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, amesema, haziwezi kuonekana mara moja nchini isipokuwa kama vita hiyo itadumu kwa muda mrefu kwa kuwa Tanzania hununua mafuta ya kutosha kwa kipindi cha miezi mitatu.

Akizungumzia kuhusu kusitishwa kwa safari za ndege na kufungwa kwa baadhi ya viwanja vya ndege vya kimataifa, Prof Kinyondo amesema Tanzania inapoteza mapato husasan kutokana na kusimama kwa biashara ya madini ya dhahabu ambayo soko letu kubwa lipo Dubai.

“Madini yanachangia asilimia 10.5 kwenye pato letu la Taifa, lakini katika asilimia hizo dhahabu inachangia asilimia nane,” amefafanua Prof Kinyondo. 

‘Vita ya kiuchumi’

Wakati athari mbalimbali za kiuchumi zikiendelea kujitokeza katika sekta na maeneo tofauti ulimwenguni, historia inaonyesha kuwa hii si mara ya kwanza kwa Marekani kuishambulia Iran na kuingia katika mzozo.

Wachambuzi wanautaja mgogoro huo kama vita ya kiuchumi licha ya maidai ya Trump ya kuwakomboa wananchi wa Iran kutoka utawala anaodai kuwa ni mbovu. Picha | Financial Times.

Juni 2025 Israel na Marekani waliishambulia Iran kwa makombora ili kudhoofosha nguvu zake za nuklia. Mwaka 2020, Marekani iliishambulia Iran na kufaniikisha kumuua kamanda wa juu wa kijeshi wa Taifa hilo Jenerali Qasem Soleimani mgogoro ambao licha ya kusababisha athari nyingine, bei ya mafuta ilipanda kwa takriban asilimia 4.5 ndani mwaka mmoja. 

Licha ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudai kuwa anaishambulia Iran kwa lengo la kuwakomboa wananchi wake kutoka kwenye utawala anaodai kuwa sio wa haki wachambuzi wana maoni tofauti.

Efron Mkungilwa, Mchambuzi wa siasa za kimataifa ameiambia Nukta Habari kuwa madai ya Trump ni propaganda ya vita akibainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Marekani ni vita ya kiuchumi hususan udhibiti wa soko la mafuta. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks